Sauti zilizotikisa Taifa na vipindi vilivyokonga nyoyo RTD

Awali ya yote, “Mzee wa Atikali” napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Raheem kwa kuniruzuku uhai Jumamosi kuntu ya leo. Kuamkia alfajiri ya leo, mvua kubwa imelinyea jiji la Bandari Salama  ikiambatana na mirindimo mikali ya radi ambapo mara ya mwisho mirindimo mikali namna hii kusikika, Morogoro Road na Ali Hassan Mwinyi Road zilikuwa ni barabara za njia moja, Kituo cha Mabasi ya Mikoani kilikuwa Mnazi Mmoja, Sinza ilikuwa ni mashamba ya mpunga, Kimara na Mbezi zilikuwa na basi moja tu la “UDA”, Mbweni kulikuwa na wanyama wa porini mfano chui wakivinjari, eneo la Best Bite, Namanga lilikuwa na Mizambarau, eneo la Mabibo lilisheheni Mikorosho huku Oysterbay ikiwa na miti mingi ya matunda mfano Mikungu, Mibuyu, Miembe, Mipera nk. Bongolanderz waliokuwepo jijini enzi hizo hawakusubiri daktari aandike ndipo wale matunda. La hasha. Walikuwa wakijiokotea tu!

Leo nimewiwa kuwakumbusheni wahenga na kuwajuza Gen Z mlioko hapa nchini kuanzia Mtambaswala- Ntwara hadi Mutukula- British Kingdom (BK) na diaspora mlioko nchi zote kuanzia Mzansi hadi  Kiribati kuhusu vipindi mujarab vilivyokuwa vikirindima Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) miaka ya 1960, 1970 & 1980 na majina ya watangazaji mahiri waliokuwa wakikonga nyoyo vilivyo enzi hizo.

Vipindi hivyo vya RTD vilikuwa sehemu ya utamaduni na maisha ya familia za Kitanzania. Ndio maana Mzee Manoni  Manoni wa Namtumbo, Ruvuma aliwapa wanae watatu majina ya vipindi (Majira, Harakati & Mchana Mwema). Tasnia ya Habari ilikuwa ikiheshimika sana na waandishi wa habari waliheshimika mno. Weledi, maadili mema na uzalendo vilikuwa vikipewa kipaumbele sana. Kuajiriwa RTD ilikuwa kipengele, kwani watangazaji hawakuwa wakiajiriwa kimagumashi.  Hakukuwa na uduwanzi wa kupachika mtu kwa vile tu ni mtoto wa dada au baada ya kupata ki-note toka kwa kingunge fulani.

Usaili thabiti ulikuwa ukifanyika kupata watangazaji bora. Usaili aliofanyiwa Mzanzibara, David Wakati, unathibitisha umakini uliokuwepo. David Wakati alitakiwa kuigiza akimhoji Sultan wa Zanzibar wa wakati ule. Ilikuwa ni shughuli pevu lakini aliifanya kwa ufanisi wa hali ya juu na akaajiriwa na akaja kuwa mtangazaji mahiri hadi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa RTD.

Aidha, mtangazaji mpya alikuwa haingii studio kabla ya kupewa mafunzo ya namna ya kuandaa na kutangaza vipindi mfano, Ahmed Jongo alipoajiriwa RTD mwaka 1967, alianza kwa kupewa basic training pale Jengo la Utangazaji kisha akapelekwa Australian Broadcasting Commission, Sydney, Australia kwa miezi sita.

Siku hizi, kutokana na utitiri wa redio na runinga uliopo nchini, mtu aweza kuajiriwa leo toka mtaani akiwa hana hata a, b, c za uandishi, na leo hii hii anaruka hewani kama mtangazaji!

RTD, iliyoanzishwa Julai 1, 1965 badala ya “Tanganyika Broadcasting Corporation” (TBC), ndiyo redio ilikuwa ikisikilizwa na wengi licha ya kuwepo zingine kama vile “Sauti ya Tanzania Zanzibar”, “BBC Swahili” na “Sauti ya Umoja wa Mataifa”. RTD ilikuwa na Idhaa ya Kiswahili na Kiingereza. Ili kuisikiliza, ilikubidi kumiliki redio kama vile 277, Phillips na National Panasonic (Dudu Proof).

Mara nyingi, baba ndiye aliyekuwa akiwasha redio. Redio hizi na betri zake zilikuwa zikiuzwa kwenye maduka ya Regional Trading Company (RTC) yaliyokuwa yametamalaki mikoa yote nchini. Betri maarufu enzi hizo zilikuwa za aina ya “National”. Kwa vile jamii nyingi zilikuwa mpechempeche, nguvu za betri zilipoisha, betri zilianikwa juani. Nguvu zilipoisha tena, betri ziligongwagongwa chini na kurudishwa tena ndani ya redio kupiga kazi!

