Anti ninashindwa niseme au nifanye nini kwani maana mke wangu anataka kuniua kwa kihoro.
Nilikuwa na uhusiano na rafiki yake (nimeacha na sitorudia tena usiniseme vibaya), amejua maana alikuta ujumbe mfupi wa mahaba akaniuliza nikakataa.
Nadhani alikuwa anatufuatilia kwani alitukuta uso kwa macho tukiwa hotelini nje ya mji tunaogelea kwenye jakuzi.
Siyo jakuzi la jumuia ni lile ambalo linakuwa upande mliokodi kwa hiyo mnaogelea nyinyi tu.
Alipohakikisha ametuona na tumemuona akawasha gari akarudi mjini. Hata niliporudi hajaniuliza chochote na maisha yanaendelea kama kawaida.
Kibaya zaidi nilimuaga nakwenda Arusha kikazi, niliporudi aliniuliza habari za Arusha, nilishindwa kujibu, nasubiri aniuliza kuhusu uhusiano na rafiki yake nimuapie kuwa nimemuacha lakini hafanyi hivyo.
Nilikuwa nadharau lakini wiki hii itatimia ya tatu tangu anifumanie na haniulizi, hajanuna tena ameongeza mahaba, nimeanza kuogopa. Nifanye nini maana natamani kuikimbia nyumba.
Kwanza kabisa kukimbia nyumba hakutatatua tatizo kutazidisha tu. Ukiondoka bila maelezo, utaongeza maumivu, hasira na kutoaminiana.
Katika maisha ya ndoa, changamoto na makosa ni mambo yanayoweza kutokea, lakini namna mtu anavyokabiliana nayo ndiyo huamua hatima ya uhusiano.
Pale mwanaume anapofumaniwa akiwa na uhusiano wa nje ya ndoa na mke wake akajua ukweli huo bila hata kumuuliza, hali huwa ya hofu, aibu na msongo mkubwa. Baadhi ya wanaume katika mazingira kama haya hufikiria kukimbia nyumba kwa kuamini kuwa kuondoka kutapunguza shinikizo au kuepusha maswali magumu.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba kukimbia hakutatui tatizo, bali huongeza maumivu, mashaka na ufa mkubwa zaidi katika ndoa.
Hatua ya kwanza muhimu ni kukubali ukweli na kuwajibika kwa kosa lililofanyika. Kukaa kimya kwa muda mrefu, kama wiki tatu au zaidi, hakumaanishi kuwa tatizo limekwisha.
Mara nyingi kimya cha mke huwa ni ishara ya maumivu ya ndani. Kusubiri kuulizwa si suluhisho; ni bora ujikaze na kuanzisha mazungumzo kwa utulivu na unyenyekevu.
Kauli ya wazi kama, “Najua kuna jambo limekuumiza, na sitaki kukimbia, nataka tuzungumze,” inaweza kuwa mwanzo wa mazungumzo yenu, mwanzoni kama ameamua kukaa kimya anaweza akakataa mazungumzo hayo, ila ukirudia mara kwa mara kwa unyenyekevu atakubali.
Ukianza omba msamaha usipoteze muda kujitetea au kutoa visingizio hivi na vile hata kama ulifikia hatua hiyo kwa sababu inayojulikana, huu siyo wakati wake kuijadili.
Visingizio huongeza machungu na majeraha, kukiri kwa dhati, kuonyesha majuto na kuahidi mabadiliko ya kweli ndiko kunakoweza kurejesha imani taratibu.
Sambamba na hilo, ni lazima uhusiano wa nje ukatwe kabisa. Haiwezekani kujenga upya ndoa huku chanzo cha maumivu kikiendelea kuwepo.
Ni muhimu pia kuelewa kuwa uponyaji hauji kwa siku moja. Mkeo anaweza kuonyesha hasira, huzuni, ukimya au kuhitaji muda wa kutafakari. Hizi ni hisia za kawaida katika hali ya usaliti.
Hapa sasa umeyakoroga lazima uyanywe unapaswa kuwa na subira na kuonyesha namna ulivyobadilika na unavyojutia ulichokifanya, inaweza isiwe jambo la kuisha mara moja, ila ukituliza akili kila kitu kitakuwa sawa.
Nakupa maneno au ushauri wa akiba inawezekana kufanya mazungumzo kujadili suala hilo lisiwe jambo rahisi, hivyo shirikisha wasimamizi wenu wa ndoa/mshenga au viongozi wa dini mnaowaamini au mtu mzima mwenye hekima anaweza kusaidia kurejesha mawasiliano na kuelekeza suluhu.
Ila ndiyo ujifunze, na kama umesema unaacha uache milele. Haya mambo mnayaona madogo huleta fadhaa kubwa kwenye familia.
