Atupwa jela miaka 12 kwa kumuua mkewe

Mtwara. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, imemuhukumu kifungo cha miaka 12 jela Ally Abrahaman (45), mkazi wa Kijiji cha Mbagala-Mbuyuni, Kata ya Mkokona mkoani Mtwara, baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia.

Abrahaman alipatikana na hatia ya kumsababishia kifo Catherine Chivale (69), ambaye ni mkewe, baada ya kumshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia mikono na kipande cha mti.

Hukumu hiyo ilitolewa hivi karibuni katika kesi ya jinai namba 5827/2025 na Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Edwin Kakolaki, baada ya kujiridhisha kuwa ushahidi uliowasilishwa ulithibitisha mshtakiwa kutenda kosa hilo kinyume na vifungu vya 195 na 198 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 na 2023).

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, tukio hilo lilitokea Agosti 21, 2024, katika Kijiji cha Mbagala-Mbuyuni. Mshtakiwa na marehemu walikuwa wakirejea nyumbani wakitoka kumtembelea binti yao aliyekuwa akiishi kijijini hapo.

Wakiwa njiani, walipishana kauli na kuzuka ugomvi uliosababisha mshtakiwa kumshambulia marehemu. Kutokana na kipigo hicho, marehemu alipiga kelele akiomba msaada, jambo lililosababisha majirani kufika eneo la tukio kumsaidia.

Majirani hao walimpeleka katika nyumba ya mjukuu wake ili kumpatia huduma ya kwanza, hata hivyo alifariki dunia usiku huo huo.

Baada ya tukio hilo, mshtakiwa alikamatwa na wananchi na baadaye kukabidhiwa kwa maofisa wa Jeshi la Polisi waliofika kijijini hapo kufanya uchunguzi, ikiwemo kuchora ramani ya eneo lilipotokea tukio hilo.

Uchunguzi wa kitabibu ulionesha kuwa chanzo cha kifo cha Catherine kilitokana na jeraha kubwa la ubongo lililosababishwa na mshtuko mkubwa kichwani.

Jaji Mfawidhi Edwin Kakolaki ameeleza kuwa kifo cha mwanamke huyo kingeweza kuepukika kama mshtakiwa angetumia njia nyingine ya kumuonya.

“Kifo cha marehemu kingeweza kuepukika kama mshtakiwa angetumia njia nyingine ya kutatua mgogoro wao badala ya kutumia nguvu na silaha hatari kumpiga sehemu nyeti za mwili,” amesema Jaji Kakolaki.

Amebainisha tukio hilo linaashiria ukatili wa majumbani dhidi ya wanawake na kwa mujibu wa miongozo ya utoaji adhabu ya mwaka 2023, linaangukia katika kosa la kuua bila kukusudia.

Mahakama imezingatia hoja za utetezi kutoka upande wa mshtakiwa kuwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza, na kwamba wakati wa tukio pande zote mbili zilikuwa zimelewa pombe. Mwenendo wa mshtakiwa kabla, wakati, na baada ya tukio ulikuwa na uwezo wa kufikiri na kutambua anachofanya.

Aidha, kwa kuzingatia ukali wa silaha iliyotumika pamoja na majeraha aliyopata marehemu, ikiwemo jeraha la kichwa na kuvunjika mkono, adhabu stahiki ingekuwa kifungo cha miaka 15 jela.

“Kwa kuzingatia majeraha aliyopata marehemu na silaha iliyotumika, mahakama inaona adhabu stahiki ingekuwa miaka 15 jela. Hata hivyo, kutokana na sababu za kupunguza adhabu, mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 12 jela,” alisema Jaji Kakolaki.

Adhabu hiyo imepunguzwa kutokana na kuzingatia kuwa ni kosa la kwanza kwa mshtakiwa na tayari alikuwa amekaa rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja na miezi sita. Mahakama imepunguza adhabu hiyo kwa miaka mitatu na kumhukumu kifungo cha miaka 12 kuanzia siku ya hukumu.