1.1 Vipindi & Watangazaji:

Taarifa ya Habari ndio ilikuwa ya muhimu zaidi kwani ilisikilizwa na Bongolanderz wengi nchini, akiwemo Rais Julius Nyerere, mawaziri na viongozi wote nchini. Kutokana na umuhimu wake, si kila Tom, Dick & Harry alikuwa akiruhusiwa kusoma Taarifa ya Habari. La hasha. Ili mtangazaji aruhusiwe kusoma Taarifa ya Habari, ilikuwa ni lazima athibitishwe kuwa na uwezo thabiti.

Kabla ya kusomwa Taarifa ya habari, ulisikika mdundo wa kipekee uliopigwa kwa umahiri na msanii maarufu aliyekuwa haoni lakini aliyeruzukiwa kipaji mujarab, Mzee Morris Nyunyusa, akitumia ngoma 10. Picha ya Mzee Nyunyusa, aliyekuwa akiishi Mtoni kwa Azziz Ali, iliwahi kuwekwa kwenye stempu ya Shirika la Posta kuenzi uwezo wale.

Kwenye kusoma Taarifa ya Habari, utamkaji wa majina magumu ya watu mfano Rais Valery Giscard d’Estaing wa Ufaransa; miji mfano Edinburgh au nchi mfano Mozambique, ulipelekea mtangazaji ajiongeze kwa kwenda kwenye balozi husika ili kufundishwa namna ya kuyatamka.

Mjomba SS Nkamba alikuwa anasumbuliwa sana na jina la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) wa wakati huo, marehemu Dag Hammarskjold. Ili asilikosee, alikuwa analitamka tangu akitoka ghorofani, chumba cha habari mpaka studio! Enzi hizo, mtangazaji akimbwela alikuwa akiwekwa kitimoto na Mkurugenzi Mkuu wa RTD au wakurugenzi wengine au mara nyingine wote hao walimgombea kama mpira wa kona!  Siku hizi, unaweza kumsikia mtangazaji anatwanga chafya asomapo Taarifa ya Habari au anatumia “R” badala ya “L” lakini viongozi wake hawajali, unastaajabu kesho mtangazaji huyo yupo studio anaendelea kuisoma na kufanya makosa yaleyale!

Baadhi ya watangazaji waliowahi kusoma Taarifa ya Habari, Idhaa ya Kiswahili na Kiingereza, kwa miaka tofauti ni Ellie Mboto, Salim Seif Nkamba “Mjomba SS Nkamba” (akiishi Majimaji Street), Ben Mkapa, Mustafa Nyang’anyi, Stephen Mlatie, Suleiman Hegga, Ahmed Kipozi, Salim Mbonde, Mikidadi Mahmoud & Richus Matipa.

Muda wa kusoma Taarifa ya Habari ulikuwa ni asubuhi saa 1, 4, 7, 10 na saa 2 usiku. Ben Mkapa alipokuwa akifanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje mwanzoni mwa miaka ya 1960 alikuwa akienda kusoma Taarifa za Habari Idhaa ya Kiingereza kutokana na umahiri wake kwani shahada yake ilikuwa BA (English- Hons). Mkapa aliwahi kusimulia: “I read news in English because of my fluency in English”. Balozi Ferdinand Ruhinda alisimulia zaidi: “Ben Mkapa would come to read English language bulletins as a part-timer. I was one of those preparing those bulletins. He liked my job and we became friends”.

Zamani kutokana na mfumo dume uliokuwa umetamalaki nchini, wanawake hawakuruhusiwa kusoma Taarifa ya Habari. Wao walipewa vipindi rahisi-rahisi kama vya muziki au mambo ya wanawake. Bi Edda William Ngurukuru, ambaye aliajiriwa mwaka 1965 na ambaye alikuja kujulikana kama Bi Edda Sanga baada ya kuolewa na Bw. Lazarus Abel Sanga mwaka 1974, siku alipokuja kuwa mwanamke wa kwanza nchini kusoma Taarifa ya Habari, baadhi ya Bongolanderz walipigwa butwaa na kuzomoka: “Wamefanya Taarifa ya Habari kama kipindi cha Mambo ya Wanawake, iweje Mwanamke akasoma Taarifa ya Habari, kitu serious hivyo?” Songombingo hii ilimkumba pia Profesa Esther Mwaikambo alipokuwa mwanamke wa kwanza nchini kuwa daktari mwaka 1969. Wagonjwa walipokuwa wakienda hospitali na kumkuta yeye, walimuuliza “Daktari yuko wapi?” Na alipowajibu kuwa ni yeye, wengi walikuwa wanasepa kwani hawakuamini kama mwanamke angeweza kuwatibu!

