Zimamoto Mbeya wasaka mwili wa mtoto aliyesombwa na mafuriko

Mbeya. Wakati matukio ya watu kusombwa na maji yakiendelea kujirudia mkoani Mbeya, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo limesema linatarajia kuanza kampeni maalumu ya kuwafikia wananchi kutoa elimu ya tahadhari, hususani kipindi hiki cha mvua.

Hatua hiyo inakuja baada ya matukio ya watu wawili, akiwamo mtumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbarali, idara ya maabara, Davi Ami, aliyeokolewa katika moja ya mito uliopo Kata ya Lugelele wilayani humo.

Baada ya kuokolewa na askari wa Zimamoto chini ya DFO Ayoub Sanga, Ami alipelekwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu, huku ikielezwa afya yake kuendelea kuimarika.

Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia leo, Machi 15, 2026 kufuatia mvua iliyonyesha, huku lingine likimkuta mtoto Moreen Mwamezi, mwenye umri wa miaka minne wa Mtaa wa Kalobe, Kata ya Nzovwe, ambaye alidaiwa kusombwa na maji na mwili wake kutopatikana.

Akizungumza na Mwananchi leo, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (SSF) mkoani Mbeya, Malumbo Ngata, amethibitisha kutokea kwa matukio hayo, akieleza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Amesema mwendelezo wa matukio ya watu kusombwa na maji unatokana na baadhi kupuuza taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), lakini kupima kina cha maji kwa macho, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.

“Kutokana na hali hii, nimewaelekeza wakuu wa zimamoto wilaya zote kushirikiana na watendaji wa mitaa na kata kuhakikisha wanatoa elimu juu ya majanga ya moto ili kusaidia jamii kuepuka changamoto hizi.

“Wale wananchi walio kwenye maeneo hatarishi waondoke mara moja, ili kunusuru maisha yao. Jeshi la Zimamoto linaendelea kutoa huduma saa 24, na tunashukuru kwa sasa wananchi wanatoa taarifa inapotokea majanga ya moto,” amesema Ngata.

Ngata ameongeza kuwa kwa sasa Serikali imetoa vifaa vya kisasa kwa jeshi hilo kukabiliana na majanga ya moto, akibainisha kuwa askari wenye weledi na uzoefu wapo tayari kufanya kazi kuhakikisha jamii inakuwa salama.

Mmoja wa wananchi katika Mtaa wa Sokoine jijini Mbeya, Tekla Mwakami, amesema kwa kipindi hiki cha mvua, jamii inapaswa kuwa makini na familia, hasa watoto, wazee na wenye ulemavu ambao ni rahisi kukutwa na majanga hayo.

Amesema akiwa mmoja wa wahanga wa matukio ya majanga ya moto, Jeshi la Zimamoto lilifika kwa wakati na kufanikiwa kuzima moto na kuokoa maisha ya familia yake na mali zilizokuwa ndani, tukio lililotokea mapema Februari Mtaa wa Chaula jijini humo.

“Tunalipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa ushirikiano wa haraka inapotokea majanga ya moto, lakini niwaombe wananchi wenzangu tuchukue tahadhari na kuwalinda watoto, wazee na wenye ulemavu, na tuwe makini na vyanzo vya moto nyumbani,” amesema Tekla.