CRDB BANK YAKUTANISHA VIONGOZI NA WATEJA MOROGORO KATIKA FUTARI YA RAMADHANI

Farida Mangube, Morogoro

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani na hata baada ya kumalizika kwa mwezi huo.

RC Malima ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya wateja wake pamoja na wadau mbalimbali wa benki hiyo mkoani Morogoro.

Amesema kipindi cha Ramadhani ni muda muhimu kwa waumini wa Kiislamu kujitathmini, kufanya ibada na kuimarisha mahusiano mema, huku akisisitiza kuwa maombi yana mchango mkubwa katika kulinda amani na maendeleo ya taifa.

“Niwaombe Watanzania wote kutumia kipindi hiki cha Ramadhani kumuomba Mwenyezi Mungu alinde amani ya nchi yetu na atupe moyo wa upendo na mshikamano ili tuendelee kujenga taifa lenye maendeleo,” alisema Malima.

Aidha, alimshukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa futari hiyo ambayo imewaleta pamoja viongozi, wateja na wadau mbalimbali katika kuimarisha mahusiano na mshikamano ndani ya jamii.

Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Kati Benki ya CRDB Bi Chabu Mishwaro amesema lengo la kuandaa futari hiyo pamoja na dua maalum ni kushiriki ibada na kuungana na wateja wao katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Amesema benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kukutana na wateja wake katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuimarisha na kuendeleza ushirikiano wa kibiashara pamoja na kushirikiana katika matendo ya kijamii yenye kuleta baraka kwa jamii.

“Futari hii ni sehemu ya kuonesha kuthamini wateja wetu ambao wamekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya benki yetu. Tunathamini sana mahusiano haya na tunaamini kuungana katika ibada na dua kunaimarisha mshikamano wetu,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa benki hiyo Mussa Kitambi amesema imekuwa ni utamaduni wa CRDB Bank kuandaa futari kwa ajili ya wateja wake kila mwaka katika mwezi wa Ramadhani.

Amesema mwezi mtukufu wa Ramadhani ni chuo cha malezi ya kiroho na nidhamu kwa waumini wa Kiislamu, huku swaumu ikiwa ni ibada inayowafanya watu wengi kuelekeza mioyo yao katika kumtii Mwenyezi Mungu, kufanya wema na kusaidia wenye uhitaji.

Aliongeza kuwa benki hiyo imekuwa ikiendelea kutoa huduma mbalimbali zinazozingatia mahitaji ya wateja Waislamu, ikiwemo programu maalum za huduma za kifedha zisizo na riba ili kuwawezesha kutimiza majukumu yao ya kiibada na kimaendeleo kwa mujibu wa misingi ya dini ya Kiislamu.

“Tunatoa huduma za uwezeshaji wa kifedha zisizo na riba kwa wateja wetu ili kuwasaidia kutekeleza shughuli zao za kiuchumi bila kwenda kinyume na misingi ya imani yao. Tunawaomba wateja wetu waendelee kuiamini na kushirikiana na benki yetu,” alisema.

Futari hiyo pia iliambatana na utoaji wa zawadi na misaada mbalimbali kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kurejesha kwa jamii na kuonesha mshikamano katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.