MTANZANIA mwingine Emmanuel Mlefu amejiunga na Sisli Yeditepe inayoshiriki Ligi ya Walemavu Uturuki kwa mkataba wa miaka miwili.
Mlefu anaungana na Mtanzania mwenzie Shedrack Hebron ambaye yupo klabuni hapo tangu msimu wa 2023 akitokea Sauti Para Sports ya Tanzania na ndiye aliyefanikisha dili hilo kwa kushawishi mabosi wa timu hiyo kumsajili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hebron alisema amefurahi na ni jambo zuri kwake kufanikisha dili hilo kuona Wabongo wengi wanacheza ligi hiyo.
“Kwa kweli nina furaha sana kufanikisha hili. Nimekuwa nikitamani kuona wachezaji zaidi kutoka Tanzania wanapata nafasi ya kucheza huku na sasa tumefanikiwa,” alisema Hebron.
“Ligi ya Tanzania bado haijawa yenye ushindani kama huku Uturuki kwa hiyo ninapoona nafasi fulani na kuna mchezaji wa Kitanzania anaweza kuikava vizuri, nazungumza na mabosi zangu ili na wenzetu wapate ajira.”
Aliongeza uwepo wa wachezaji wawili Wabongo katika timu moja utasaidia kuongeza ushindani pamoja na kuonyesha vipaji vya Watanzania.
“Nafurahi kwa sababu sasa tutacheza pamoja. Hii ni nafasi nzuri ya kuonyesha uwezo wetu na kuiwakilisha vizuri Tanzania na naamini akifanya vizuri zaidi mwezangu itafanya tuaminike,” alisema.
Baada ya kusainiwa Mlefu alisema “Nashukuru Mungu kusajili hapa kwa sababu Sisli ni timu kubwa na nimekuja kucheza ligi kubwa duniani na kuonyesha uwezo wangu.”
Mlefu anakuwa mchezaji wa saba kutoka Tanzania kuitumikia ligi hiyo, wengine ni Ramadhan Chomelo (Despas Enerji), Hebron, Mudrick Mohamed (Mersin), Kassim Mbarouk (Dispas SC), Richard Swai (Mersin) na Frank Ngailo (Izmir BBSK).