Dar es Salaam. Magari ya mizigo, mabasi ya abiria, daladala na magari binafsi yanaendelea kupishana kwa kasi katika Barabara ya Mandela, mojawapo ya barabara muhimu inayounganisha maeneo mbalimbali ya jiji ikitokea bandarini.
Lakini, kadiri magari yanavyokaribia kipande kabla ya kuzifikia taa za barabarani zilizo chini ya daraja la Mfugale lililopo eneo la Tazara inawalazimu madereva kupunguza mwendo na kuongeza umakini.
Kwa mujibu wa watumiaji wa barabara hiyo sababu si msongamano wa magari pekee, bali ni matuta na mikunjo iliyotokea katikati ya barabara.
Hali hii ipo pia katika kipande cha barabara eneo la Tabata Matumbi kabla ya kuvuka mataa ya Tabata, pia hivyo pia eneo la Mabibo External kabla ya kuvuka taa.
Mwananchi ilitembelea katika maeneo hayo na kubaini kuwa katika baadhi ya sehemu za barabara hiyo tabaka la juu limeanza kuvimba na kutengeneza matuta makubwa, ambayo yanawalazimu madereva kupunguza mwendo ili kuepuka uharibifu wa magari au ajali.
Madereva waliozungumza na gazeti hili wameeleza hali hiyo imeanza kusababisha taharuki hasa kwa wale wanaopita eneo hilo kwa mara ya kwanza au wakati wa usiku.
Dereva wa lori, Hassan Juma, amesema wakati mwingine madereva hulazimika kupunguza mwendo ghafla wanapokutana na matuta hayo kwa sababu hali hiyo husababisha mtikisiko mkubwa ambao unaweza kuharibu baadhi ya mifumo ya gari.
“Ukifika hapa ghafla unakutana na tuta katikati ya barabara. Kama ulikuwa unaendesha kwa mwendo wa kawaida lazima upunguze haraka kwani gari inaweza kuyumba na kama ndiyo una mzigo basi hatari yake ni kubwa.
“Lori likipanda tuta kubwa linatikisika sana. Sasa fikiria magari madogo au pikipiki, kwao inaweza kuwa hatari zaidi,” ameeleza.
John Mallya, dereva wa teksi anayepita barabara hiyo mara kwa mara, amesema hali hiyo imeanza kuwa kero kwa madereva wengi.
“Hii barabara ilikuwa nzuri sana, lakini sasa imeanza kuvimba sehemu kadhaa. Ukiwa hujui unaweza kuharibu gari lako. Unapojaribu kulikwepa unaweza kujikuta unaingia upande mwingine wa barabara kama huna tahadhari,” amesema.
Salim Mussa, dereva wa daladala ya Mbagala-Mbezi amesema madereva wengi wameanza kuzoea kupunguza mwendo wanapofika kipande hicho cha barabara.
“Ukifika hapa lazima uwe makini. Ukipanda tuta kwa kasi abiria wote wanahisi mtikisiko mkali ndani ya gari,” amesema.
Mbali na hatari ya ajali, madereva wanasema matuta hayo yanaongeza gharama za matengenezo ya magari yao.
“Magari yanapata mishtuko kila siku. Hii inaathiri sana ‘shock absorber’,” amesema Daudi Ezekiah ambaye pia ni dereva wa daladala.
Balozi wa usalama barabarani, William Mwakyusa, amesema matuta barabarani yanaweza kuwa hatari, hasa kwa waendesha pikipiki na magari madogo.
Ameeleza kwamba hatari hiyo huongezeka zaidi wakati wa usiku au mvua, ambapo mwonekano wa barabara hupungua.
“Dereva anapokutana na tuta kubwa bila kulitegemea anaweza kupoteza udhibiti wa gari au pikipiki. Ndiyo maana ni muhimu barabara inapopata dosari kama hizi ifanyiwe matengenezo mapema ili kulinda usalama wa watumiaji,” amesema Mwakyusa.
Hali hii inasababishwa na nini?
Wataalamu wa ujenzi wa barabara wameeleza kuwa hali ya kuvimba kwa barabara na kutengeneza matuta inaweza kuwa ishara ya uchakavu wa miundombinu au mzigo mkubwa unaopita katika barabara husika.
Kuhusu barabara ya Mandela, Mhandisi wa barabara, Fredy Nyenga amesema imezidiwa na mizigo, ndiyo maana mataifa yaliyoendelea yanahimiza matumizi ya usafiri wa treni katika usafirishaji wa mizigo.
“Usanifu wa barabara ya lami una ukomo wake. Ukizidi kiwango hicho, ni lazima kuweka barabara ya zege ili iweze kudumu vizuri. Ukienda bandarini utaona barabara nyingi zimejengwa kwa zege, jambo linaloonyesha kuwa zimebeba mizigo mikubwa kupita uwezo wa lami,” amesema.
Amesema barabara hiyo imezidiwa kwa sababu inatumiwa na malori mengi yenye mizigo mizito, hali inayozidi kiwango kinachopaswa kubebwa na barabara ya lami, suluhisho linalofaa ni kujenga ya zege ambayo inaweza kuwa salama na imara zaidi.
“Endapo itashindikana kujenga barabara ya zege, basi zijengwe bandari kavu nyingi nje ya Dar es Salaam ili kupunguza idadi ya magari. Pia, yajengwe maeneo kama Vigwaza mkoani Pwani ili malori yapungue,” amesema.
Nyenga amesema kitaalamu barabara ya lami huwa na uwezo wa kunyumbulika; gari linapopita huibonyea chini na baada ya kupita hurudi juu.
