Viongozi wa vyama vya wafanyakazi waonywa kuwatetea wanachama wanaovunja maadili

Dodoma. Baadhi ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi wameonywa kuacha kuwatetea wanachama wanaokiuka maadili ya kazi, kwa kuwa tabia hiyo inatajwa kuchochea utovu wa nidhamu katika utumishi wa umma.

Onyo hilo limetolewa leo Machi 14, 2026 na mwakilishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Mwantumu Mussa, wakati akizungumza na viongozi na wajumbe wa Chama cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu Tanzania (Chakuhawata) katika mkutano wa kiutendaji uliofanyika jijini Dodoma.

Mwantumu amesema viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanapaswa kuwaelimisha wanachama wao kuhusu wajibu na maadili ya kazi badala ya kuwakingia kifua wanapobainika kukiuka sheria na taratibu za kiutumishi.

“Acheni kuwatetea wafanyakazi wanaovunja sheria na kukiuka maadili ya kazi. Mnapaswa kuwaelimisha wanachama wenu kuhusu wajibu wao badala ya kuwakingia kifua wanapokosea,” amesema.

Amesema katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwapo ongezeko la matukio ya utoro kazini, ulevi, mavazi yasiyoendana na maadili ya kazi pamoja na mahusiano yasiyofaa mahali pa kazi, hali inayodhoofisha taswira ya taaluma ya ualimu.

Amesema changamoto nyingine inayowakabili walimu ni matatizo ya kifedha yanayotokana na kuchukua mikopo bila mpangilio, jambo linalosababisha baadhi yao kubaki bila kipato cha kutosha baada ya makato ya mishahara.

“Hili nalo ni jambo la kuangaliwa kwa makini. Baadhi ya walimu wanachukua mikopo bila mpangilio na mwisho wa siku wanajikuta hawana kipato kinachobaki baada ya makato, hali inayosababisha changamoto katika maisha yao ya kila siku,” amesema.

Aidha, amewataka walimu kuimarisha mshikamano kazini na kuepuka tabia ya kujengeana chuki na majungu, akisema hali hiyo haiwasaidii katika kuboresha taaluma yao.

Katika mkutano huo, mgeni rasmi ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Elimu Tanzania (ADEM), Dk Maulid Maulid, amesema Chakuhawata ni chama halali kisheria na kina haki ya kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Amesisitiza kuwa walimu hawapaswi kulazimishwa kujiunga na chama chochote cha wafanyakazi, bali wanapaswa kuwa na uhuru wa kuchagua chama wanachotaka kujiunga nacho.

Dk Maulid pia amekemea taarifa za baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri kudaiwa kuchelewesha au kutowasilisha makato ya wanachama wa Chakuhawata licha ya chama hicho kutambuliwa kisheria.

“Mimi nitalifikisha jambo hili kwa wakubwa wangu ambao nao watalifikisha hadi kwa Mheshimiwa Rais ili haki itendeke. Serikali inatambua uwepo wa chama hiki na haki zake kisheria,” amesema.

Hata hivyo, amewashauri viongozi wa Chakuhawata kuepuka migogoro isiyo ya lazima na badala yake kutumia njia za mazungumzo katika kutatua changamoto zinazojitokeza.

“Chama hiki kiwe sehemu ya kujenga suluhu badala ya kuongeza migogoro. Tuko tayari kukutana na viongozi wa juu wa chama chenu ili kujadili namna ya kutatua changamoto zilizopo,” amesema.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chakuhawata, Abias Lutandula amesema tangu chama hicho kisajiliwe mwishoni mwa mwaka 2015 kimeendelea kukua kwa kasi kwa kuongeza idadi ya wanachama.

Amesema chama hicho kilianza na wanachama 182 waliokuwa wote kutoka Manispaa ya Kigoma, lakini sasa kina wanachama 49,754 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kutokana na ongezeko hilo, amesema chama kimeamua kuhamishia makao makuu yake jijini Dodoma ili kurahisisha uratibu wa shughuli zake na kuwahudumia wanachama kwa ufanisi zaidi.

“Kwa sasa tuna wanachama katika wilaya 84 nchini na viongozi wao ndio wamehudhuria mkutano huu. Uamuzi wa kuhamisha makao makuu Dodoma utarahisisha uratibu wa shughuli za chama,” amesema.

Lutandula ameongeza kuwa chama hicho kinatarajia kufanya uchaguzi katika wilaya 44 hivi karibuni baada ya kufikisha idadi inayohitajika ya wanachama katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Lutandula, kila mwanachama wa Chakuhawata anatakiwa kuchangia Sh5, 000 kwa mwezi kama ada ya uendeshaji wa chama hicho.