Chaumma yaingia TCD na matarajio makubwa

Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimedhamiria kutumia uanachama wake wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) katika kukuza demokrasia nchini.

Hayo yamebainishwa  Machi 13, 2025 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu wakati wa Iftar iliyoandaliwa na TCD, ikiwashirikisha wadau tofauti wa demokrasia vikiwamo vyama vya siasa.

Akizungumza na mwananchi kwenye hafla hiyo, Mwalimu amesema hii ndiyo mara ya kwanza kwa Chaumma kuwa mwanachama wa TCD baada ya kukidhi vigezo kwa kupata wawakilishi bungeni na kwenye mabaraza ya madiwani.

Katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, Chaumma kilifanikiwa kupata wabunge wawili, mmoja akishinda jimbo la Segerea na mwingine akichaguliwa kuwa mbunge wa viti maalumu akitoka kwenye chama hicho. Hivyo, wamekidhi vigezo vya kuingia TCD kwani wamepata wawakilishi.

“Hatujawahi kuwa wanachama wa TCD, huu ndio mkusanyiko wetu wa kwanza, kwa hiyo kama wanachama tutatoa mchango wetu katika kuhakikisha kwamba demokrasia inashamiri, haki inashamiri na Watanzania wanapata maendeleo,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Tuna wajibu wa kuwaeleza wanachama wetu kuhusu nini maana ya TCD, nini wajibu wetu na nini faida ya kuwa mwanachama wa TCD.”

Mwalimu amefafanua kuwa sasa uchaguzi umekwisha, chama kimekaa na kutengeneza mikakati ya kukirudisha kwenye harakati zake na watakuja na mkakati mpya na kukijenga chama chao.

“Jambo la msingi ni kwamba hakuna uadui kwenye siasa, tunapishana kwa hoja lakini sio kugombana. Lazima tujenge maisha nje ya siasa, tuhimili chuki zetu ili tusijenge Taifa lenye chuki, bali lenye umoja,” amesema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Miraji Mtibwiriko amesema umoja uliopo TCD ni jambo kubwa ambalo kila mmoja analitamani, Tanzania ina vyama vingi lakini wanaunganishwa kwa Utanzania wao.

“Pamoja na kwamba tunatofautiana, wote lengo letu ni moja, kila mmoja anataka kushika dola ili aweze kuleta maendeleo kwa Watanzania. TCD ina lengo kuu la kukuza demokrasia nchini, tuko pamoja kuhakikisha kwamba siku zijazo tunakuwa na demokrasia iliyokomaa,” amesema.

Kwa upande wake, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema jambo muhimu kwao ni kujilinda na kuitetea demokrasia. Amesema wanaweza kuwa na tofauti lakini la msingi linalowakutanisha ni kuzungumza na kusisitiza amani, maendeleo na demokrasia ya kweli.

“Jukwaa hili ni muhimu kwetu kwa sababu linalotukutanisha wadau wa vyama vya siasa kujadili mambo ya kuimarisha demokrasia.

“Siasa za vyama vingi zinahusisha itikadi tofauti, malengo tofauti na kutofautiana sio uadui, ni chanzo cha kuwa na mawazo bora. Kwa hiyo, mawazo hayo yakikusanywa kwa pamoja yanaweza kuleta maendeleo katika Taifa letu,” amesema Semu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa TCD.