Mbarali. Kwa miaka mingi baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari katika Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kila siku kufuata masomo, hali inayochosha na wakati mwingine kuwakatisha tamaa ya kuendelea na shule.
Hata hivyo, hali hiyo huenda ikawa historia baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kutenga zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa mabweni yatakayosaidia wanafunzi kukaa karibu na shule.
Fedha hizo zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2025/2026 kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwemo mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Machi 14, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli amesema fedha hizo zinalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia ili wanafunzi waweze kupata elimu katika mazingira bora.
Mweli amesema pamoja na kuimarisha miundombinu ya elimu, halmashauri hiyo pia imeanza mikakati ya kutatua changamoto nyingine zinazogusa sekta hiyo, ikiwemo uhaba wa maji safi katika baadhi ya maeneo.
“Tunaendelea kutatua changamoto zinazojitokeza katika sekta ya elimu. Sambamba na hilo, tumeanza ziara za kukagua miradi ya maendeleo na kufanya mikutano ya hadhara ili kusikiliza kero za wananchi,” amesema Mweli.
Amesema katika ziara yake ya hivi karibuni katika Kata ya Kongoro Mswisi alibaini changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufika Shule ya Sekondari Jakaya, jambo lililobainisha umuhimu wa kujenga bweni la wanafunzi.
“Baada ya kuona changamoto hiyo, tayari nimetoa maelekezo ili kuanza maandalizi ya ujenzi wa bweni kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027. Tunatafuta namna bora ya kutenga fedha kwa ajili ya mradi huo pamoja na miradi mingine muhimu,” amesema.
Mweli amesema mkakati wa kujenga mabweni katika shule za sekondari ni sehemu ya juhudi za halmashauri kuboresha miundombinu ya elimu na kupunguza changamoto wanazokutana nazo wanafunzi, hususan wale wanaotoka mbali na shule.
Amesema katika utekelezaji wa miradi hiyo, gharama za ujenzi wa bweni katika halmashauri hiyo zinakadiriwa kuwa kati ya Sh130 milioni hadi Sh135 milioni.
“Tunafanya kila jitihada kuhakikisha fedha zinapatikana ili kutekeleza miradi hii kwa ufanisi. Mabweni yatasaidia wanafunzi kupata mazingira mazuri ya kusoma bila changamoto ya kusafiri umbali mrefu kila siku,” amesema.
Mweli ameongeza kuwa hatua hiyo pia inalenga kuwasaidia zaidi watoto wa kike ambao mara nyingi hukumbana na changamoto mbalimbali wanapolazimika kusafiri umbali mrefu kwenda au kurudi shuleni.
“Tunafahamu umuhimu wa kuwasaidia mabinti zetu kupata elimu bora. Tuna wajibu wa kuhakikisha wanapata haki yao ya elimu bila vikwazo kwa kuboresha miundombinu ya shule,” amesema.
Mbali na sekta ya elimu, Mweli amesema halmashauri hiyo imeanza tathmini ya maeneo yenye changamoto ya huduma ya maji safi kwa lengo la kuanzisha miradi ya uchimbaji wa visima.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kongoro Mswisi, Leonard Mwampyate amesema mpango wa ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Jakaya utasaidia kupunguza tatizo la utoro miongoni mwa wanafunzi.
“Kimsingi ukosefu wa bweni ni changamoto kubwa kwa wanafunzi, hasa watoto wa kike, kupata elimu bora. Nashukuru halmashauri kwa kuweka mpango wa ujenzi wa bweni kupitia mapato ya ndani,” amesema Mwampyate.
Hatua hiyo imemfurahisha mkulima wa mpunga, Ester Kiswaga ambaye amesema ujenzi wa mabweni utasaidia wanafunzi wengi kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata masomo.
“Watoto wengi wanachoka njiani au kuchelewa kufika shuleni kwa sababu wanatoka mbali. Mabweni yatawasaidia kusoma vizuri na hata kupunguza utoro,” amesema Kiswaga.
