Dar es Salaam. Siku moja baada ya Tume za Rais kuhusu mgogoro wa ardhi na uhamaji wa hiari Ngorongoro kukabidhi ripoti zake, wadau wa sheria na haki za binadamu wametoa maoni tofauti kuhusu maudhui yake, baadhi wakipongeza na wengine wakionyesha mapungufu.
Wanaopongeza, wanasema ripoti zimependekeza mambo yanayogusa yaliyokuwa yanalalamikiwa, ikiwemo mabadiliko ya sheria, kutambua makosa wakati wa mchakato wa uhamishaji wananchi na kuanzishwa chombo cha utatuzi migogoro.
Wadau wengine, wanasema ingawa tume imebainisha kuwepo kasoro na makosa katika uhamishaji wananchi, haijatoa jawabu la utatuzi wa makosa hayo wala kuwajibisha walioyasababisha.
Tume hizo ni ile ya Dk Gerald Ndika, ilichunguza matumizi ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha na nyingine iliongozwa na Mussa Iyombe, ikichunguza utekelezaji wa shughuli ya uhamaji wa wakazi kutoka katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Ripoti ya tume ya Iyombe, ilibainisha mambo matano yaliyosababisha kukwama kwa mpango wa uhamaji wa hiari, ikiwemo wananchi kutoshirikishwa vya kutosha, upungufu wa sheria na kanuni zinazoongoza mpango huo, ujenzi wa nyumba moja kwa familia zenye mke zaidi ya mmoja, kupungua kwa motisha ya waliohama na mpango kuendeshwa kwa ushawishi zaidi ya utashi.
Kwa upande wa tume ya Dk Ndika, ilipendekeza kufanywa marekebisho ya sheria ili kuondoa utaratibu wa matumizi mseto ya ardhi ndani ya hifadhi hiyo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga amesema angalau taarifa ya tume imeelezwa hadharani na watu wamejua mambo yanayoendelea, hivyo ni jambo la kupongeza.
Jambo lingine analosema linaonekana chanya katika taarifa hiyo ni pendekezo la kuundwa kwa chombo maalumu cha kushughulikia masuala ya wananchi wa Ngorongoro.
Amesema kuundwa kwa chombo hicho, kutawezesha suluhisho la mgogoro huo kuwa endelevu, kwa kuwa haukuanza sasa, hivyo isingewezekana umalizwe kwa siku moja.
“Mgogoro ulianza zamani, kwa hiyo kuundwa kwa chombo ni jambo zuri, ingawa itakuwa gharama, angalau kutasaidia kubaini migogoro na kuitafutia ufumbuzi kila inapotokea,” amesema.
Hata hivyo, amependekeza chombo hicho kitakachoundwa kipewe muda maalumu wa kumaliza kazi, kisiwe endelevu kama wizara.
Kwa upande mwingine, Dk Henga amesema pendekezo la maboresho ya baadhi ya sheria ni jambo jema, kwa kuwa zilizopo zilitungwa kwa ajili ya Wamasai, ilhali kwa sasa maeneo hayo zinaishi na jamii nyingine.
“Sheria ikirekebishwa tuhakikishe inaangalia na makabila mengine ili yatendewe haki, tusijikute tunamaliza mgogoro wa Wamasai kesho unaibuka wa kabila lingine linaloishi kule,” amesema.
Hata hivyo, msomi huyo wa sheria, amegusia pendekezo la tume hiyo linalotaka wanaohamishwa wasijengewe nyumba badala yake wapewe fidia, akisema linahitaji kutekelezwa kwa umakini.
Katika ufafanuzi wake, amesema kwa tamaduni za Wamasai baba ana sauti zaidi ya mama, akipewa fidia anaweza kuitumia kuoa mke mwingine na asizitumie kujenga makazi, hatimaye mwanamke akaathirika.
Pia, Dk Henga amesema kwa hali ilivyo sasa, inaonyesha ardhi ya Msomera haikidhi mahitaji ya wananchi wote, hivyo muhimu iangaliwe namna ya ama kuiongeza au kutafutwa mahali kwingine ili itosheleze.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi amesema hatua ya kufikiria kwamba unaweza kumhamisha mtu kutoka eneo lake la asili ni kosa.
Kwa maana hiyo, Mwabukusi amesema kitendo kilichofanywa na Serikali kuwahamisha wananchi katika ardhi yao ya Ngorongoro ni makosa na kinavunja haki zao.
“Ripoti imejikita katika kukiri makosa ya mchakato wa uhamishaji, ilhali msingi wa kosa unaanzia kwenye kuamua kumhamisha mtu kutoka katika makazi yake,” amesema.
