Katika maisha ya binadamu, kuna mambo mengi ya kufanya na kutofanya. Kwa vile hii ni safu ya ndoa, leo, tutaangalia mafanikio na maanguko katika ndoa.
Hapa, kuna swali huwa linatushughulisha sisi kama wanandoa tena wa muda si haba. Je, inakuwaje baadhi ya wanandoa huweza kufanikisha mambo yanayowashinda wengi katika ndoa wakati wengine wakishindwa kabisa japo wana mafanikio mengine nje ya ndoa?
Inakuwaje mtu anakuwa kiongozi, msomi, au tajiri kubwa lakini anashindwa ndoa? Je, ni kupanga au majaliwa au ni kuonyesha namna ambavyo binadamu haawezi kupata vyote?
Katika kudurusu hali hii, tutaanza mfano wa Malkia wa Uingereza marehemu Elizabeth (1926 – 2022). Huyu mama, kutokana na usiri wake, hatuwezi kusema kuwa tunaijua ndoa yake vilivyo. Hata hivyo, kwa juujuu inajulikana. Pamoja na matatizo ya hapa na pale, Malkia alibainisha kuwa ndoa inaweza kuwa na mafanikio katika mambo ambayo wengi huwashinda hata kusababisha wawe na ndoa zenye changamoto na mazonge kutokana na baadhi ya mafanikio yao.
Tunadhani Elizabth ni mmoja katika wachache waliokaa kwenye ndoa na mafanikio ya kiutawala kwa miaka mingi karibia kuliko wote.
Kwani, aliishi kwenye ndoa kwa takriban miaka 74 na kwenye utawala kwa takriban miaka 64. Hii ni kutokana na baadhi ya matatizo ya wahusika kuwa kikwazo kwa ndoa zao kutokana na majukumu kiasi cha kutokuwa na muda wa kuimarisha ndoa yao.
Je, huwaje kunakuwapo watu waliofanikiwa kitaaluma, kiuchumi, na mengine lakini wakashindwa katika ndoa?
Pia, kwanini kuna watu waliofeli katika mambo mengine lakini wakafanikiwa katika ndoa? Siri hapa ni nini? Mfano, unakuta mtu ni tajiri lakini maskini wa ndoa.
Mwingine ni msomi wa kupigiwa mfano lakini asiye na ndoa au kama anayo, inayumbayumba au kukosa ladha na raha.
Wapo matajiri wa kuitwa utajiri lakini hawamo katika ndoa au ndoa zao zimevunjika. Jikumbushe watu waliofanikiwa kama vile Mfalme Charles wa Uingereza, Bill Gates, Donald Trump, Jeff Bizos na wengine ambao ni watu waliofanikiwa katika nyanja mbali mbali lakini ndoa ziliwashinda hadi zikavunjika au kuwa na maskandali kila uchao. Walinganishe hawa waliofanikiwa na watu wa daraja lao kama vile Tadashi Yanai tajiri mkubwa Japan, Warren Buffet, Zhong Shanshan tajiri mkubwa wa China, na wengine ambao ni matajiri wenye ndoa za kupigiwa mfano.
Je, kuna siri gani katika kushinda na au kumudu taasisi tata lakini nyeti ya ndoa?
Pia, lipo kundi la mabilionea ambao hawajawahi kuoa au kuolewa kama vile Andreas von Bechtolsheim, Diane Hendricks, Elon Musk, Oprah Winfrey, Michael Bloomberg, na wengine. Je, tatizo ni nini?
Utakuta mtu maskini au asiye msomi ana ndoa imara kuliko ya tajiri ilhali wasomi na matajiri zinawashinda. Nenda mbele zaidi.
Utakuta mama mrembo asiye na ndoa ilhali yule asiye mrembo anayo tena imara. Inakuwaje matajiri, wasomi, na warembo japo si wote wasiolewe lakini maskini, wasiosoma, na wasio warembo wakaolewa na kuishi kwenye ndoa imara? Hapa kuna fumbo vile vile na somo.
Jiulize. Ni kinamama tena matajiri au wasomi aka mishangazi japo hatupendi kushabikia neno hili wangapi wanaishi bila ndoa tena wengine wakitamani au kutangaza kutaka kuolewa wasiolewe? Wakati huo huo, unaweza kumkuta muuza baa akiwa kaolewa na anafaidi ndoa!
Je, hapa, tatizo ni wahusika au jamii? Nini suluhu ya kadhia hii? Maswali haya chokonozi na tekenyeshi kifikra yanajibiwa na the American Boys and Men (2025) ambalo linabainisha kuwa ni asilimia 50 tu ya wanawake wasomi wanaoolewa tena na wasomi wenzao. Nusu ya idadi iliyobaki, huolewa na watu wasio wasomi. Waliobaki wanabakia bila ndoa.
Tumalizie. Ni wangapi unaowajua wanaojikuta katika hali hii tuliyodurusu? Je, baadhi ya mafanikio ni chanzo cha maanguko katika ndoa na baadhi ya maanguko ni chanzo cha mafanikio katika ndoa?
Ama kweli wahenga walinena kuwa Mungu hawezi kukupa au kukunyima vyote. Anakupa hiki au hivi na kukunyima vingine.
Je, wewe kati ya mafanikio ya vitu na ndoa, unaridhika au kuchagua kipi? Kila la heri wanandoa na watarajiwa wote.