Hata hivyo, hali huwa tofauti katika barabara hii, ambapo magari mengi hukaa yamepaki kwa muda mrefu kutokana na msongamano.
“Magari mengi yanayopaki ni yenye mizigo mizito. Hali hiyo hujitokeza hasa karibu na matuta, mizani na mataa ya kuongozea magari, ambako magari hulazimika kusimama kwa muda mrefu,” amesema.
Amesema kuendelea kutumia barabara ya lami kunasababisha gharama kubwa za matengenezo.
Pia, barabara hiyo haiwezi kubaki katika hali nzuri muda wote kiasi cha kumwezesha dereva kuendesha vizuri bila changamoto.
“Barabara itaendelea kuwa na manundu na matuta mengi. Inashangaza kuweka kitu cha gharama kubwa lakini hakidumu. Matengenezo yake ni ya gharama kwa sababu kila baada ya muda mafundi hulazimika kufanya marekebisho na kuweka lami upya,” amesema.
Amesema kutokana na hali hiyo, uhai wa barabara ya lami unaotarajiwa kufikia miaka 15 unaweza usifike huko.
Mtaalamu kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Lazaro Kumbo, amesema tatizo la barabara hiyo linatokana na ukosefu wa usimamizi mzuri katika kudhibiti uzito wa magari yanayopaswa kupita.
“Utakuta kuna magari makubwa yanabeba mizigo kutoka bandarini yenye uzito unaozidi kiwango cha uwezo wa barabara, jambo ambalo linakuwa chanzo cha barabara kubonyea,” amesema.
Kumbo ameshauri kuwa wasimamizi wa barabara wanapaswa kuzingatia utaratibu wa kuhakikisha uzito wa gari linalopita unaendana na aina ya barabara iliyopo.
“Barabara zimetengenezwa na kuwekwa ukomo wa uzito wake. Sasa ukipitisha gari lenye uzito unaozidi uwezo huo, barabara huharibika, kutitia au kuwa na mikunjo. Sidhani kama kuna usimamizi wa kutosha kwenye barabara hiyo,” amesema Kumbo.
Hilo limeelezwa pia na Mhandisi Milton Nyerere ambaye amesema barabara hiyo inapitiwa na magari yenye uzito mkubwa kuliko ule uliotumika katika usanifu wake, huku pia ikiwa imepita muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo ya tabaka la juu.
“Barabara ya lami ina umri wake. Kwa kawaida, baada ya miaka 15 tabaka la juu linapaswa kutolewa na kuwekwa lingine. Wakichelewa kufanya hivyo, madhara yake ni kama haya, ikiwemo kuwa na mikunjo. Sikumbuki Mandela Road ilifanyiwa maboresho hayo lini,” amesema.
Nyerere amesema hatua muhimu inayotakiwa kuchukuliwa ni kuimarisha barabara hiyo kwa kubadilisha tabaka la juu, jambo ambalo litasaidia kurejesha ubora wake.
Mtaalamu wa uhandisi wa barabara, Joseph Mrema, amesema barabara nyingi hujengwa kwa kuzingatia kiwango fulani cha uzito wa magari yanayotarajiwa kupita.
“Endapo magari yenye uzito mkubwa yanapita mara kwa mara kuliko kiwango kilichopangwa, inaweza kusababisha tabaka la juu la barabara kuharibika au kuvimba,” amesema.
Amesema maji ya mvua pia yanaweza kuwa sababu ya kuharibika kwa sehemu za barabara ikiwa yataingia katika tabaka la chini la barabara.
“Maji yanapopenya chini ya barabara yanaweza kusababisha udongo kulegea na hatimaye barabara kuanza kuvimba au kupasuka. Ikiwa matengenezo hayatofanyika mapema, hali hiyo inaweza kuendelea kuwa mbaya zaidi na kusababisha mashimo au nyufa kubwa katika barabara
Akitoa ufafanuzi kuhusu hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Ephatar Mlavi, amesema hali hiyo inachangiwa na mambo mbalimbali, ikiwemo umri wa barabara kutumika kwa muda mrefu, aina ya udongo pamoja na uzito wa mizigo inayobebwa, ambayo inaweza kusababisha kutokea kwa mibonyeo hiyo.
“Mibonyeo hiyo huwa inajitokeza katika barabara za lami, na tunachokifanya ni kutuma wataalamu wetu kuangalia na kufanya tathmini ili kubaini marekebisho yanayoweza kufanyika kwa lengo la kuiondoa,” amesema.
Katika maelezo yake, amesema huwa wanafuatilia mtandao wa barabara zao mara kwa mara na kuzifanyia maboresho ili watumiaji waweze kupita kwa usalama zaidi.
“Hata hiyo barabara unayosema tutatuma wataalamu wetu wafuatilie ili tuweze kufanyia maboresho ili kuondoa mibonyeo hiyo,” amesema
Barabara ya zege ni suluhu
Kukabiliana na uharibifu huo, mhandisi wa barabara, Fredy Nyenga ameshauri kujengwa barabara ya zege, akieleza kuwa ni rahisi zaidi kwa sababu malighafi nyingi zinapatikana ndani ya nchi.
“Kokoto, saruji na nondo vinazalishwa hapa nchini, lakini lami hutoka nje na huongeza gharama za usafirishaji. Ikiwa mahitaji hayo yapo hapa nchini, kwa nini kila jambo liwe changamoto?” amehoji.
Amefafanua ujenzi wa barabara ya zege hauhitaji mitambo mingi kama ilivyo kwa lami. Zege inaweza kujengwa kidogo kidogo na ikishajengwa kwa ubora haihitaji kurudiwa tena mara kwa mara, isipokuwa kunahitajika utashi wa kufanya hivyo.
