VINARA wa Ligi Daraja la kwanza Kanda ya Unguja, Black Sailors, wamesema msimamo umekuwa hamasa nzuri ya kuanza mazoezi kwa ari zaidi.
Kauli hiyo imetolewa na Kocha Msaidizi, Said Mwinyi akisema amefurahishwa na namna wachezaji walivyoanza mazoezi kwa ari kubwa.
Black Sailor inaongoza ligi hiyo kwa pointi 53 ilizovuna katika mechi 20 na kubakisha mechi 10 kukamilisha msimu wa 2025-2026.
“Wachezaji wanaendelea kuonyesha kiwango kizuri na utimamu wa mwili tangu walivyorejea mazoezini kutoka mapumziko mafupi kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, hali inayotupa matumaini makubwa benchi la ufundi kuelekea michezo iliyobaki,” amesema.
Amesema sio kawaida kwa timu kuanza mazoezi kwa ari kubwa kwani hawakuonekana kama walikuwa wametoka katika mapumziko akibainisha jambo hilo linaashiria wengi wao waliendelea kufanya mazoezi binafsi wakati wa kipindi chote cha mapumziko.
“Mazoezi yanaendelea vizuri na wachezaji wanaonesha kujituma kwa kiwango kikubwa, hali yao ya mwili ni nzuri na inaonekana walikuwa wanafanya mazoezi binafsi hata wakati wa mapumziko,” alisema Mwinyi.
Baada ya ligi hiyo kurejea, Black Sailors mchezo wake wa kwanza itacheza Machi 30, 2026 dhidi ya Sebleni United, kisha Aprili 6, dhidi ya ZAFSA. Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, timu mbili za juu katika msimamo wa ligi zitapanda daraja kucheza Ligi Kuu Zanzibar, wakati timu nne za mwisho zikishuka daraja la pili Mkoa. Ligi hiyo ina timu 16.