Raundi 10 ZPL kuchezwa Gombani, Bodi yafafanua

KATIKA kuhakikisha Pemba inafunguka kimichezo, Bodi ya Ligi Zanzibar (ZBL) ipo katika mazungumzo ya kuomba kuutumia uwanja mkubwa wa Gombani katika raundi 10 zilizosalia za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).

Hatua hiyo inalenga kuzisaidia timu, hasa kutoka Pemba, kurushwa mubashara kama ilivyo za Unguja.

Katika misimu miwili mfululizo, mechi zinazochezwa kwenye Uwanja wa Mao Zedong uliopo Unguja, zimerushwa mubashara huku mechi zilizochezwa Pemba zikikosa fursa hiyo kwa madai ya uwanja unaotumika kutokuwa na viwango.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Issa Kassim alisema sababu ya kufanya hivyo ni kumpa nafasi mdhamini wa ligi hiyo kuweka usawa na kupunguza malalamiko kwa washiriki kutoka kisiwani Pemba.

“Kwa sasa timu zinatumia kiwanja cha nje katika Uwanja wa Gombani, ambacho si rafiki katika kuonyesha mechi mubashara, na kama mazungumzo yatakwenda vizuri, basi mashabiki wa ligi ndani na nje ya Zanzibar watashuhudia mubashara mechi za Pemba,” alisema Issa.

Ameeleza, Bodi hiyo inapambana kufanikisha hilo ili kuleta usawa baina ya Unguja na Pemba, lakini pia itasaidia sana kukuza ushindani wa soka visiwani.

Alisema kuwa Bodi itafuatilia hatua kwa hatua michezo yote itakayochezwa kuanzia mwenendo wa mechi, viongozi au mashabiki wa timu, ili kwa atakayebainika kufanya vitendo kinyume na sheria za mpira wa miguu achukuliwe hatua.

Pia, Mtendaji huyu alisema watakaa na klabu kuzikumbusha mashabiki wao na viongozi kuzingatia kanuni na sheria kabla ya kuendelea kwa mechi za Ligi kipindi cha lala salama.

Kwa kawaida, yapo matukio ambayo yanatokea kwenye baadhi ya mechi zinazochezwa Pemba, huku utolewaji wa uamuzi ukichukua mchakato, na wakati mwingine timu kutoridhika na adhabu zinazotolewa.

Hivyo basi, uamuzi wa kuzirusha mubashara mechi hizo zitakazochezwa Pemba, itawapunguzia mzigo Bodi hiyo na kurahisisha utendaji kazi.