Kili Marathon Yatangaza barabara zitakazofungwa siku ya mbio

 

Wiki moja tu kabla ya kuanza kwa Kilimanjaro Premium Lager International Marathon, waandaaji wa mbio hizi zenye hadhi ya kimataifa wametoa mwongozo wa kina kwa wananchi na washiriki, ikiwemo taarifa za kufungwa kwa barabara, maegesho, na masuala mengine ya kiitifaki. Tukio hili linalosubiriwa kwa hamu kubwa litafanyika Jumapili, Machi 22, 2026, katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji, barabara kuu kama Sokoine kutoka kona ya KCMC hadi Barabara ya Kilimanjaro itafungwa kuanzia saa 12 asubuhi hadi 3:30 asubuhi. Madereva wanashauriwa kutumia njia mbadala kupitia Shanty Town na Rau, huku barabara nyingine kuelekea Mweka pia zikifungwa kuanzia saa 12:30 asubuhi hadi 2:30 asubuhi. Vilevile, barabara za Moshi Klabu hadi Weru Weru kupitia daraja la zamani na klabu ya Wessa zitaathirika kuanzia saa 1:15 asubuhi hadi 3:15 asubuhi.

“Hii itawawezesha wakimbiaji kufika kwenye maegesho yaliyoko kwenye shule ya polisi (TPS/CCP) na MoCU kwa urahisi, pamoja na kutoa nafasi ya kuanza mbio bila vikwazo,” ilisema taarifa hiyo. Barabara zote zitadhibitiwa kwa makini na askari wa usalama barabarani, hasa maeneo kama Umbwe, kuhakikisha washiriki wanakimbia kwa usalama.

Waandaaji pia wametoa taarifa kuhusu maegesho: hakutakuwa na maegesho katika Barabara ya Sokoine kutoka kona ya Barabara ya Kilimanjaro, na magari yoyote yatakayopakiwa hapa yatachukuliwa na polisi. Hata hivyo, maegesho ya bure yatapatikana kwenye shule ya polisi na eneo la MoCU, likiwa umbali wa dakika chache kutoka sehemu ambapo mbio za kilomita 42, 21 (Half Marathon) na 5 km (CRDB Fun Run) zitaanza.

Kwa upande wa ukusanyaji wa namba za ushiriki, zoezi hilo linaanza Ijumaa, Machi 13, 2026 katika Duka la Mlimani City, kuendelea Arusha kati ya Machi 17–18, na hatimaye Moshi kuanzia Machi 19–21, 2026 kwenye Uwanja wa MoCU. Tiketi za mbio za CRDB Fun Run 5Km bado zinapatikana, na washiriki wanashauriwa kuchangamkia fursa hii.

Wadhamini wa mwaka huu ni pamoja na Kilimanjaro Premium Lager (mdhamini mkuu wa mbio za 42 km), YAS (21km Kili Half Marathon), na CRDB Bank (mbio za kujifurahisha za 5 km). Wadhamini wasaidizi ni pamoja na Kilimanjaro Water na TPC Sugar, huku washirika rasmi wakiwemo GardaWorld Security, Toyota Tanzania, Columbia Sportswear, Simba Cement, Harleys Healthcare Solutions na ALAF Limited. Wasambazaji rasmi ni Salinero Hotel, Kibo Palace Hotel Arusha na Keys Hotel Moshi.

Waandaaji wa Kilimanjaro Marathon Company Limited, kwa ushirikiano na Wild Frontiers Events, wamesema kuwa maandalizi yote ya usafiri, usalama na masoko yamekamilika, kuhakikisha mbio za mwaka huu zinaenda kwa usalama na kufurahisha washiriki wote.