KUELEKEA mechi ya Dar es Salaam Dabi, itakayopigwa kesho Machi 15, kocha wa Azam, Florent Ibenge, ametaja sifa tatu za wapinzani hao huku akisema kuwa kocha wa Yanga, Pedro Goncalves ana ufundi wa hali ya juu.
Yanga inatarajiwa kuvaana na Azam kesho kwenye mchezo mkali wa Ligi Kuu zikiwa ni timu mbili ambazo hadi sasa hazijapoteza mchezo wowote tangu ligi ilipoanza, Yanga ipo kileleni ikiwa na pointi 35 baada ya kucheza michezo 33, huku Azam ikiwa nafasi ya tatu na pointi 27 ikiwa imecheza mechi sawa na Yanga, pia ndiyo timu ambazo zimefunga mabao mengi kwenye ligi hadi sasa, Yanga wamefunga 31 huku Azam ikifunga 21.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema mchezo ujao dhidi ya Yanga hautakuwa rahisi kwani wanakwenda kukutana na timu yenye sifa tatu.
Alisema kuwa anawaamini sana mastaa wa kikosi hicho kwamba watakwenda kufanya kitu na kupata matokeo mazuri.
“Sifa ya kwanza ni timu ambayo inaongoza ligi kwa sasa, ikiwa na kiwango bora cha kutokupoteza mchezo hata mmoja.
“Sifa ya pili ni timu yenye wachezaji waliokomaa na wenye uzoefu wa kucheza mechi kubwa na ngumu za ndani na nje ya ligi.
“Sifa ya tatu ni timu inayotaka kutetea ubingwa, imechukua mara nne mfululizo, hivyo inalinda heshima yake.”
Ibenge alisema timu yake itaingia kwenye maandalizi ya mchezo huo kwa lengo moja tu la kutaka kupunguza tofauti ya pointi baina ya timu hizo, kusiwe na utofauti mkubwa kama ilivyokuwa msimu uliopita.
“Nafurahia kwamba safu yetu ya ushambuliaji imeimarika kwa kufunga mabao matatu, ni hatua nzuri wakati tunaelekea kwenye mchezo mkubwa.
“Kuhusu Pedro kuja kuangalia mechi yetu dhidi ya Dodoma Jiji si kitu kibaya, ni hatua nzuri kwani siku zote Azam imekuwa ikiangaliwa na makocha tofauti.”
Matajiri hao wa Chamazi watakuwa wenyeji wa Mzizima Dabi, mchezo utakaowakutanisha na vinara wa ligi na mabingwa watetezi Yanga, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 2:30 usiku.
