Ndoa ni taasisi kongwe zaidi duniani, lakini bado inasalia kuwa mada yenye utata, hisia kali na tafsiri tofauti kulingana na utamaduni, dini na mabadiliko ya kijamii.
Katika jamii yetu ya Kitanzania, maneno haya matatu: kuoa, kuolewa na kuoana hutumika kwa kubadilishana kana kwamba yana maana moja. Hata hivyo, wataalamu wa saikolojia na uhusiano wanabainisha kuwa kuna tofauti kubwa ya kifikra, kijamii na kihisia nyuma ya kila neno.
Je, unajua ni kwa nini mwanaume anasema ‘ameoa’, mwanamke anasema ‘ameolewa’, lakini wanandoa wa kisasa wanapendelea neno ‘tumeoana’?
Kwa karne nyingi, mfumo wa maisha umekuwa ukimpa mwanaume nafasi ya “mtendaji” na mwanamke nafasi ya “mtendewa” . Neno Kuoa kimsingi linaashiria umiliki na mamlaka.
Katika muktadha wa kijadi, mwanaume anapooa, anachukua jukumu la uongozi, ulinzi na utoaji. Hata hivyo, mtaalamu wa saikolojia ya familia, Dk Chris Mauki, anabainisha kuwa mtazamo huu wakati mwingine huleta mkanganyiko wa kisaikolojia.
“Unaposema ‘nimeoa’, kisaikolojia unajiona kama mmiliki wa mradi. Hii inaweza kuleta hali ya mwanaume kujihisi yuko juu ya sheria za ndoa na mwanamke ni mfuasi tu. Ni muhimu kuelewa kuwa kuoa si kununua bidhaa, bali ni kuingia kwenye mkataba wa kisheria na kijamii unaohitaji unyenyekevu,” anasema.
Kwa upande mwingine, neno kuolewa mara nyingi limekuwa likitazamwa kama hatua ya mwanamke “kuchukuliwa” kutoka kwao na kuingizwa kwenye himaya nyingine. Hapa ndipo dhana ya mahari inapoingia.
Ingawa mahari ni ishara ya shukrani, wataalamu wanaonya kuwa baadhi ya wanaume huitafsiri kama risiti ya ununuzi, jambo linalofanya neno ‘kuolewa’ lionekane kama kupoteza uhuru wa mwanamke.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na msukumo mkubwa wa kutumia neno kuoana. Hii si tu mabadiliko ya lugha, bali ni mabadiliko ya kiitikadi.
Kuoana kunamaanisha ushirika. Hakuna aliye juu ya mwenzake; wote wawili wameamua kwa hiari kuunganisha maisha yao, ndoto zao na rasilimali zao.
Mshauri wa uhusiano na mwandishi, Genny Lwakatare, anasema kuwa ndoa nyingi zinazostawi leo ni zile ambazo wahusika wanajiona kama timu moja.
“Tofauti ya kuoana na yale maneno mengine ni ushirika. Katika ‘kuoana’, hakuna anayemvuta mwenzake kwa nguvu. Ni watu wawili wanaotembea upande mmoja. Hapa ndipo tunapopata dhana ya ‘sauti moja’ ndani ya nyumba. Mwanaume anajua ana msaidizi, na mwanamke anajua ana mshirika, si bosi,” anasisitiza Lwakatare.
Hali hii ya kuoana inapunguza migogoro ya nani ana mamlaka zaidi. Inajenga mazingira ambapo uamuzi wa kifedha, malezi ya watoto na maendeleo ya familia vinafanywa kwa pamoja.
Hii inaondoa ule mzigo mzito kwa mwanaume wa kuhisi lazima afanye kila kitu peke yake (kwa sababu yeye ndiye ‘aliyeoa’) na inaondoa unyonge kwa mwanamke wa kuhisi hawezi kuchangia chochote (kwa sababu yeye ‘ameolewa’).
Athari za kisaikolojia na kijamii
Uchaguzi wa neno unaloamua kulitumia unaakisi jinsi unavyomchukulia mwenza wako. Ikiwa mwanaume atasisitiza kuwa “mimi ndiye nimekuoa”, mara nyingi hujenga ukuta wa mawasiliano.
Vivyo hivyo, mwanamke anayejiona “ameolewa” tu bila kuwa na sauti, anajiondoa kwenye wajibu wa kusaidia ukuaji wa familia.
Mhadhiri wa dini ya Kiislam, Sheikh Hussein Ali, anatoa mtazamo wa kiroho na kijamii akisisitiza kuwa lugha hizi zisitumike kukandamiza upande mwingine.
“Dini na mila zetu zinatambua majukumu ya kila mmoja, lakini msingi wa ndoa ni ‘mawadda na rahma’ (upendo na huruma). Iwe umesema umeoa au umeolewa, mwishowe lengo ni ‘kuoana’ katika roho na vitendo. Bila huruma, maneno haya yanabaki kuwa vifungo vya kisheria badala ya kuwa chemchemi ya furaha,” anafafanua.
Katika ulimwengu wa leo ambapo wanawake wanachangia uchumi wa familia kwa asilimia kubwa, dhana ya ‘kuoana’ inazidi kushika kasi.
Ni lazima jamii itambue kuwa ndoa si mashindano ya nani kamuwahi mwenzake au nani ana nguvu zaidi, bali ni safari ya hiari ya watu wawili walioamua kuwa kitu kimoja.
Je, wewe unajiona kama nani? Je, umeoa, umeolewa, au mmeoana? Jibu la swali hili linaweza kuwa ndilo siri ya furaha au machungu katika nyumba yako.
