Kigoma. Wananchi, watumishi na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma wameanza kuwasili katika kiwanja cha mpira cha Kazegunga huku maandalizi yakiendelea kwa ajili ya shughuli ya kuaga miili ya watu saba waliokufa kwenye ajali ya boti.
Ajali hiyo ya boti ilitokea jana Machi 13, 2026 katika kijiji cha Kalalangabo, watumishi hao wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wakiwamo na wengine watatu walikuwa kwenye majukumu yao kazi.
Ajali hiyo ilitokea saa 2 asubuhi, baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Kigoma Mjini kwenda Kijiji cha Kagunga kupinduka na kuzama kutokana na upepo mkali ndani ya Ziwa Tanganyika walipokuwa wakienda kwa shughuli ya usimamizi shirikishi kwenye vituo vya afya na kuhamasisha Bima ya Afya kwa Wote.
Wakizungumza leo Jumamosi, Machi 14, 2026 kwenye kiwanja inakoagwa miili hiyo, baadhi ya watumishi na wananchi na viongozi, wamesema wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na kwamba kinachowahuzunisha zaidi waliopoteza maisha ni vijana wadogo ambao walikuwa bado na ndoto zao za kutimiza.
Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Peter Farayo amesema bado hadi sasa hajaamini kama watumishi wenzake wamefariki dunia na watawakumbuka kwa mengi mema wakati wa uhai wao.
“Nimepokea taarifa hizi kwa masikitiko makubwa vifo vya watumishi wenzetu tunaziombea roho zao zipumzike kwa amani na Mungu awape faraja na subira kwa familia zao,” amesema.
Mkazi wa Kagegunga, Rashid Abdul amesema sio rahisi nafasi zao kuzibika kwani wamekuwa wakijitoa kulitumia Taifa lao, ila kwake watumishi hao wamekufa kishujaa kwa nchi yao.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kiza Mayeye amesema alipokea msiba huo kwa mshtuko mkubwa akiwa Dodoma na watumishi hao ni vijana walikutwa na mauti wakiwa njiani kwenda kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Amesema kinachomuumiza zaidi ni kwamba msiba huo umekuja katika kipindi ambacho jimbo lake lina kwamba hao waliokuwepo wamepungua, tena kwa idadi kubwa.
“Msiba hauzoeleki hata kidogo tumepoteza nguvu kazi ni msiba mkubwa sana kwetu kama jimbo, mkoa na Taifa, tunawaombea faraja ndugu, jamaa na marafiki,” amesema Mayeye.
Miili hiyo inayotarajia kuagwa leo ni watumishi wanne ambao ni pamoja na Muuguzi msaidizi, Paul Luvanda (29), Katibu wa afya, Rachel Msalila (28), Tatibu wa kinywa na meno, Joyce Kandole (29), Mfamasia, Winny Nyabusani ( 31).
Pia wamo watatu ambao walikuwa wasaidizi wa shughuli ya uandikishaji Bima ya Afya kwa Wote waliotambulika kwa jina moja moja ambao ni Erick, Omary na Geofrey ambaye alikuwa dereva bodaboda.
Mtumishi mwingine wa afya Amos Sika (33), ambaye ni Tatibu na mwili wake haujapatikana hadi sasa na juhudi za kumtafuta zinaendelea,
Watumishi hao wanatarajia kusafirishwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya taratibu za mazishi katika wilaya za Chunya na Mbarali (Mbeya), Mpwapwa (Dodoma), Temeke (Dar es Salaam) na Butiama (Mara).