Umahiri ambao Bi Edda Sanga alikuwa akiuonesha kwenye kusoma Taarifa ya Habari hatimaye ukawaziba midomo wanaume wote waliokuwa na wasiwasi.

Vipindi vya RTD vilikuwa vikianza saa 11.00 alfajiri. Kilikuwa kinaanza kipindi cha dini ya Kiislamu kikifuatiwa na cha dini ya Kikristo kilichoitwa “Inueni Mioyo”.

Sarah Dumba alikuwa ndiye mara nyingi akitangaza Alfajiri. Alikuwa anaishi Kigamboni na alikuwa akiwahi sana kazini. Alikuwa mwanamama makini na mchapakazi hodari aliyeipenda sana kazi yake.

Wahenga waliponena “Ujana Maji ya Moto” na “Kazi na Dawa”, hawakukosea. Ujanani Sarah Dumba alipenda sana muziki. Akimaliza vipindi vyake alikuwa anabuzibuzi kisha anazama DDC Kariakoo kwenye Msondo Ngoma hadi alfajiri! Akitoka hapo alikuwa akienda Kamata kuvizia gari la RTD na akifika kazini anafungua kipindi bila mtu kugundua kuwa alitoka kujirusha Msondo usiku kucha. Aliipenda mno Msondo kiasi kuna wakati alikuwa akitinga DDC Kariakoo huku akiwa na mimba kubwa ya mwanae, Rashid!

“Kumekucha” ni kipindi kilichokuwa kikianza saa 11.30 hadi saa 12.00 asubuhi. Kipindi hiki kilikuwa kikichukiwa sana na madenti kwani walitakiwa kuamka kwenda shule kuwahi namba. Wimbo wa kipindi hiki ulinyofolewa toka bendi ya Safari Trippers, mwimbaji akiwa jabali la muziki, Marijani Rajab: “Kumekuchaaa sasa kumekuchaaa, majogoo vijijini yanawikaa…….”

1.1.4 Mazungumzo Baada ya Habari:

“Mazungumzo Baada ya Habari” ni kipindi kilichoanzishwa mwaka 1973 na Paul Sozigwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utangazaji (1972-1979). Sozigwa, aliyewahi kuwa Mwandishi wa Rais Nyerere, ndiye aliyekuwa akiandika na kisha watangazaji maalumu walichaguliwa kutangaza. Akili kubwa sana ilitumika kukitayarisha.  Mtangazaji wa kwanza kutangaza kipindi cha “Mazungumzo Baada ya Habari” alikuwa ni Abdul Baker kisha akaja Abdul Ngarawa na baadaye Juma Ngondae. Lengo lilikuwa ni kueneza propaganda za TANU & CCM na maamuzi mbalimbali ya Chama na Serikali.

1.1.5 Kipindi cha Michezo:

Miaka ya 1960, watangazaji mahiri wa kipindi cha michezo  walikuwa ni Kwegyir Munthali na Ally Saleh. Hawa walidanja kwa ajali mwaka 1964. Gari la Kwegyir, aliyepewa jina hilo la gwiji Mghana, James Emman Kwegyir Aggrey, lililigonga treni pale relini makutano ya Shaurimoyo/Pugu rd (Treni huwaga haigongi gari/mtu. Ni kinyume chake- Kifungu cha 84 cha the Railways Act Cap 168 RE 2023). Ally Saleh alidanja hapohapo pamoja na mtu mwingine lakini Kwegyir alifia Muhimbili Juni 20, 1964, ikiwa ni siku chache baada ya ajali. Msiba huu ulitikisa nchi nzima.

Kipindi cha michezo kilikuwa maarufu sana na kilianza na kumalizika kwa wimbo wa Mmarekani, Alois Maxwell, ulioitwa Cotton Candy uliopigwa mwaka 1964. Bongolanderz walijitungia maneno yao “Baba yake Juma amevaa viraka, Vinaulizana umekuja lini? Nimekuja jana, nimekuja juzi, nimekuja leo tataaaaa tataaaa taraaaaa”. Muda wa kipindi hiki ulikuwa ni kuanzia saa mbili kasorobo usiku hadi saa mbili kamili usiku.

Watangazaji wengine waliokuja kukitangaza ni Dustan Tido Mhando, Abdul Masudi, Mikidadi Mahmoud & Abdallah Majura.

