Global Publishers
March 15, 2026
0 Comments
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Marekani inapanga kuhakikisha kuwa Strait of Hormuz inafunguliwa na kubaki salama kwa usafirishaji wa kimataifa, huku akisisitiza kuwa hatua hiyo itafanyika kwa njia yoyote ile.
Kupitia chapisho aliloweka kwenye jukwaa lake la Truth Social, Trump alisema kuwa anatarajia mataifa kadhaa yenye nguvu duniani ikiwemo China, France, Japan, South Korea na United Kingdom yatatuma meli za kivita kusaidia kulinda njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.
Trump alisisitiza kuwa mataifa mengi yataungana kuhakikisha kuwa njia hiyo ya baharini inabaki wazi na salama kwa meli zinazopita katika eneo hilo, ambalo ni moja ya njia muhimu zaidi za biashara ya mafuta duniani.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa Marekani alisema kuwa hadi hatua hiyo itakapokamilika, jeshi la Marekani litaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya boti na meli za Iran katika eneo la bahari, akidai kuwa hatua hizo ni sehemu ya kulinda usalama wa usafirishaji wa kimataifa.
Trump pia alidai kuwa Marekani tayari imeharibu asilimia 100 ya uwezo wa kijeshi wa Iran, lakini akakiri kuwa bado Iran ina uwezo wa kutumia silaha kama ndege zisizo na rubani, mabomu na makombora ya masafa mafupi.
Hata hivyo, madai hayo yamepingwa vikali na Tehran. Mwakilishi wa Iran katika ofisi za kimataifa mjini Geneva, Ali Bahrani, amesema kauli ya Trump kwamba Marekani imeondoa uwezo wa kijeshi wa Iran “inategemea uongo wa kutunga”.
Kauli hizo zinaongeza mvutano kati ya Washington na Tehran, huku Strait of Hormuz ikiendelea kuwa eneo nyeti sana kimkakati kutokana na kupitisha sehemu kubwa ya mafuta yanayosafirishwa duniani.