Staa wa zamani wa Bongo Fleva asimikwa kuwa mchungaji

Dodoma. Miaka kadhaa iliyopita jina la Ainea lilisikika sana kwenye anga la muziki wa Bongo Fleva, akitamba na vibao vilivyotikisa redio na majukwaa ya burudani. Lakini leo, sauti hiyo iliyowahi kuwaburudisha mashabiki imegeuka kuwa chombo cha kuhubiri neno la Mungu.

Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Kedmon Ainea maarufu kama Ainea, sasa ameanza rasmi maisha mapya ya kiroho baada ya kusimikwa kuwa mchungaji wa Kanisa la Anglikana Tanzania.

Ainea alisimikwa kuwa mchungaji katika ibada ya kuwekwa wakfu iliyofanyika Machi 8, 2026 katika Kanisa la Mtakatifu Petro Mwanachugu, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma. Baada ya kusimikwa, amepangiwa kuhudumu katika Kanisa la Mtakatifu Paulo lililopo Buza Mashine ya Maji Namba 5 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Digital leo Machi 14, 2026, Ainea amesema alianza rasmi huduma ya uchungaji Januari 13, 2026, ingawa ibada ya kusimikwa ilifanyika baadaye kutokana na ratiba za kanisa.

“Namshukuru Mungu kwa kunifikisha hapa. Kutoka kwenye muziki wa Bongo Fleva hadi kuvaa kola ya uchungaji haikuwa safari rahisi. Kulikuwa na changamoto nyingi, lakini Mungu ameniongoza hatua kwa hatua hadi kufikia hapa,” amesema Ainea.

Kedmon Ainea akiwa kwenye vazi la kichungaji.

Amesema kwa sasa ameacha kabisa muziki wa kibiashara na ameamua kujikita kikamilifu katika huduma ya kumtumikia Mungu kupitia kanisa alilopangiwa.

Kwa mujibu wa Ainea, iwapo ataimba tena, itakuwa ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu na kuwajenga waumini kiroho badala ya kufanya muziki wa burudani kama ilivyokuwa hapo awali.

“Sasa hivi mimi ni mtumishi wa Mungu. Kama nitakuwa naimba basi nitakuwa naimba nyimbo za kumtukuza Mungu na kuwajenga watu kiroho. Sitakuwa tena nafanya muziki wa kibiashara kama zamani,” amesema.

Ainea aliwahi kutamba katika muziki wa Bongo Fleva mwanzoni mwa miaka ya 2000 kupitia nyimbo mbalimbali zilizopata umaarufu mkubwa, ikiwemo Sina Mpango Naye alioshirikiana na Mr Blue pamoja na Somebody aliomshirikisha msanii Shetta.

Licha ya mafanikio aliyoyapata katika muziki, ndoto ya kumtumikia Mungu ilikuwa ndani ya moyo wake kwa muda mrefu, ameeleza.

“Moyo wangu umejaa furaha isiyo na kifani kwa sababu kumtumikia Mungu ilikuwa ndoto yangu ya muda mrefu sana. Leo ndoto hiyo imetimia,” amesema.

Aidha, amewahimiza vijana wenye ndoto ya kumtumikia Mungu lakini hawajui pa kuanzia kuendelea kumuomba Mungu ili awaonyeshe njia sahihi kama alivyomwonyesha yeye.

“Kwa vijana wenzangu ambao wana ndoto ya kumtumikia Mungu lakini bado hawajaiona njia, waendelee kumuomba Mungu. Mungu anaweza kufungua milango kwa wakati wake kama alivyofanya kwangu,” amesema.

Ainea alihitimu masomo ya uchungaji mwaka 2024 katika Chuo cha Theolojia cha Msalato mkoani Dodoma, hatua iliyofungua njia ya safari yake mpya ya kiroho.