Unguja. Abdulazizi Ali Khamis amepata kitita cha Sh30 milioni baada ya kuibuka kidedea katika mashindano ya kuhifadhi Quran yaliyofanyika Zanzibar.
Mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya tatu mfululizo, yamewashirikisha washiriki 11 kutoka mabara sita katika mataifa ya Uingereza, Brazir, Comoro, Tunisia, Australia, Afrika Kusini, Marekani, Nigeria, Tanzania na mwenyeji Zanzibar.
Mshindi wa pili kutoka nchini Nigeria, Ibrahim Usman amepata Sh20 milioni na mshindi wa tatu kutoka Marekani, Hafidh Adam akipata Sh10 milioni huku washiriki wengine wanane wakipata Sh3 milioni kila mmoja.
Katika mashindano hayo ambayo yamefanyika leo Machi 14, 2026 uwanja wa New Amani Complex Unguja, mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ambapo amesema hatua hiyo inaonesha jinsi ambavyo kuna umuhimu kuendelea kufanya mambo makubwa kama hayo katika kisiwa hicho
Amesema washiriki wote wameonesha umahiri mkubwa jambo linaloashiria kuwepo na maandalizi makubwa na mazuri katika kusimamia misingi ya kitabu kitukufu cha mwenyezi Mungu.
“Hili ni jambo jema kwani linachochea pia ukuaji wa sekta ya utalii kupitia matukio na matamasha, tuendelee kuyaunga mkono mashindano haya ili nchi yetu iendelee kupata utambulisho mwema duniani na kunufaika na faida mbalimbali zinazotokana na mashindano haya,” amesema Dk Mwinyi.
Dk Mwinyi amesema mashindano hayo yamekuwa kivutio na utambulisho mwingine wa Zanzibar katika uga wa kimataifa ni, “ni dhahiri taarifa za mashindano haya yameenea kila kona duniani na kufuatiliwa watu mataifa mbalimbali.”
Kiongozi huyo mkuu wa Zanzibar, amesema mafundisho ya Kiislamu yanawaelekeza Quran ndio mwongozo wa viumbe vyote kwa hiyo hawana budi kushika mwongozo huo na kuufanyia kazi ili kuwe na jamii inayoogopa kwa mwangaza wa vitabu hivi vitukufu.
Amewasihi washiriki hao kwamba wasiwe washindi wa kupata zawadi na cheti bali ni kupata radhi na kuishi kwa mujibu wa mafundisho ya Quran ya kuwa na tabia njema.
Amesema kuhamasika huko inaonesha wazi kuna mshikamano na umoja miongoni mwao na kuleta maendeleo ya nchi hivyo waombe Mungu aendelee kuwazidishia amani na mshikamano kwa kuzingatia mafundisho yake.
Kwa upande wa jamii ameitaka iimarishe maadili na tabia njema na kutunza amani na mshikamano wao hivyo watakuwa wamekitendea wema kitabu hicho kitakatifu.
Amesema washiriki wote ni washindi na kazi kubwa imefanyika kuwaandaa vijana hao. “Niwapongeze vijana kazi kubwa waliyoifanya,” amesema.
Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema matukio kama hayo yanaendelea kuitangaza Zanzibar kimataifa na kujenga mshikamano miongoni mwa Wazanzibari na mataifa mengine.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohamed Ali amesema ni katika historia ya Zanzibar imekuwa na umoja na mshikamano kupiia matukio hayo ambapo imeendelea kuonekana duniani kote.
Naye mshindi wa kwanza amesema kushika nafasi hiyo sio kwa uwezo wake bali ni kutokana na malezi ya wazazi na maandalizi ya walimu wake.
