Ludewa. Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) imetoa Sh3.1 bilioni kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji sita vilivyopo ukanda wa Ziwa Nyasa, wilayani Ludewa mkoani Njombe.
Mradi huo ulianza kutekelezwa Julai 13, mwaka 2025 na unatarajiwa kukamilika Aprili 13, 2026, ukilenga kuwapatia huduma ya umeme wateja wa awali takribani 160.
Akizungumza katika ziara ya kutembelea mradi huo katika Kijiji cha Madunda, Kata ya Mawengi wilayani Ludewa, Msimamizi wa Miradi wa Rea Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Dastan Kalugira, amesema baada ya kukamilika, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) litaunganisha umeme kwa wateja hao kwa gharama ya Sh27,000.
Kalugira amesema mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni Suma JKT, ambaye amekamilisha kazi ya kusimamisha nguzo zote 105 zinazohitajika katika mradi huo.
Ameongeza kuwa hatua iliyobaki ni kuvuta waya ili kukamilisha miundombinu ya usambazaji wa umeme kabla ya wananchi kuanza kupata huduma hiyo.
“Mradi huu ni wa kipekee kutokana na mazingira ya milimani katika eneo hilo, hali iliyosababisha changamoto katika utekelezaji wake,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa ingawa mradi huo upo katika Mkoa wa Njombe, baadhi ya vitongoji vinne vilivyopo upande wa ufukwe wa Matema wilayani Kyela mkoani Mbeya vimeunganishwa na umeme kutoka upande huo kutokana na ugumu wa kuvifikia kupitia Njombe.
Vitongoji vitakavyonufaika na mradi huo ni Kitewele na Kimata vilivyopo wilayani Ludewa, pamoja na Kigulu, Chanjale, Lumbira na Nkanda vilivyopo upande wa Matema wilayani Kyela.
“Njombe kuna vijiji 381 na vyote tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme. Kati ya vitongoji 1,833 vilivyopo mkoani humo, vitongoji 1,249 tayari vimepata umeme na vitongoji 584 bado havijafikiwa na huduma hiyo,” amesema.
Kwa upande wake, msimamizi wa mradi huo kutoka Suma JKT, Yassin Selemani, amesema changamoto kubwa walizokutana nazo wakati wa utekelezaji ni milima mikali na hali mbaya ya hewa ikiwemo mvua, hali iliyowalazimu kusafirisha nguzo moja tu kwa siku, wakati mwingine wakitumia trekta kutokana na ugumu wa njia.
“Licha ya changamoto hizo, tumefanikiwa kusimamisha nguzo zote 105 na sasa tunasubiri vifaa kwa ajili ya kuvuta waya,” amesema.
Selemani amesema utekelezaji wa mradi huo pia umechangia kutoa ajira kwa wananchi wa eneo hilo, ambapo jumla ya watu 80 walipata fursa ya kufanya kazi wakati wa utekelezaji wake.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema miradi ya kusambaza umeme vijijini inayotekelezwa na Rea inaonesha wazi namna makato ya asilimia tatu ya ununuzi wa umeme yanavyotumika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Balile amesema mradi huo ni ushahidi kuwa michango ya wananchi kupitia makato hayo inarejea kwa jamii kwa kugharamia miradi ya maendeleo.
“Tumeshuhudia vitongoji sita vilivyopo katika mazingira magumu vikielekea kupata huduma ya umeme. Hii inaonesha wazi kuwa ile asilimia tatu inayokatwa kila tunaponunua umeme kupitia Rea inafanya kazi,” amesema Balile.
Ameongeza kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila wananchi kushiriki kugharamia miradi ya maendeleo.
“Hakuna mahali tunaweza kupiga hatua bila kugharamia maendeleo yetu wenyewe. Ni lazima tuchangie maendeleo ili nchi yetu ipige hatua hata bila kusubiri wafadhili,” amesema.