1.1.6 Matangazo ya mpira:

Matangazo ya mpira yalikuwa kuanzia saa 10:30 jioni hadi saa 12: 00 jioni kasoro mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki iliyopigwa Uwanja wa Amani Januari 13, 1975 saa 2 usiku ambapo Yanga iliishenyenta Simba 2-0 (Sunday Manara & Gipson Sembuli). Ahmed Kipozi ndiye aliyetangaza mbungi hii:

“Usiku wa leo, mtangazaji wako ni mimi Ahmed Kipozi nikiwa uwanja wa Amani, Zanzibar. Muda huu ni saa 2 kamili usiku ikiwa bado dakika 5 tu pambano hili la watani wa jadi lianze”.

Watangazaji maarufu wa mpira walikuwa Mshindo Mkeyenge, Tido Mhando, Ahmed Jongo, Ahmed Kipozi, Mikidadi Mahmoud, Salim Mbonde, Charles Hilary, Suleiman Kumchaya, Abdallah Majura, Chilambo Dominic, Abdul Omar Masudi Jawewa & Yusuph Omar Chunda aliyekuwa akitangaza mpira Zenji.

Abdul Omar Masudi Jawewa, aliyewahi kuwa pia Katibu mwenezi wa Yanga, alikuja kuacha RTD akaajiriwa na Mdosi, Mohamed Virani, kwenye kiwanda cha Bobby Soap. Mkewe alikuwa Benki Kuu akaliwa kichwa 1993 kwa retrenchment. Dada yake, Bi Rehema Masudi, anafanya kazi Benki Kuu, Tawi la Mwanza. Mabandido walimdanjisha Masudi nyumbani kwake Temeke wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan Juni 1986. Mabandido hao walimkuta Masudi akifuturu na wakamuamuru afanye dua yake ya mwisho kabla ya kwenda ahera. Aliwasihi sana wasimuue akiwaeleza yuko tayari kuwapa chochote ili wasimtoe roho, lakini wakamwambia uovu alioufanya adhabu yake ni moja tu kisha wakammiminia shaba kama zote mbele ya familia yake na kutawanyika bila kuchukua kitu chochote. Masudi hakuomba hata maji!

Suleiman Omar Kumchaya, aliyekuja kuwa DC mkoani Tabora, alikuwa mtangazaji hodari wa mpira na ndiye aliyempa beki mahiri wa Yanga, Ahmed Amasha, nickname ya “Mathematician” baada ya kumlamba chenga murua Ramadhan Lenny “Abega wa Simba. Amasha ndiye “MVP 1985”.

Watangazaji hawa mara nyingine walikuwa wakijisahau na kuonesha mapenzi yao mfano, Mshindo Mkeyenge siku moja alighafirika na kutangaza “Simba moja, sisi  mbili”. Hiyo “sisi” alimaanisha Yanga. Licha ya kuwa mtangazaji, Mkeyenge alikuwa pia Katibu mwenezi wa Yanga 1967-1976.

Tido Mhando ndiye aliyechaguliwa na Mkurugenzi wa RTD 1977, Paul Sozigwa (Yanga kindakindaki) na msaidizi wake, Sammy Mdee (Yanga lialia) kutangaza mbungi ya Simba dhidi ya Yanga Julai 19, 1977. Simba iliandika historia baada ya kuikung’uta Yanga 6-0. Tido aliitendea haki siku hiyo ambayo Abdallah Kibaden “King” aliweka historia ya kufunga Hat Trick.

Ahmed Jongo alikuwa na uwezo mkubwa wa kutangaza mbungi kiasi kwamba waliokuwa nyumbani ni kama nao walikuwa uwanjani! Alitunga vimbwanga vingi vya mbungi mfano “Maguu kumi na mbili”, “Mtambaa panya” nk.

Miaka ya 1980s, Charles Hilary naye alishika usukani na alikuwa na sauti nzuri sana na aliwatungia nicknames wachezaji wengi.

Charles Hilary alikuwa na uwezo sana na aliwahi kutangaza mechi ya Sigara dhidi ya Nyota Nyekundu bila kuwa na karatasi. Kama kuna mechi aliitendea haki ni ya Biashara Shinyanga dhidi ya Simba “Shamba la Bibi”. Edibily Lunyamila alikuwa kidato cha 4 na wa moto sana akiichezea Biashara Shinyanga. Kwenye mechi hiyo alikuwa akimpita Aboubakar Kombo, mbavu ya kulia ya Simba, kama atakavyo na ndani ya dakika 15 tu alikuwa ametoa assists mbili. Charles Hilary ndiye aliyemtambulisha Lunyamila kwa manazi wa soka nchini. Aidha, kolabo ya Charles Hilary na Dominic Chilambo wa Mwanza ilifurahisha sana ambapo walitangaza mbungi kwa kupokezana. Hapa chini ni jinsi Charles Hilary alivyokuwa akipiga “kolabo” na Dominic Chilambo :

“Chilambo….Chilambo….. unanisikia? Hapa Uwanja wa Taifa kumekuchaaaa……. Zamoyoni Mogela “Golden boy” anaipatia Simba bao la kuongoza. Mogella alipiga tiktaka, kipa Morris Nyuchi wa Nyota Nyekundu wala hakujitingisha, alisimama kama sanamu la Askari Monument. Simba 1, Nyota Nyekundu 0, kwako Chilambo…….”

