Dosari za kisheria zamnusuru kunyongwa hadi kufa

Arusha. Mahakama ya Rufani imemwachilia huru James Kaliwa aliyehukumiwa adhabu ya kifo kwa kosa la mauaji, baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi yake bila shaka yoyote.

Uamuzi huo uliobatilisha adhabu hiyo umetolewa Machi 9,2026 na  jopo la majaji watatu ambao ni Ferdinand Wambali,Omar Othuman Makungu na Agnes Mgeyekwa.

Mahakama hiyo  ilibaini kuwa kulikuwa na mapungufu kadhaa makubwa katika kesi ya upande wa mashtaka ikiwemo kutokuwepo kwa ushahidi wa kuthibitisha kuwa mtu aliyedaiwa kuuawa ndiye Iddi kama ilivyoelezwa katika shtaka.

Aidha, hakukuwa na ushahidi unaoonyesha kuwa mabaki ya viungo vya binadamu yaliyopatikana yalikuwa ya mtu huyo, ambapo ilibaini kuwa upande wa mashtaka haukuwasilisha amri ya mahakama ya kufukua mabaki ya binadamu ambayo ilidaiwa kuwa ilitolewa wakati wa uchunguzi.

Nyingine ni kutokuwepo kwa amri hiyo kuliweka shaka kuhusu uhalali wa mabaki yaliyodaiwa kupatikana kutoka eneo la tukio.

Jaji Wambali amesema kasoro nyingine iliyobainika ni kutokuitwa kwa shahidi muhimu aliyehusika katika kusafirisha mabaki ya viungo vya binadamu kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi wa maabara.

Mahakama ilieleza kuwa ushahidi wa shahidi huyo ungeweza kusaidia kueleza mnyororo wa utunzaji na usafirishaji wa vielelezo muhimu katika kesi hiyo, na kuwa kutoitwa kwa shahidi huyo kulifanya ushahidi uliotolewa kuwa na mapungufu makubwa.

Baada ya kuchambua ushahidi wote pamoja na hoja za pande zote, Mahakama ya Rufani ilifikia hitimisho kuwa kesi ya upande wa mashtaka haikuthibitishwa bila shaka yoyote na kuwa mapungufu yaliyokuwepo katika ushahidi yalikuwa makubwa kiasi kwamba hayakuweza kuunga mkono hatia ya mrufani.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama iliruhusu rufaa hiyo, ikafuta hukumu ya hatia na adhabu ya kifo iliyotolewa na Mahakama Kuu na kuamuru mrufani aachiliwe huru mara moja kutoka kizuizini isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.

Kupitia wakili wake, mrufani huyo aliwasilisha sababu tano za kupinga hukumu hiyo ikiwemo madai kuwa upande wa mashtaka haukuonyesha mnyororo sahihi wa utunzaji wa viungo vya binadamu vilivyotumika kama ushahidi.

Alidai pia kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kumwita shahidi muhimu aliyekuwa amehusika katika kusafirisha mabaki ya viungo vya binadamu kwenda maabara kwa uchunguzi.

Upande wa mjibu rufaa uliunga mkono rufaa hiyo baada ya kubaini mapungufu makubwa katika ushahidi uliotolewa katika Mahakama Kuu.

Kesi ya awali ilihusisha tukio la Julai 2017 katika kijiji cha Jisesa, wilayani Busega, mkoani Simiyu, ambapo James Kaliwa alishtakiwa kumuua mtu aliyejulikana kama Iddi.

Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita na vielelezo vitano, ikiwemo mabaki ya viungo vya binadamu yaliyopatikana nyumbani kwa Mathias, mtu aliyehusishwa na tukio hilo.

Uchunguzi wa maabara ulionyesha kuwa mabaki hayo yalitoka kwa mtu mmoja, huku baadhi yake yakionyesha DNA inayolingana na damu iliyopatikana kwenye nguo zilizowasilishwa.

Mahakama Kuu, ikitegemea ushahidi wa mazingira na ushahidi wa mashahidi, iliona kuwa mnyororo wa matukio unaomuunganisha mrufani na mauaji ulikuwa dhahiri, na kumuhukumu James Kaliwa adhabu ya kifo kwa kunyongwa.