Simba yatambulisha mshambuliaji | Mwanaspoti

KAIMU kocha mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema kwa sababu ya majeruhi, walikuwa na uhitaji wa mshambuliaji dirisha dogo.

Simba imemtambulisha mshambuliaji kutoka Camerron, Ernestine Heutchou ukiwa ni usajili pekee wa waliofanya kipindi cha dirisha dogo na anaungana na nyota wengine watatu katika eneo hilo ambao ni Jentrix Shikangwa ambaye ni mfungaji bora akiwa na mabao 10, Zawadi Usananase na Cynthia Musungu.

Nyota wawili waliopata majeraha, Usananse na Musungu, watakaa nje muda mrefu hivyo Simba ikalazimika kuingia tena sokoni kuongeza mshambuliaji.

Akizungumza na Mwanaspoti Mgosi alisema walikuwa na uhitaji mkubwa kwenye eneo hilo kwani ukimtoa Shikangwa hawakuwa na straika mwingine na Simba ina majeruhi saba kuanzia eneo la beki hadi washambuliaji lakini walisajili eneo hilo ili kuziba pengo na uhitaji wake.

“Tulihitaji straika kwa sababu wengine wawili waliumia raundi ya kwanza. Tumefanya usajili kwa sababu tulikuwa na mapungufu hasa eneo la ushambuliaji,” alisema Mgosi na kuongeza;

“Tunaamini tumeenda kutibu tatizo kwa sababu ingekuwa ngumu kumtegemea mshambuliaji mmoja na tunaamini ongezeko lake litatusaidia kwa sababu ni mchezaji mzuri na umri bado wake bado mdogo.”