Mbeya. Ili kumaliza tatizo la ajali mkoani Mbeya, Jeshi la Polisi limesema litaanzisha operesheni maalumu kuwabaini na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waendesha vyombo vya moto wasio na leseni. Hatua hii inakuja kufuatia kushirikiana na Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) mkoani humo kuanzisha mafunzo ya udereva wa awali yatakayodumu kwa mwezi mmoja.
Mkoa wa Mbeya umekuwa ukitajwa kinara kwa ajali, ikiwemo tukio la Juni 7, 2025 mteremko wa Iwambi lililoua 28 na kujeruhi saba likihusisha magari matatu.
Akifungua mafunzo hayo leo Machi 13, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema hawatamuhurumia yeyote atakayekiuka sheria za usalama barabarani. “Wapo wahalifu wanaendesha vyombo bila leseni na kujihalalisha kuwa madereva. Tumeanzisha mafunzo ya mwezi mmoja kwa ajili ya kutoa elimu kabla ya kuanza operesheni hiyo,” amesema.
Kuzaga ameongeza kuwa ujumbe wa elimu umeshirikisha makundi yote, lakini baadhi ya madereva wa bodaboda, guta na kirikuu hawakujitokeza. “Tutahakikisha hakuna wahalifu kuingia barabarani. Lengo letu ni usalama wa raia na mali zao,” amesema.
Watumishi wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama jijini Mbeya wakiwa katika mafunzo ya udereva wa awali yaliyoanza leo Machi 13 yakidumu kwa mwezi mmoja.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amelipongeza Jeshi la Polisi na kusisitiza kuwa mafunzo hayo yawafikie pia wakazi wa vijijini. Pia aliridhishwa na juhudi za Veta kupunguza gharama ya mafunzo kutoka Sh210,000 hadi Sh105,000, hatua inayolenga kuwafikia watumiaji wengi wa barabara.
Kwa upande wake, Hezron Mkangi, Mkuu wa Usalama Barabarani wilayani Mbeya, amesema jumla ya washiriki 160 wanashiriki mafunzo hayo, yanayolenga kuboresha uelewa wa sheria za barabarani.
Mbunge wa Mbeya Mjini na Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Patrick Mwalunenge, ameomba makundi yote yakiwamo bodaboda na bajaji kufikiwa na mafunzo hayo, akisisitiza kuwa ajali zinapunguza nguvu kazi na kuongeza umaskini.
Mmoja wa washiriki, Mediana Masota, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuwa madereva bora na salama wawapo barabarani.