Mbeya. Wasambazaji na wauzaji wa movies, Muziki na Filamu jijini Mbeya wamelalamikia baadhi ya mawakala wanaopita kukusanya fedha kinyume na utaratibu, wakiomba serikali kuingilia kati ili kunusuru vibarua na usalama wao katika shughuli zao.
Imeleezwa kuwa mawakala hao hujitambulisha kutoka Umoja wa wasambazaji Movies ‘Films Distributers’, ambapo hupita kila kibanda kukusanya Sh10,000 kwa kila wiki, huku wakitoa vitisho pale wanapohojiwa uhalali wao wa kufanya hivyo kisheria.
Wakizungumza leo Machi 13, 2026 baadhi ya wajasiriamali hao wamesema changamoto hiyo imekuwa kubwa na wanapohoji hupewa vitisho na muda mwingine kulazimisha kufungiwa ofisi na kuharibiwa vitendea kazi.
Gliba Mwakapesa amesema alifikiwa na kundi la watu takribani 11 wakimtaka kutoa Sh 15,000 kwa ajili ya kulipia movies za wiki moja nyuma wakijitambulisha kuwa na utambulisho wa Halmashauri ya Jiji.
Amesema katika kutaka kuwahoji na kujitetea waliamua kuingia ofisini kwake kwa nguvu na kuharibu vitendea kazi na kufuta taarifa zake muhimu, ambapo alipofuatilia kwa baadhi ya mamlaka hakupata msaada.
“Wanajitambulisha kwamba ni Umoja wa wasambazaji Movies, wanadai hatupaswi kuwa na movies bila kibali chao, wanakusanya Sh 10,000 kwa kila msambazaji, walitumia nguvu wakanikaba wakaingia ofisini wakafuta miziki kwenye diski.
“Wanadai filamu zote ziko chini yao na ndio wenye mamlaka kuzisambaza, nikahoji wana uthibitisho gani wakajibu ndio wamiliki na sheria inawatambua, lazima serikali ijue sisi tumejiajiri na maisha yetu yanategemea hii kazi,” amesema Mwakapesa.
Kwa upande wake Cleopart Mzumbwe amesema mawakala hao wametawanywa kila Kata, ambapo hukusanya Sh 10,000 na kwamba wanahofu ni watu wanaojipatia kipato kwa njia zisizo halali kwani hawatoi risiti wala kuweka wazi taarifa zao.
“Wanadai wanafanya kazi nchi nzima, wakishakusanya hicho kiasi husema wanakigawa kwa baadhi ya watumishi na watendaji wa serikali kwa kila mmoja kupewa Sh 1,000, hawana ofisi na taarifa zao haziko wazi,” amesema Mzumbwe.
Naye kiongozi wa Chama cha Maktaba ya Video mkoani Mbeya Nikolonda Mwabwalwa amesema kwa sasa wapo wajasiriamali zaidi ya 500, akieleza kuwa kero ya Sh 10,000 kwa kila kibanda imekuwa tatizo kwao.
“Ina maana kwa wiki wanakusanya Sh 800,000 kila Kata, ukizidisha kwa kwa Kata zote za Mkoa wa Mbeya utagundua fedha inayoenda bila utaratibu hata serikali huenda inapoteza mapato kupitia kikundi hiki.
“Tunajiuliza na kuwahoji umiliki wao halali wa hizi filamu hatuelewi, mawakala wapo kila Kata, wanaye kiongozi wao anayewapangia maeneo kwa ajili ya makusanyo,” amesema Mwabwalwa.
Katibu wa Chama cha Sanaa mkoani humo (Chasambe), Chifu Nyemba amesema wamepokea malalamiko ya uwapo wa kundi hilo ambalo halitambuliki kisheria, akieleza kuwa wanaendelea kuwasiliana na mamlaka ili hatua zichukuliwe.
“Nimefuatilia malalamiko hayo na tumebaini mengi, kinachosikitisha ni wasambazaji kufutiwa taarifa zao ofisini, Chasambe tutafanyia kazi changamoto hizi kwakuwa hii ni kazi kama zilivyo nyingine, huu umoja binafsi siutambui” amesema Nyemba.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu wa Taasisi ya Mlezi Foundation George Makona amewaomba wajasiriamali hao kuunda umoja au chama chao na kujisajili ili kuweza kutambulika na kupata haki zao.
“Yote haya ni kukosa umoja wenu, sasa tenegenezeni katiba chaguaneni viongozi ili muondokane na changamoto hizi, lakini mkiwa na umoja mtapata fursa nyingi ikiwamo mikopo ya serikali, semina na mafunzo,” amesema Makona.
Akitolea ufafanuzi wa tuhuma hizo, wakala wa Umoja wa wasambazaji movies ‘Films Distributers’ mkoani humo George Mlagalila, amesema kampuni hiyo imesajiliwa kisheria na kazi inazofanya ni halali na imefuata taratibu zote.
“Kampuni inafanya biashara kihalali, tunauza kazi za watu na tumetambulishwa kwa ngazi zote kuanzia mkoani, hao wafanyabiashara wanataka hizo filamu ziuzwe bure wasanii wasinufaike, wauze bila utarartibu.
“Sh 10,000 tunazochukua ni mali ya kampuni, wanachofanya ni kinyume na utaratibu, ni kweli nakiri nilifuta kazi za huyo mfanyabiashara baada ya kukaidi maelekezo, tunachofanya kipo kisheria,” amesema Mlagalila
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justice Kijazi alionekana kushtushwa na taarifa hizo, huku akimtaka Afisa Utamaduni wa Jiji hilo, Nimwindaeli Joseph kulitolea ufafanuzi zaidi, huku akisisitiza kuwa kundi hilo lisakwe kwani halina kibali cha kufanya kazi hiyo.
Akielezea sakata hilo, Nimwindaeli amesema Umoja huo ulishafika ofisi za Halmashauri ya Jiji la Mbeya wakiwa na barua kutoka Bodi ya Filamu, lakini barua hiyo iliandikwa kwa wenyeviti wa kamati za michezo ambapo walirudishwa.
Amefafanua kuwa waliporudishwa waliwashauri kurejea kwa Bodi ya Filamu kwa sababu mawakala hao hawana mamlaka ya kumuandikia Mkurugenzi na kuwataarifu Mkoa, hivyo umoja huo hauna uhalali.
“Kwanza siyo kweli kwamba wanaleta Sh 1,000 kwa Afisa Utamaduni lakini hawapo rasmi, walishafika ofisini miaka mitatu nyuma na sijui kama bado wanaendelea kuwepo hapa Mbeya, tuliwarudisha kwakuwa hawana uwezo wa kumuandikia Mkurugenzi.
“Tuliwajulisha pia na Bodi ya Filamu kuwafahamisha kuwa watu wao waliowaagiza kwetu, tumewaripoti mkoani na tangu mwaka juzi sina taarifa zao, labda naomba nilifuatilie tena kwa hatua zaidi,” amesema Nimwindaeli.