“Charles, Charles wakati unarudisha matangazo, Mao Mkami “Ball dancer”aliuchukua mpira akampiga chenga beki David Rogers aliyelala Yombo akamkosa, kisha akampasia Beya Simba aliyempelekea Juma Amir “Pele wa Mwanza” aliyegonga kisigino kwa Kitwana Selemani aliyempa pasi saafi Fumo Felician, ambaye aliachia fataki kali la mita 40 lililoenda kugonga nguzo pembeni anakotagia njiwa na kujaa kambani, likimuacha kipa Bahatisha Ndulute wa Ushirika Moshi akigaagaa. Hili ni goli la karne! Tous Puissant Lindanda “Wana Kawekamo” Pamba 1 Ushirika 0″.

Zamani hakukuwa na “vibanda umiza”, mashabiki waliizunguka redio na kusikiliza mbungi pamoja kitaa.

Dunia Wiki Hii ni kipindi kilichokuwa kikidadavua mambo yaliyotokea kwa wiki nzima duniani kote. Watangazaji Sekione Kitojo, Mohammed Dahman, Dustan Tido Mhando & Nassor Nsekeli, aliyekuwa na “sauti ya mafua” ndio waliokiendesha.

Mchezo wa Redio ni kipindi maarufu kilichokuwepo kila Ijumaa saa 2: 0 usiku. Kilikuwa kipindi kitamu sana kilichowapa umaarufu mkubwa Mzee Jongo, Babu Kipara, Mariam Yusuph nk. Mchezo pendwa wa redio “Penzi Kitovu cha Uzembe” kilikipaisha sana kipindi hiki kwani uliburudisha na kufundisha.

Aidha, mkasa wa “Mkwawa & Wajerumani”  ulibamba sana.

Wakati wa Kazi ni kipindi kilichokuwa kikienda hewani kila siku ya kazi kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 6 mchana na kiliendeshwa na Bathlomeo Kombwa (Bati Kombwa). Walihojiwa wafanyakazi tofauti kisha walipewa fursa ya kuchagua wimbo. Wimbo “Nidhamu ya Kazi” wa Juwata haukukosa kupigwa.

Mchana Mwema ni kipindi kilichokuwa kikirindima kila ilipofika saa 6 kamili hadi saa 7 mchana. Al Marhum Bi Salama Mfamao ndiye aliyekuwa kwenye usukani wa kipindi hiki.

Mkazi huyu wa Mtaa wa Usoke, Migomigo, aliwahi kusepa RTD akaenda kusomea ualimu na kuanza kufundisha Shule ya Msingi Mnazi Mmoja lakini alipoona miyeyusho, akarudia kazi yake ya utangazaji.

“Wakati umewajia wa salamu kwa wagonjwa hospitalini tunawapa pole. Ajuaye Bwana Mungu kwa mzima kuwa mfu mgonjwa kuwa salama, leo tunawapa pole”. Huu ni ubeti wa wimbo wa Omar Kungubaya kuashiria kuanza kwa kipindi cha wagonjwa.

Kipindi hiki kilikuwa cha Jumapili asubuhi kikiletwa na Chisunga Stephen ambapo wagonjwa waliolazwa walitembelewa na kuhojiwa mahospitalini kujua hali zao kisha kupewa fursa ya kuchagua wimbo. Cha ajabu, wimbo “Siku ya kufa” wa “Orchestra Makassy” ulioimbwa na Dk Remy Ongara,  ndio ulikuwa ukichaguliwa na wengi!

Watu wengine walibaini ndugu zao kuwa ni wagonjwa kupitia kipindi hiki.

Kipindi cha Majira kilikuwa kikitangazwa saa 3 usiku ambapo “Bongolanderz” wengi walipenda kumsikiliza Ben Hamis Kikoromo @ Ben Kiko wa Dodoma kwani alikuwa na utangazaji wa kipekee wa mikogo, hasa alivyowasifia “CDA watoto wa nyumbani”. Ben Kiko aliipenda sana kaziye akimalizia kwa kusema “Huyu ni Ben Kiko, Majira, Dodoma”. Alitangaza “Vita vya Kagera” mubashara akiwa na vikosi vya JWTZ. Baadaye alisaidia sana kuitambulisha Tabora.

