Kuna kauli siku hizi imekuwa maarufu sana mitandaoni na hata kwenye vijiwe vya kahawa: “Natafuta mke mwenye kazi, anisaidie maisha.”
Ukiisikia mara ya kwanza unaweza kudhani ni kauli ya maendeleo, usawa wa kijinsia na mipango ya kisasa ya ndoa. Lakini ukiichambua vizuri, unaweza kubaini kuna harufu fulani ya uvivu iliyojificha nyuma ya maneno hayo matamu.
Kwa mzaha tu, lakini kwa uzito wake kauli hii mara nyingi haitolewi na mwanamume wa kweli, bali na kijana anayehitaji mfadhili wa maisha yake ya ndoto.
Tusielewane vibaya. Hakuna tatizo mwanamke kuwa na kazi. Hakuna tatizo wanandoa kusaidiana. Hata kusaidiana ndiyo roho ya ndoa.
Lakini tatizo linaanzia pale mwanaume anapoweka wazi kabisa kuwa anatafuta mke kwa sababu ya mshahara wake.
Hapo ndipo swali linazaliwa: Je, unatafuta mke au unatafuta mkopo wa maisha? Kiasili na kihistoria, katika jamii nyingi, mwanaume alijulikana kama mtafutaji.
Ndiye aliyekwenda shambani, porini au kazini kutafuta riziki, kisha akarudi nyumbani kuleta chakula na mahitaji ya familia.
Hata methali zetu hazikuacha jambo hili. Zilisema, “Mwanaume ni kichwa cha familia.” Hazikusema, “Mwanaume ni msaidizi wa mshahara wa mkewe.”
Sasa leo, kijana anakaa kijiweni, anamaliza bando la wiki kuperuzi mitandao, halafu anasema kwa kujiamini kabisa: “Mimi sitaki mke wa kukaa nyumbani, nataka mwenye kazi anisaidie.” Akusaidie nini wakati hata hujaanza kusaidika?
Ndoa ni ushirikiano. Lakini ushirikiano hauanzi na orodha ya mahitaji ya kifedha kutoka upande mmoja. Mwanaume anayesimama kifua mbele na kusema, “Mimi nitafanya hivi, nitahakikisha familia yangu inakaa vizuri,” hata kama ana kipato kidogo, anaonesha dhamira.
Lakini yule anayesema, “Mimi mshahara wangu ni wa vocha na mafuta ya gari, wa mke ndiyo wa maisha,” huyo anahitaji kikao cha dharura na dhamiri yake.
Wapo wanaume wanaotangaza waziwazi: “Sitaki mke asiye na kazi.” Sawa. Lakini ukimuuliza yeye anafanya nini, anakwambia, “Nipo kwenye mipango.” Hiyo mipango imeanza tangu lini?
Inaonekana kuna kizazi cha wanaume wa kisasa wanaotaka kulelewa kwa ustaarabu. Wanataka mke anayelipa kodi, analipia umeme, analipia ada ya watoto, halafu yeye anabaki na jukumu la kupost picha za familia mitandaoni.
Mke anahangaika kazini mchana kutwa, jioni anarudi kupika, kusafisha na kulea watoto. Bwana mkubwa yeye anachoka kwa sababu mechi ya jioni ilikuwa ngumu.
Ni vizuri mwanamke kuwa na kipato. Ni vizuri familia kuwa na vyanzo viwili vya mapato. Lakini mwanaume wa kweli hafanyi kipato cha mke kuwa nguzo kuu ya maisha kabla hata hajajenga msingi wake.
Mwanaume wa kweli hutafuta, hujipanga na hujenga. Mke akija na kazi yake, inakuwa ni nyongeza ya baraka, si sharti la kuanza maisha.
Kuna tofauti kati ya kusema, “Tujenge pamoja,” na kusema, “Njoo unijenge.”
Wengine wanadhani uanaume ni sauti nzito na kutembea kwa mwendo wa nguvu. Lakini uanaume wa kweli unaonekana kwenye uwajibikaji.
Ni rahisi kusema, “Nataka mwanamke anayejitegemea.” Lakini je, wewe unajitegemea?
Kama bado unamtegemea mama yako kukutumia nauli ya kurudi kazini, basi kabla hujatafuta mke mwenye kazi, tafuta kwanza kazi yenyewe.
Kwa mzaha, lakini kwa ukweli wake, wanaume wanaotanguliza mshahara wa mke kama kigezo kikuu cha ndoa wanapaswa kujiuliza upya. Ndoa si zabuni ya kifedha. Si mradi wa kutafuta mfadhili.
Na kama kweli unataka kusaidiana, basi anza kwa kuonyesha unaweza kubeba mzigo wako. Ukifanya hivyo, hata kama mke atakuwa na kazi kubwa kuliko yako, hakutakuwa na shida, kwa sababu wewe tayari umeonyesha kuwa unaweza kusimama.
Hakuna anayekataza mwanamke kufanya kazi. Lakini mwanaume anayekimbia jukumu la kutafuta na kuleta nyumbani, halafu anaficha uvivu wake nyuma ya pazia la “maisha ni magumu,” anapaswa kujitafakari.
Maisha ni magumu kweli. Lakini si sababu ya kuhamishia mzigo wako kwa mtu ambaye hata bado hujamuoa.
Mwanaume wa kweli hafanyi ndoa kuwa mkakati wa kujikimu. Anaifanya kuwa safari ya kujenga pamoja.
