Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Makame amemwagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Songwe kundaa na kutekeleza mpango wa muda mfupi, utakaoweza kuleta nafuu ya tatizo la umeme katika Wilaya ya Songwe ikiwemo maeneo yanakochimbwa madini.
Makame ametoa maagizo hayo akiwa ziarani wilayani Songwe kukagua hali ya upatikanaji wa umeme katika migodi ya madini kwa wachimbaji wa kati na wadogo.
Amesema ukosefu wa umeme wa uhakika katika Wilaya ya Songwe umetajwa kuathiri shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kuwa kikwazo kikubwa katika maendeleo ya sekta hiyo na uwekezaji.
“Nimetoa maagizo hayo wa Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) kufuatia kampuni nyingi za uchimbaji wa madini kulalamika kwamba wanatumia gharama kubwa kuendesha mitambo kwa kutumia mafuta, huku wachimbaji wengi wadogo wakisema wanakosa kufanya shughuli zao kutokana na changamoto hiyo,” amesema Makame.
Akizungumza na wananchi na wadau wa sekta ya madini, Makame amesema ili kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa pamoja na dira ya maendeleo, ni lazima Serikali iendelee kuweka mazingira yatakayowawezesha wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa kufanya shughuli zao bila vikwazo.
Ameeleza kuwa kwa sasa Wilaya ya Songwe inakabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, umeme usio na nguvu ya kutosha pamoja na kutokidhi mahitaji ya wananchi na wawekezaji.
Amesema hali hiyo inatokana na kasi kubwa ya maendeleo na uwekezaji unaoendelea katika sekta ya madini na shughuli nyingine za kiuchumi.
“Miaka kadhaa iliyopita uwekezaji katika sekta ya madini haukuwa mkubwa kama ulivyo sasa, jambo linaloifanya Serikali kuongeza jitihada za kuhakikisha miundombinu ya umeme inaendana na kasi ya maendeleo ya wananchi.
“Mkoa wa Songwe bado haujaunganishwa kikamilifu kwenye Gridi ya Taifa, jambo linalochangia changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika hivyo Serikali, tayari imetoa fedha za kutekeleza miradi mikubwa ya umeme mkoani humo,” ameongeza Makame.
Kwa upande wake, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Songwe, Mhandisi Tumaini Chonya ameeleza kwamba Serikali kwa sasa inatekeleza mipango ya kudumu ya kutatua changamoto ya umeme ikiwemo ujenzi wa mradi wa Taza ambao utauingiza mkoa huo kwenye Gridi ya Taifa, na mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea umeme katika Mji wa Saza ambao upo katika hatua za awali.
“Tanesco inatarajia kujenga laini maalumu ya umeme kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini, hatua ambayo itasaidia kupunguza mzigo kwenye laini,” amesema Mhandisi Chonya.