1.1.12 Taarifa ya Habari Maalum:

Taarifa ya Habari Maalum ilitangazwa na Mkurugenzi mwenyewe wa RTD, David Wakati. Ilikuwa ukiskia sauti yake kwenye Taarifa ya Habari ujue kuna jambo muhimu la kitaifa, kama ilivyotokea Novemba 11, 1979:

“Hii ni Taarifa ya habari kutoka Radio Tanzania Dar es Salaam. Kwanza ni habari kwa ufupi: Rais Nyerere leo amekubali ombi la Waziri wa Fedha, Edwin Mtei, kujiuzulu”.

Nipe Habari ni kipindi kilichokuwa kikitangazwa na David Wakati kila Jumapili Saa 8:30 mchana. Huyu Mwamba alikuwa akiongea kwa sauti nzito ya mamlaka.

1.1.14 Kipindi cha Mama na Mwana:

Umoja wa Mataifa (UN) iliutangaza mwaka 1979 kuwa ni mwaka wa mtoto. Mzee Suleiman Hega akaamua kianzishwe kipindi cha watoto.

Bi Sango Athumani aliyekuja kuitwa Sango Kipozi baada ya kuolewa na mtangazaji mwenzie Ahmed Kipozi na ambaye ndiye mama wa “Unique Sisters”, akapelekwa Masri kwa mafunzo. Baada ya kurejea, akaasisi kipindi cha “Mama na Mwana” baada ya kupata mafunzo Masri 1980. Alipohamishiwa Dodoma miezi 6 baadaye, ndipo Debora Mwenda aliposhika usukani.

Kipindi hiki kilinguruma kila saa 8:30 alasiri Jumamosi. Kipindi hiki kilikuwa kikipendwa hata na watu wazima:

Wimbo wa kufungua kipindi hiki ulikuwa mzuri sana:

“Karibuni watotoo wa Afrika”

“Karibuni kipindi cha watotooo”

“Msikie nyimbo, hadithi na vicheko, Mengineyo mambo muhimu ya masomoo”. Wazazi wengi walikorofishana sana na watoto wao walipowatuma kazi kipindi hiki kilipoanza.

Debora Mwenda alikitendea haki kipindi hiki na alifanya watoto wabanane ilipo redio kusikia mikasa: “Binti Chura”, “Ua Jekundu”, “Adili na Nduguze”, “Kisa cha Mfalme Juha nk!

Bi Mwamvita Makamba aliwahi kushiriki kipindi hiki babake, Yusuph Makamba, alipokuwa RC Mwisho wa Reli.

Debora Mwenda alipendwa sana hadi akawa anatumiwa zawadi kedekede Posta na wazazi na watoto mfano Khanga, pipi, sukari nk.

Kama ilivyokuwa kwa  Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ambaye baba yake alitokea Nothern Rhodesia (Zambia), wazazi wa Debora Mwenda wakiwa na watoto wao wadogo wanne, akiwemo Debora, walikuja Tanganyika wakitokea Southern Rhodesia (Zimbabwe) mwaka 1946 na kulowea hapa.

Baba yake Deborah alikuwa Meneja wa ukumbi wa Anatouglo. Alikuwa na tabia kama za wazungu na ukienda bila tai ujue huingii, aslan abadan!

“Mzee wa Atikali” alifanya mafundisho ya Kipaimara na mwanaye Debora akiitwa Michael Mwenda, Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay.

Mtangazaji Michael Katembo alipenda sana nyimbo za asili na ndiye aliyekuwa akikivurumisha kipindi hiki.

Katembo alikuwa na mikogo na mbwembwe sana. Kuna wakati nyimbo za ngoma zinaanza ghafla redioni basi utamsikia “Nyie Wahaya mna haraka sana, nyie nani kwani, rudini, rudini, nani kawaita?”

Mikingamo kilikuwa ni kipindi cha kipekee. Abisay Stephen ndiye alikuwa akikitangaza kipindi hiki. Aidha, awali, Salim Seif Nkamba naye alitia fora alipokuwa akichimba mkwara: “Tuambie; Nani, Yuko wapi na anafanya nini kuhujumu uchumi”.

Huenda hakijawahi kutokea kipindi chenye vituko na hekaheka toka nchi yetu ipate uhuru kama kipindi hiki kilichosimamiwa na Nadhir Mayoka. Kipindi hiki kilikuwa kikianza saa 12 jioni na Bongolanderz wengi walikaa nje pembeni ya redio zao wakiwa wamejitayarisha kukauka mbavu. Kuumwa mbu na hatimaye kuugua malaria ilikuwa kitu cha kawaida kisha unakunywa chloroquine 4-4-2 na kuwashwa mwili mzima kila uzitumiapo! Hata hivyo, watu hawakuacha kukaa nje kutokana na burudani ya kipindi hicho.

