Uganda na Tanzania kuondoa vikwazo vyote vya biashara ifikapo Juni

Dar es Salaam. Uganda na Tanzania zimekubaliana kuondoa vikwazo vyote vya biashara kati ya nchi hizo mbili ifikapo mwezi Juni mwaka huu, hatua inayolenga kupunguza gharama za kufanya biashara, kuimarisha biashara ya pande mbili na kukuza ushirikiano wa kiuchumi.

Ahadi hiyo ilitangazwa wakati wa chakula cha jioni rasmi kilichoandaliwa na Ubalozi wa Uganda nchini Tanzania jijini Dar es Salaam Alhamisi jioni, kuelekea Kikao cha Tano cha Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Uganda na Tanzania (JPC).

Kikao hicho kimefanyika kuanzia Machi 11 hadi Machi 13, 2026 katika Julius Nyerere International Convention Centre, na kimewakutanisha maafisa wa serikali kutoka nchi zote mbili kujadili na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Fred Mwesigye, alisema nchi hizo mbili zina uhusiano wa kihistoria unaozidi urafiki wa kawaida na kufikia kiwango cha undugu wa karibu.

“Tungependa kuwaambia Watanzania na Waganda kwamba sisi si marafiki tu, bali ni ndugu. Kila tunachofanya tunakifanya kama ndugu—bila migogoro, bila vikwazo na bila changamoto zisizo za lazima,” alisema.

Kwa mujibu wa balozi huyo, lengo kuu la mazungumzo yanayoendelea kati ya serikali hizo mbili ni kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi na kuhakikisha wafanyabiashara wa pande zote wanafanya biashara bila vikwazo visivyo vya lazima.

“Tunapoelekea kwenye kikao cha tano cha JPC, tumekubaliana kuwa vikwazo vyote vilivyopo katika biashara vitaondolewa ifikapo mwezi Juni. Hii ina maana tunatarajia kuona nafaka zikiingia Uganda bila vizuizi, na wafanyabiashara wa Uganda wakifanya biashara Tanzania bila vikwazo,” alisema Balozi Mwesigye.

Alieleza kuwa baadhi ya tozo na gharama zinazohusiana na kodi zimekuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazoongeza gharama kwa wafanyabiashara kati ya nchi hizo mbili. Kuondolewa kwa vikwazo hivyo kutasaidia biashara kukua kwa kasi na kuimarisha ujumuishaji wa kiuchumi.

Balozi Mwesigye pia aliipongeza Tanzania kwa kuboresha miundombinu inayorahisisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Alitaja maendeleo ya barabara zinazounganisha Tanzania na Uganda, mipango ya kuufikisha Reli ya Kisasa (SGR) hadi Uganda pamoja na maboresho katika bandari zinazotumiwa na wafanyabiashara wa Uganda, ikiwemo Tanga, Mwanzana Dar es Salaam.

“Maboresho haya yatafanya usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi zetu uwe rahisi zaidi. Mara tu gharama zilizobaki zitakaposhughulikiwa, biashara kati ya Uganda na Tanzania itakua kwa kasi zaidi,” alisema.

Balozi Mwesigye pia alizungumzia kile alichokiita kutokuwepo kwa uwiano katika uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Alisema uwekezaji wa Watanzania nchini Uganda kwa sasa unazidi dola bilioni 2, huku uwekezaji wa Waganda nchini Tanzania ukiwa takribani dola milioni 200.

“Huo ni utofauti mkubwa. Lakini mara vikwazo vilivyosalia vitakapoondolewa, tunatarajia bidhaa za Uganda kama sukari kuingia Tanzania bila changamoto, huku bidhaa za Tanzania kama mchele zikifika kwa urahisi zaidi katika soko la Uganda,” aliongeza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Uganda, Vincent Bagiire, aliwapongeza maafisa kutoka nchi zote mbili kwa mafanikio yaliyopatikana katika siku mbili za majadiliano kuelekea kikao cha JPC.

Alisema diplomasia ya kisasa inazidi kuelekeza nguvu katika masuala ya uchumi na biashara, huku majukwaa kama JPC yakisaidia kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi.

“Diplomasia ya sasa inalenga zaidi maslahi ya kiuchumi na kibiashara. Mifumo kama JPC ni nyenzo muhimu katika kutekeleza mtazamo huo na kusaidia kukuza uchumi wetu,” alisema.

Aidha alimpongeza Ubalozi wa Uganda jijini Dar es Salaam kwa juhudi zake katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo mipango ya kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Alitaja pia juhudi zinazoendelea za kuuza mabasi ya umeme yanayotengenezwa Uganda katika masoko ya kikanda ikiwemo Tanzania, akisema tayari kuna dalili kuwa mabasi hayo yanaweza kupata soko nchini Tanzania.

Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Uganda anayeshughulikia Ushirikiano wa Kikanda, John Mulimba, alisema ushirikiano wa kikanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unaendelea kuwa msingi muhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama.

Alibainisha kuwa mageuzi ya hivi karibuni ndani ya jumuiya hiyo yanatarajiwa kuboresha maamuzi na kuimarisha taasisi za kikanda.

“Tumekutana hapa kwa ajili ya JPC ili kuthibitisha upya dhamira yetu ya kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja na Umoja wa Forodha. Mifumo hii tayari inatoa mwongozo wa masuala mengi tunayojadili,” alisema.

Alisisitiza kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa yanatekelezwa kwa vitendo.

“Lazima tuondoke hapa tukiwa na ratiba na majukumu yaliyo wazi ili wizara, idara na taasisi ziweze kutekeleza tuliyokubaliana badala ya kuweka nyaraka makabatini,” alisema.

Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) ni jukwaa muhimu la ushirikiano wa pande mbili ambapo Tanzania na Uganda hupitia na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, miundombinu, usalama na ujumuishwaji wa kikanda.