Dar/mikoani. Mtu mmoja amefariki dunia ka kusombwa na maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi. Huku katika baadhi ya maeneo shughuli zikisimama kufuatia mvua hizo.
Usiku wa kuamkia jana ilinyesha mvua kubwa iliyoambatana na ngurumo za radi ilisababisha kuharibu barabara na kuwakwamisha wananchi katika shughuli zao za kila siku.
Katibu wa Mbunge wa Simanjiro (James Ole Millya), Frank Oleleshwa, alisema amepata taarifa ya kufariki dunia kwa mvuvi mmoja wa bwawa la Kidawashi aliyesombwa na maji katika Kata ya Shambarai.
Mbali na tukio hilo, viongozi mbalimbali wamezungumzia hali ilivyo katika ameneo yao, ambapo yapo yenye changamoto na mengine yalikuwa shwari.
Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Brigedia Jenerali Wilson Sakulo, alisema imekuwa shida kuyafikia baadhi ya maeneo wilayani humo, hivyo hata tathmini ya athari imekuwa vigumu kuifanya.
“Kuna Mto Munic unaojaa maji mimi kwa sasa niko Arusha ila wakati nakuja hivi nilikaa pale kama saa sita hapapitiki, mpaka maji yapungue ni changamoto kwelikweli, ila kesho ninarudi Jumatatu nitafute nitakupa taarifa zaidi,” alisema
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alisema hakuna athari za moja kwa moja zilizojitokeza, zaidi ya maji kujaa na kuondoka katika baadhi ya maeneo.
“Wanaolalamikia barabara ni ngumu kuzitengeneza wakati mvua zinaendelea, lakini mipango mikakati ipo, kukinyauka kidogo zitatengenezwa,” alisema.
Diwani wa Endiamtu, Lucas Zacharia, aliwaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanawatunza watoto ili wasichukuliwe na mafuriko.
“Hata hivyo, tunashukuru hakuna madhara ya vifo kwa binadamu zaidi ya maji kuzunguka makazi au mazao mashambani kuchukuliwa na maji,” alisema.
Kwa upande wa Unguja visiwani Zanzibar, mvua hizo hazijasababisha madhara kwa uhai wa binadamu wala kusimamisha shughuli kama anavyoeleza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma.
“Ni kweli leo imenyesha mvua kubwa wakati wa usiku na alfajiri, lakini bado tupo salama hakuna athari yoyote kupitia taarifa tulizonazo mpaka sasa,” alisema alipozungumza na Mwananchi jana saa 3:00 asubuhi.
Katika kukabiliana na athari za mvua ambazo tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ilitoa tahadhari, alisema tayari wameanza kujenga mitaro katika baadhi ya maeneo.
“Unajua Zanzibar kila mwaka wakati wa mvua za masika tulikuwa tukipata madhara, barabara nyingi hazikuwa na mitaro, sasa tumeshaanza kutengeneza mitaro hiyo kwa hiyo maji hayapati tena nafasi ya kutuama,” alisema
Katika Jiji la Dar es Salaam, mvua zilizonyesha zimeacha athari katika baadhi ya barabara ikiwemo ya Tabata Kimanga wilayani Ilala, iliyojaa madimbwi ya maji na kusababisha ugumu wa kupitika.
Dereva wa daladala anayefanya safari za Kimanga hadi Muhimbili, Shedrack Mrope, alisema hali ya barabara hiyo inaleta changamoto kwa madereva.
“Dimbwi ni kubwa sana na hapa sio sababu ya mvua ya jana tu ni zaidi ya mwaka, wakati mwingine tunalazimika kupita mtaani ili kuepuka kuharibu gari au kukwama kwenye maji, hii inatupotezea muda na pia inaathiri ratiba ya safari,” alisema.
Muuza duka eneo la Shiba, Rehema Samson, alisema wateja wengi wanashindwa kufika kwa sababu ya maji yaliyotuama.
“Maji yamejaa wateja wengine wanaogopa kupita hapa kwa sababu ya madimbwi na wengine wanapita mbali au wanaamua kwenda sehemu ambazo hakuna maji,” alisema.
Alisema wameshaomba kuboreshewa mifereji, lakini hilo halijawahi kutekelezwa, zaidi ya barabara kukwanguliwa na kufukiwa kwa mifereji, hali inayosababisha maji yanakosa njia na yanatuama barabarani.
Imeandikwa na Janeth Mushi (Arusha), Joseph Lyimo (Manyara), Devotha Kihwelo (Dar), Jesse Mikofu (Unguja)