1.1.18 Club Raha leo Shoo:

Enoc Ngombale, mdogo wa Kingunge Ngombale Mwiru, ndiye aliyekiendesha kipindi hiki cha starehe. Baadaye, Julius Nyaisanga “Uncle J” akakitendea haki vilivyo kipindi hiki.

Kwenye kipindi hiki, mwanamuziki alipokuwa akitambulishwa ama ataimba au atapiga chombo kisha anashangiliwa sana na umati.

Michael Katembo ndiye aliyekiongoza kipindi hiki kilichopendwa zaidi na watu wa “Uswekeni”.  Baadaye kikaja kujulikana kama “Mbiu ya Mikoa”.

Ombi lako ni kipindi kilichokuwa kikirushwa hewani na Bi Christine Chokunogela. Hiki kilikuwa kipindi cha kutuma ombi la kuchagua wimbo na wadau walizoea kumsihi “Tafadhali usinitupe kapuni”.

1.1.21 Chei Chei Shangazi:

“Chei Chei Shangazi Shangazi, Tufurahi Shangazi Shangazi, Uje tena, Shangazi Shangazi “.  Sarah Dumba, Nellie Grace Kidela & Aloysia Maneno ndio waliokuwa wakiimbiwa na wanafunzi – watoto.

1.1.22 Mawaidha ya Kiislamu:

Kila Ijumaa Saa 8:00 mchana Sheikh Mkuu, Sheikh Hemedi Bin Jumaa Bin Hemedi, alikuwa akitoa mawaidha kuntu akikonga nyoyo hata za Wakristu. Huyu Sheikh Mkuu alipendwa mno.

1.1.23 Kijaruba: Hivi vilikuwa viunga vya Mzee-Mzima Abdallah Mlawa.

Kulikuwa na watangazaji ambao walikuwa wakituma taarifa kutokea mikoani:

2.1 Tumbo Tamimu Risasi- Songea

2.2 Nswima Ernest- Sumbawanga

2.3 Benjamin Rwegasira- BK

2.4  Richard Leo- Idodomia

2.6 Suleiman Muhogola- Ruvuma

2.8 Chisunga Stephen- Kigoma

2.9 Abisay Stephen- Ruvuma.

2.10 Nechi Lyimo- Kilimanjaro

Aidha, Bi Halima Kihemba, aliyeitwa Halima Meza kabla ya kuolewa na mtangazaji mwenzie, Abbas Kihemba, alikuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kumwakilisha Mkurugenzi wa RTD Kanda ya Mashariki 1990. Ofisi yake ilikuwa Idara ya Habari Maelezo akiwa na Fundi mitambo, Francis Kapungu na alipodanja akaenda Consalva Mwereke. Baadaye walipanga ofisi ya CCM Morogoro mjini. Mwaka 1992 vyama vingi vilipoanza wakahamia jengo la TRA Stesheni Rd. Alikaa hapo hadi 1999 Rais Mkapa alipomteua kuwa DC, Ulanga.

Mkurugenzi Mkuu wa kwanza Mzalendo wa RTD, Miki Mdoe, ambaye aliwahi kuwa mume wa Bibi Titi Mohammed, alikuwa akitangaza idhaa ya “External Service” ie Kiingereza. Alikuwa na sauti nzuri sana.

Kwa miaka tofauti, (Ben Mkapa (part-timer), Abdul Mtulya (kipindi chake “Face the Mic” kilikuwa maarufu sana akiwahoji wapigania uhuru), Edda Sanga & Richus Matipa walikuwa wakisoma kwa umahiri taarifa za Kimombo.

RTD ni Tunu ya Afrika kwani, kupitia “External Service”, ilitoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru barani Afrika.  Wapigania uhuru waliitumia kufikisha ujumbe na kuelezea mambo ya nchi zao mfano Robert Mugabe, Samora Machel, Sam Nujoma, Dk Eduardo Mondlane nk.

RTD ilikuwa na vikorombwezo vingi,  mfano;

4.1 “Mpango wa pili wa maendeleo unasema kuleni kuku mayai, mboga samaki, maziwaa”

4.2 “Ati dereva kanywa gongo, ati sawa hiyo? Hataaaaaa, hiyo si sawa dereva, acha vitukoo”

4.3 “Shambani x 4, mazao bora shambani, wananchi tukalime..”

Jacob Tesha alikuwa mtangazaji mahiri sana wa kipindi hiki kilichopendwa sana na washua, hususan wanafunzi wa UDSM. Bi Nellie Grace Kidela ambaye alijiunga RTD 1976 na ambaye aliwahi kufundisha Oysterbay Primary School, skuli aliyosoma “Mzee wa Atikali”, alijizolea sifa kemkem kwenye kipindi hiki kwani alikuwa mmoja wa watangazaji ambao walikuwa  wanatema yai vilivyo. Ung’eng’e ulikuwa ndio mahala pake.

