MITI 1,500 YAPANDWA SHULE YA MSINJAHILI KUELEKEA SIKU YA MISITU DUNIANI

Jumla ya miti 1,500 ya matunda na kivuli imepandwa leo katika Shule ya Msingi Msinjahili, Manispaa ya Lindi, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kujiandaa na maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani pamoja na Wiki ya Upandaji Miti Kitaifa itakayofanyika mkoani Lindi.

Zoezi hilo limeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, ambaye amewahimiza wananchi, wanafunzi na taasisi mbalimbali kuendelea kushiriki kikamilifu katika kampeni ya upandaji miti ili kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mwanziva amesema kuwa miti ina mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira, kuboresha hali ya hewa na kutoa manufaa mbalimbali ikiwemo matunda, kivuli na malighafi muhimu kwa jamii. Amesisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kupanda na kuitunza miti ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Akieleza kuhusu kampeni ya upandaji miti pamoja na maandalizi ya maadhimisho ya upandaji miti kitaifa, Saimoni Kipeleja kutoka Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili na Utalii amesema serikali inaendelea kuhamasisha upandaji miti nchini kama sehemu ya mkakati wa kuongeza uoto wa asili na kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Kipeleja amesema kuwa maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, taasisi, wanafunzi na wananchi kwa lengo la kuhamasisha upandaji miti na kuimarisha juhudi za uhifadhi wa misitu.

Awali, Mhifadhi wa Wilaya ya Lindi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Gaspar Vicent, amesema taasisi hiyo imekuwa ikizalisha miche ya miti zaidi ya laki mbili kila mwaka na kuigawa kwa taasisi mbalimbali pamoja na watu binafsi ili kuongeza kasi ya upandaji miti katika jamii.

Vicent amebainisha kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa ipasavyo ili kufikia malengo ya kuongeza uoto wa asili na kulinda rasilimali za misitu. Zoezi hilo la upandaji miti limehudhuriwa na viongozi wa serikali, walimu, wanafunzi pamoja na wadau wa mazingira. 

Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya upandaji miti Kitaifa yanaenda sambamba na Kauli mbiu isemayo Misitu ni uchumi endelevu,Tuhifadhi kwa Maendeleo ya Taifa.