Wawekezaji watakiwa kukata bima kulinda miradi mikubwa ya Tanga

Tanga. Wawekezaji wametakiwa kuona umuhimu wa kujiunga na huduma za bima ikiwa ni jitihada za kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inalindwa dhidi ya majanga na hasara zisizotarajiwa.

Wito huo umetolewa Ijumaa, Machi 13, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, alipokuwa mgeni rasmi katika hafla fupi ya futari iliyoandaliwa na NIC kwa wadau wake ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kolimba alisema uwekezaji mkubwa uliofanywa katika mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Tanga uliogharimu takribani Sh 429 bilioni, ni miongoni mwa miradi mikubwa inayochochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.

Mbali na mradi huo wa bandari, Kolimba amesema Tanga inaendelea kupokea miradi mingine mingi ya kimkakati, jambo ambalo linaifanya kuwa kitovu muhimu cha maendeleo.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa uwekezaji huo mkubwa unahitaji ulinzi madhubuti ili kuepusha hasara endapo majanga yatatokea.

Ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Chongoleani ambao umeajiri vijana wengi wa Tanga, pamoja na ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Bagamoyo.

“Tunayo miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa hapa Tanga. Ni muhimu wawekezaji kukata bima ili kujiepusha na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza na kusababisha hasara kubwa,” amesema Kolimba.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema  kasi ya uwekezaji inayoendelea mkoani Tanga inaashiria uwezekano mkubwa wa mkoa huo kupanda katika nafasi za juu kitaifa kwa ukusanyaji wa mapato.

Amesema kwa sasa Tanga ipo nafasi ya sita, lakini inaweza kufikia nafasi ya pili au ya tatu kati ya mikoa 26 nchini, ikichuana na Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa pato la Mkoa wa Tanga limeongezeka kutoka Sh 6 trilioni hadi Sh 9 trilioni, hali inayotokana na uwekezaji unaoendelea na mazingira ya amani na utulivu.

Kutokana na hali hiyo, Kolimba amewataka wawekezaji zaidi kuchagua Tanga kama eneo la uwekezaji akieleza kuwa ni mkoa wenye usalama, utulivu na wananchi wakarimu wanaokaribisha maendeleo.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Alhaj Juma Luwuchu, ameipongeza NIC kwa kuandaa hafla hiyo ya kufuturisha wadau mbalimbali, akisema kitendo hicho kinaimarisha mshikamano na upendo katika jamii.

Amesema Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kipindi muhimu kwa waumini wa Kiislamu kufanya mema na kujenga mshikamano, hivyo amewahimiza waumini kuendeleza wema na kulinda amani ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Mkoa wa Tanga, Mariam Gambazi, amesema imekuwa desturi ya shirika hilo kufuturisha wadau wake kila mwaka wakati wa Ramadhani kwa lengo la kuimarisha mahusiano na ushirikiano.