MEELA AWAOMBA VIONGOZI WA DINI KUKEMEA SWALA LA WIZI.

MOSHI. 

Wimbi la wizi, hasa wa mita za maji, limeendelea kuwa changamoto kubwa katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, hali inayozua wasiwasi kwa wananchi na viongozi wa jamii.

Kutokana na hali hiyo, viongozi wa dini wametakiwa kutumia nafasi zao kuzungumzia na kukemea vitendo hivyo pamoja na kuwaombea vijana wanaojihusisha na uhalifu ili waweze kubadilika na kurejea katika maadili mema.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, John Meela, wakati akitoa msaada wa vyakula kwa ajili ya futari kwa baadhi ya waumini katika Msikiti wa Njiapanda, wilayani Moshi, ikiwa ni sehemu ya kushirikiana na jamii katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Meela, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Njiapanda, amesema wizi huo umekuwa ukiongezeka katika kipindi cha hivi karibuni, huku akitaja wizi wa mita kuwa miongoni mwa matukio yanayolalamikiwa zaidi na wananchi.

 Amesisitiza kuwa ushirikiano wa viongozi wa dini na jamii kwa ujumla ni muhimu katika kudhibiti vitendo hivyo.

Ameongeza kuwa ushirikiano na mshikamano katika jamii ni muhimu, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kuombeana na kushirikiana ili kuimarisha amani na maendeleo ya eneo hilo.

“Katika kipindi hiki cha Ramadhani huwa napenda kutembelea misikiti na kushiriki na jamii kwa kutoa kile ambacho Mungu amenijalia, ili tushirikiane na kusaidiana. Leo nimeona ni vyema kuja katika msikiti wetu hapa Njiapanda,” amesema Meela.

“Ndugu zangu Waislamu na wananchi kwa ujumla,  ni muhimu tuendelee kushirikiana, kuombeana na kumuomba Mungu atujaalie zaidi ili wakati mwingine tuweze kusaidiana na kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kijamii,” amesema.