Kwenye kipindi hiki, kulikuwa na ngoma za kishua sana na soul music ilibamba sana.

Ujumbe wa Leo kilikuwa kipindi kilichokuwa kikianza saa 2:15 usiku hadi Saa 2:30 usiku. Mara nyingi hotuba za zamani za Rais Nyerere ndizo zilizokuwa zikiwekwa. Ilikuwa ni burudani kubwa kumsikiliza Mchonga, Musa & Mzee Haambiliki akihutubia.

Watangazaji waliokuwa kwenye usukani kwenye vipindi vya salamu (Jambo asubuhi/Mchana mwema/Jioni njema/) ni Khalid Ponela, Salama Mfamao na Malima Ndelema aliyezijua lugha karibu zote za nchi hii. “Post cards” za kutuma Posta zilihusika sana.

Wafuatao ndio walikuwa Mabingwa:

7.1 Fundi Wajad Fundi (Mahuta Shimoni- Newala)

7.4 Sudi Saleh “Baba Dula One” Makokora Tanga)

7.5 Limonga Justin Limonga

7.7 Thobias Mnyani (Uhuru na Msimbazi)

7.8 Rashindi Nguruwe (Sokoni, Korogwe)

7.9 Chivalavala A. Chivalavala aliyependa kusema: “Nikiwa safarini kwenda “South”, salamu special kwa mke wangu kipenzi, Ziada Napinda”. “Mzee wa Atikali” alidhani ni Afrika Kusini kumbe Ntwara!

7.10 Chidi Chidi Chitenda

7.12 Zainab Wajad- Mahuta

7.13 Kondo Ali Kondo (Tabora)

7.15 Fundi Hamis, Full Migebuka wa Mwandiga Fashion Kigoma sokoni

7.17 Kuambiana S. Kuambiana

7.18 Irene Kawiche (tofauti na jina lake lionekanavyo, huyu alikuwa dume!)

7.19 Alphonce Majiyapwani: Huyu alikuwa maarufu sana kwenye kipindi cha “From Me to You” cha External Service ya RTD.

7.22. Chesko Mzee wa Matunda, Afrika Sana, Sinza

7.25. Lawena Sonda Baba Mzazi  Makongorosi, Chunya

7.26. Issa Hassan Majeshi, Ukonga

7.28. Haruna Damla- Damla, Ukame Na.10 Magomeni Mapipa.

7.29. Kipe wa Kipesile- Katumba, Tukuyu

7.31 Zacharia Ndemfoo: wa Babati. Huyu ndo alikuwa Gwiji wa Salamu. Alianza toka wakati wa Ukoloni na alikuwa akituma salam hadi nje ya nchi.

Hawa watuma salamu walikuwa wakituma salamu kisha humalizia kwa kuchombeza kwa vijimaneno:

“Salamu ni nusu ya kuonana” au “Kula na kulipa ndio mtindo wa kisasa” nk.

RTD ilikuwa haikeshi hivyo ilipokuwa inafika saa 6 kamili usiku, unaskia wimbo wa Taifa “Mungu Ibariki Tanzania” kisha mitambo inazimwa hadi keshoye alfajiri.

Baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari (redio na runinga), siku hizi wanaajiri wanahabari mpechempeche na ndilo maana Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete aliwahi kusema “waandishi wengi siku hizi ni makanjanja”. Baadhi ya Watangazaji wasiokuwa na taaluma ya habari wanadhalilisha sana lugha za Kiswahili na Kiingereza. Ni nadra sana kumkuta mtangazaji asiyetumia “Kiswa-Nglishi”

Zamani, watangazaji walikuwa wanajielewa. walikuwa na weledi, sio kama watangazaji wa mwendokasi tulionao leo wenye makosa lukuki ya lugha mfano “R” na “L”, Mdada/Mmama badala ya dada/mama, Lisaa badala ya saa na pia kusoma habari kwa kutofuata “nukta” & “koma” nk.

Siku hizi, “studio” nyingi zimegeuka vijiwe vya michapo, “ubuyu”, “kuchambana” na mambo ya ngono. Vipindi vya kuelimisha jamii ni vichache mno.

Aidha, kuna watangazaji wameokotwa mitaani na kuambiwa tu “kaa hapo mwanangu, upige kazi”, wakati hana hata a, b, c za utangazaji. Kwenye vipindi vingi vya michezo, wachambuzi wengi ni wacha- mbuzi.

“Mzee wa Atikali” anaamini Atikali hii itakuwa chachu ya kuleta mabadiliko kwenye Tasnia hii muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu.

Imeandikwa na Mzee wa Atikali