ULE uhondo na utamu wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) unatarajiwa kuendelea Machi 28, 2026 baada ya ligi hiyo kusimama kupisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaokaribia ukingoni.
Katika mzunguko huu wa mwisho wa ligi hiyo, zimesalia mechi 10 kila timu baada ya kuchezwa 20 kati ya 30 na tamati ya ligi hiyo itakuwa Mei 2026.
Ukiachana na timu kuvuna ilichokipanda katika mechi 20, kuna kibarua kizito kwa mechi zilizosalia kwani zitakuwa za jasho na damu huku kila timu ikitazamiwa kutokuwa tayari kupoteza nafasi yake.
Msimu huu umekuwa bora na wenye ushindani mkubwa ikilinganishwa na uliopita ambao ushindani wake ulikuwa wa kawaida.
Mzunguko huu ukipigwa umeacha, kwani dakika hizi za lala salama ukizubaa wengine wanachukua kijiti kuendelea na mbio za kusaka ubingwa.
Ushindani wa kusaka ubingwa msimu wa 2025-2026 bado mbichi kwani timu nne zinazoongoza msimamo zimepishana kwa tofauti ya pointi moja isipokuwa mbili zenye tofauti ya mabao.
Kwenye msimamo wa ZPL, Fufuni ndiyo kinara wa ligi hiyo na pointi 38 sawa na Zimamoto iliyopo nafasi ya pili, zikipishana kwa idadi ya mabao, Fufuni ikifunga 26 na kufungwa 12, wakati Zimamoto imefunga 21 na kufungwa manane.
Msimamo huo unatukumbusha msimu wa 2024-2025 ambao Mlandege ilitwaa ubingwa kwa tofauti ya mabao, ikimaliza na pointi 62 sawa na ilizokuwa nazo KVZ, lakini uwiano wa kufunga na kufungwa uliibeba na kuipa taji hilo.
Mlandege ilimaliza msimu na jumla ya mabao 67 ya kufunga na kufungwa 21, ikiwa na maana ina tofauti ya mabao 46, wakati KVZ ilifunga mabao 35 na kufungwa 12, tofauti yake ni mabao 23 yaliyozuia kuwapiku mabingwa hao.
Kati ya timu nne zilizopo nafasi za juu katika ligi hiyo, miongoni mwao ni KVZ iliyomaliza msimu ikiwa nafasi ya pili, sasa ipo nafasi ya tatu na kuvuna alama 37 ikiwa na tofauti ya alama moja na kinara wa ligi hiyo.
KVZ pamoja na Uhamiaji inayoshikilia nafasi ya nne huku ikiwa na alama 36, ndizo zinazoongoza kufunga mabao mengi kwenye mechi 20 zilizocheza. Timu hizo zimefunga mabao 34, huku KVZ ikifungwa 21 na Uhamiaji 17.
Katika kuelekea mechi 10 za mwisho na ukipigwa au sare unashushwa timu zitachuana vikali kufanikisha hilo.
Vinara hao wa ligi, wamepanda daraja msimu huu na kuongoza msimamo, wakati ilizopanda nazo New Stone Town kutoka Pemba, Polisi na New King za Unguja hali sio nzuri.
Fufuni ambayo inatokea Pemba, katika duru la kwanza baada ya mechi 15, ilimaliza ya pili ikikusanya pointi 30, moja nyuma ya Zimamoto iliyokuwa kinara na pointi 31.
Kwa awamu hii, mambo yamegeuka, Fufuni ipo nafasi ya kwanza ikifikisha pointi 38 na uwiano mzuri wa mabao ikiacha Zimamoto nayo ikiwa na 38 katika nafasi ya pili.
Hali si shwari chini ya msimamo wa ligi hiyo kwani wakati wengine wakiwania ubingwa, zipo zinazopambana kufanya maombi ya kusalia zisishuke daraja.
Timu hizo zinafanya jitihada ya kujinusuru na janga la kushuka daraja msimu huu ikiwemo Malindi, Polisi, Junguni na New Stone Town.
Baada ya kuanza vizuri msimu huu wa Ligi Kuu Soka Zanzibar, Malindi SC ghafla kibao kimegeuka kwa kutoka kuwania ubingwa wa ZPL msimu huu hadi kujinusuru kulinda daraja ili isishuke.
Malindi ambayo baada ya mechi sita za kwanza ilikuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Soka Zanzibar ikikusanya pointi 14, kwa sasa imeporomoka hadi nafasi ya 13 ikifikisha pointi 24.
Timu hiyo iliyocheza mechi 20 imefunga mabao 19 na kufungwa mabao 22, Polisi ipo nafasi ya 14, imefunga mabao 12 na kufungwa mabao 21 ikivuna alama 19.
Timu ya Junguni United iliyopo nafasi ya 15 ambayo ina jumla ya mabao 16 ya kufunga na 48 ya kufungwa, imekusanya alama 10.
Junguni United imekuwa timu ya kwanza msimu huu kutozwa faini ya Sh200,000 kwa kufika uwanjani bila ya kuvaa jezi jambo lililosababisha kuvunjwa kwa mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa Septemba 26, 2025 dhidi ya Zimamoto kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, ikiwa ni mzunguko wa kwanza.
Junguni imekuwa timu ya pili kutoka mwisho iliyofungwa mabao mengi (48) msimu huu ikifuatiwa na New Stone iliyofungwa mabao 55 kwenye mechi 20.
New Stone Town mpaka sasa katika Ligi kuu Zanzibar ndiyo timu pekee ambayo haijapta sare kwenye michezo 20 iliyochezwa, timu hiyo inaburuza mkia katika msimamo wa ligi wakiwa na alama tatu tangu kuanza kwa Ligi.
Katika michezo hiyo iliyocheza wameshinda mmoja na kupoteza 19 huku ikiwa timu inayoongoza kupoteza michezo mechi na kuruhusu mabao 55 ikifunga 11.
Ili kuendelea kubaki kwenye ligi hiyo, inatakiwa kushinda mechi 10 huku wakiombea wapinzani wake wapoteze ili wao kusalia katika ligi hiyo.
Mechi 10 za mwisho zitakazoamua kwa kutoa bingwa wa msimu huu na na nani atasalia katika ligi hiyo kati ya nne zenye dalili ya kushuka daraja.
Ligi hiyo ilianza rasmi kutimua vumbi visiwani hapa Septemba 25, 2025 kwa michezo ya wiki ya kwanza na kutamatika Mei 31, 2026, ambapo Ngao ya Jamii ilichezwa Septemba 14, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex na KMKM kuchukua Ngao hiyo.