Wadau wa elimu wataja njia kuinua ufaulu wa hisabati

Dar es Salaam. Wakati leo Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hisabati, wadau wa elimu nchini wameeleza wasiwasi kuhusu kiwango cha ufaulu wa somo hilo wakisema bado hakiridhishi licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali na wadau wa elimu.

Wadau hao wanasema ili kuboresha ufaulu wa somo hilo ni muhimu kuimarisha mbinu za ufundishaji darasani pamoja na kuwajengea walimu uwezo wa kufundisha hisabati kwa njia rahisi na inayovutia wanafunzi.

Kwa mujibu wa wadau hao, katika zama za sayansi na teknolojia mwanafunzi hapaswi kutishwa na somo la hisabati bali anatakiwa kujengewa mazingira yatakayomfanya alipende na kulielewa kuanzia ngazi ya elimu ya msingi.

Ikumbukwe kila mwaka Machi 14 mataifa mbalimbali duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hisabati kwa lengo la kuhamasisha matumizi na umuhimu wa somo hilo katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na uchumi.

Siku hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 2019 na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kwa lengo la kuhamasisha matumizi na umuhimu wa hisabati katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na maisha ya kila siku.

Maadhimisho ya siku hiyo pia hulenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu nafasi ya hisabati katika kutatua changamoto mbalimbali duniani ikiwemo majanga ya asili, milipuko ya magonjwa na maendeleo ya teknolojia.

Mwaka huu maadhimisho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Hisabati na Matumaini,” huku hapa nchini yakitarajiwa kufanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce).

Kwa upande wa Serikali ya Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan akifungua Bunge la 13, Novemba 14, 2025 jijini Dodoma alisema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake Serikali itaanza utekelezaji kamili wa maboresho ya sera ya elimu yanayolenga kuimarisha elimu ya ujuzi.

Alisema Serikali itaendelea kuweka mkazo zaidi kwenye masomo ya sayansi na hisabati (STEM) ili kuongeza idadi ya wataalamu katika maeneo ya sayansi ya data, akili unde, sayansi ya kompyuta na teknolojia za viwanda.

Takwimu zinaonyesha ufaulu wa somo la hisabati bado ni changamoto katika mitihani ya Taifa.

Kwa mujibu wa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2025, asilimia 73.55 ya watahiniwa walipata daraja F katika somo la hisabati huku waliopata daraja A hadi C wakiwa asilimia 15.86.

Mwaka 2024 hali ilikuwa karibu sawa ambapo takriban asilimia 25 pekee ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walifaulu huku zaidi ya asilimia 74 wakifanya vibaya.

Matokeo ya mwaka 2023 pia yalionyesha takriban robo ya watahiniwa tu ndio waliofaulu somo hilo huku wengi wakipata alama za chini.

Hali hiyo inaonyesha bado kuna haja ya juhudi zaidi kutoka kwa walimu, wazazi, Serikali na wadau wengine wa elimu ili kuboresha ufaulu wa somo hilo.

Akizungumzia namna ya kuboresha ufaulu wa somo hilo, mdau wa elimu Alistidia Kamugisha anasema ufaulu wa somo la hisabati nchini ni tatizo.

Anasema ni muhimu jamii kubadili mtazamo kuhusu hisabati kwani bado kuna dhana potofu kuwa ni somo gumu kwa wanafunzi.

“Tujenge misingi ya wanafunzi kulipenda somo hili kuanzia shule za msingi na tuepuke lugha za kutisha darasani.

Wapo walimu wanaowakatisha tamaa wanafunzi, hasa wasichana, kwa kusema kuwa wapo nyuma, badala yake wanapaswa kuwahamasisha na kuwajengea kujiamini,” anasema.

Anasema hisabati ni somo muhimu kwa maendeleo ya taifa kwani ndilo msingi wa teknolojia na ubunifu unaohitajika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Sylvester Rugeiyamu anasema mafanikio ya mwanafunzi katika hisabati huanza na maandalizi mazuri kuanzia ngazi za awali za elimu.

“Ufaulu wa somo hili bado ni tatizo, mwanafunzi anatakiwa afundishwe kwa njia inayomfanya afurahie kujifunza kuanzia shule ya msingi. Usipomjengea msingi mzuri katika hatua za mwanzo, inakuwa vigumu kwake kupenda somo hilo anapofika sekondari,” anasema.

Anasema pia mbinu za ufundishaji zinazotumiwa na baadhi ya walimu huchangia wanafunzi kulikimbia somo hilo, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuwajengea walimu uwezo kupitia mafunzo ya kisasa ya ufundishaji.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (Chahita), Dk Said Sima, anasema licha ya changamoto zilizopo kuna dalili za kuimarika kwa ufaulu wa somo hilo kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali.

Anasema moja ya hatua hizo ni utoaji wa mafunzo kwa walimu kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), ambao umesaidia kuongeza uwezo wa walimu kufundisha masomo ya sayansi na hisabati.

“Juhudi hizo pia zimeiwezesha Tanzania kushiriki katika mashindano ya hisabati barani Afrika na kwa nyakati tofauti tumefanikiwa kupata tuzo,” anasema.

Aidha, anasema Serikali imeanzisha mpango wa Samia Scholarship unaowawezesha wanafunzi wanaofaulu vizuri masomo ya sayansi kuendelea na masomo ya juu katika fani mbalimbali za sayansi na teknolojia.

Kwa mujibu wa Dk Sima, kuongeza idadi ya wataalamu wa hisabati kutasaidia Tanzania kutokuwa mtumiaji wa teknolojia pekee bali pia kuwa mtengenezaji wa teknolojia.