Hata hivyo, mtaalamu huyo wa sheria, amesema atakuwa na mengi zaidi ya kueleza, baada ya kuisoma taarifa hiyo, akisisitiza maelezo ya majukwaani mara nyingi ni usuli wa ripoti kamili.
Wakazi wanalinda ikolojia
Mbali na wanasheria hayo, mwanasiasa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Amani Golugwa amesema chama hicho kilisimamia kilichomo kwenye michoro na mipaka ya awali, ambayo iliwapa haki wananchi wenyeji kuishi katika maeneo ya miji ya Ngorongoro.
Amesema aina ya maisha ya wananchi hao ambao ni jamii ya Wamasai, ndiyo inayolinda ikolojia ya eneo husika na kilichoharibu ni maendeleo ya wawekezaji yaliyopelekwa na Serikali.
“Tulichokuwa tunakipigania ni kuwepo kwa maeneo ya miji ambayo ilikuwepo tangu miaka ya 1950 na wananchi waliishi bila shida,” amesema.
Amesema msimamo wa chama hicho ni miji iliyokuwa makazi ya wenyeji iendelee kuwepo na aina ya maisha ya wWamasai haikuwahi kuathiri mzunguko wa ikolojia ya eneo la Ngorongoro.
Amesema watu hawakuhamishwa kwa hiari bali walishurutishwa.
Amesema ile miji isiyokuwepo katika njia za wanyama inapaswa kuendelea kuwepo na wenyewe ni sehemu ya mzunguko wa ikolojia.
“GN zilizofuta vijiji na vitongoji na zilirudishwa kadhaa na baadhi hazikurudishwa, zirudishwe. Serikali iondoe uwekezaji wa hoteli katika maeneo ya njia za wanyama, huko ndiko kuharibu ikolojia,” amesema.
Mmoja wa wananchi wa Ngorongoro aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema ni vema tume imetambua wananchi wa Ngorongoro wanaendelea na manung’uniko na wana hofu ya kupoteza utambulisho wao, lakini haijatoa jawabu la utatuzi wa hayo.
Mwananchi huyo, amesema tume pia imefanya vema kwa kuhoji wananchi wengi na imepata majibu mazuri kutoka kwao na imetambua kuwepo tatizo, lakini haitoi majibu yanayolenga kuleta utatuzi, bali imeegemea kwa wahifadhi.
Amekwenda mbali zaidi na kutaka ripoti ya tume hiyo iwekwe wazi kwa majadiliano, itolewe kwa kiswahili na wananchi wa Ngorongoro wapewe na isiwe ya mwisho, bali kuwe na fursa ya majadiliano kwa hatua zaidi.
“Tume imewasilisha na baadhi ya maoni ni mazuri lakini sehemu kubwa haionyeshi kama inalenga kutatua matatizo ya wananchi wa Ngorongoro.
“Kwa sehemu kubwa mrengo wa tume umejikita kutetea uhifadhi na sio wananchi na kwamba uhamaji utaendelea bila kuonyesha namna gani wananchi watashirikishwa ipasavyo,” amesema.
Amesema bahati nzuri Wamasai wa Ngorongoro hawali wanyama, ndio maana wanalala karibu na mazizi ya ng’ombe kwa kuwa ni maeneo salama.
Hadi hifadhi hiyo inaonekana ilivyo sasa, amesema ni kwa sababu wananchi wa Ngorongoro na Loliondo wameilinda, haiwezekani sasa ndiyo waonekane hawafai na wanapaswa kuhamishwa.
“Iweje sasa wananchi wamehifadhi ikolojia hadi wanyama wanasifiwa kuwa wengi, lakini sasa wanaondolewa kwa madai kuwa wanaharibu,” amesema.
Amesema kwa sasa eneo lote limechukuliwa na wafugaji hawana maeneo ya malisho, ndiyo maana wanalazimika kuingiza mifugo kwenye maeneo hatari.
Amesema wanatambua kuwa hifadhi ni muhimu, lakini wao waachwe waendelee kuitunza.
“Kuna haja ya kuendelea kushirikisha wananchi, bila kuwa na wazo la kuhamisha watu. Watu wanaweza wakahama kama kuna eneo zuri linalofaa kwa ufugaji na sio mbali na walikokuwa wanaishi,” amesema.
Kwa sababu, amesema Ngorongoro kuna maeneo ya makaburi na mambo mengine ya asili, hayo yatawalazimu wananchi warudi.
