Wanne waliohukumiwa kunyongwa waachiwa huru

Arusha. Mahakama ya Rufani, imebatilisha adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa watu wanne waliokutwa na hatia ya mauaji na kuamuru waachiliwe huru baada ya kubaini kulikuwa na kasoro za kisheria katika mwenendo wa kesi yao.

Agosti 15, 2018 walidaiwa kumuua mke wa  mfanyabiashara wa dhahabu, Mwasi Kakolo na kuiba fedha Sh30 milioni na gramu 260 za dhahabu.

Walioachiwa huru ni Jacob Shindika, Boaz Saidi, Rashidi Mwaulezi na Japhet Sanga, ambao Desemba 30, 2022 Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya iliwahukumu kunyongwa.

Hukumu iliyobatilisha adhabu hiyo na kuwaachia huru warufani hao, imetolewa Machi 11, 2026 na majaji watatu ambao ni Rehema Mkuye, Sam Rumanyika na Profesa Ubena Agatho.

Jaji Agatho amesema Mahakama imebaini kulikuwa na tatizo katika uwakilishi wa kisheria uliotolewa kwa warufani wakati wa kesi katika Mahakama Kuu, kwani rekodi zilionesha warufani wa kwanza na wa pili waliwakilishwa na wakili mmoja, huku warufani wa tatu na wa nne nao wakiwakilishwa na wakili mmoja.

Majaji walieleza hali hiyo ilisababisha mgongano wa masilahi kwani warufani walikuwa wanatuhumiana katika kauli zao za tahadhari.

Kutokana na uwakilishi huo, haikuwezekana kwa warufani kuhojiana ipasavyo mahakamani jambo ambalo ni haki yao ya msingi katika kesi ya jinai na kuwa Mahakama ilisema hali hiyo ilisababisha kesi kukosa misingi ya haki na hivyo kuathiri mwenendo mzima.

Jaji Agatho, amesema Mahakama pia ilibaini kulikuwa na ucheleweshaji usio na maelezo ya kuwafikisha warufani mahakamani baada ya kukamatwa ambapo kwa mujibu wa rekodi za kesi, baadhi ya warufani walikaa mahabusu kwa muda wa kati ya miezi miwili hadi minne kabla ya kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.

Majaji walisema kuchelewa huko kulikiuka matakwa ya kifungu cha 33(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinachotaka mtuhumiwa kufikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

Jaji Agatho, amesema kwa kuwa upande wa mashtaka haukutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kuchelewa huko, Mahakama iliona kuwa haki za warufani zilikiukwa.

Ametaja kasoro nyingine iliyobainika ni kutokuitwa kwa shahidi muhimu ambaye alikuwepo wakati wa tukio na kuwa ndugu wa mfanyabiashara aliyeshambuliwa, Mgema Limbu, alikuwa shahidi muhimu kwani alishuhudia tukio hilo ila upande wa mashtaka haukumwita kutoa ushahidi bila kutoa sababu zozote.

Majaji walisema kutokuitwa kwa shahidi huyo kuliifanya Mahakama kutoa hitimisho kuwa ushahidi wake ungeweza kuwa na madhara kwa upande wa mashtaka.

Kuhusu suala la utambuzi wa washambuliaji uliotolewa na shahidi mkuu, ingawa shahidi huyo alisema aliwatambua baadhi ya washambuliaji kutokana na mwanga uliokuwepo nyumbani kwake na kuwa ushahidi huo haukuwa thabiti.

Walibainisha kuwa shahidi huyo alipoteza fahamu wakati wa tukio na hivyo hali yake ya akili haikufafanuliwa kikamilifu mahakamani,hivyo iliona kuwa ushahidi wa utambuzi haukuwa wa kuaminika bila kuungwa mkono na ushahidi mwingine madhubuti.

Kuhusu ombi la upande wa Jamhuri kuomba kesi hiyo irudiwe, Jaji Agatho amesema mapungufu yaliyokuwepo katika ushahidi wa upande wa mashtaka yalikuwa makubwa kiasi kwamba kuamuru kesi irudiwe kungeweza kuipa fursa upande huo kurekebisha makosa yake.

Mahakama imesema kufanya hivyo kungekuwa kinyume na masilahi ya haki kwa warufani ambapo kutokana na sababu hizo, Mahakama ya Rufani iliruhusu rufaa hiyo, ikafuta hatia na hukumu iliyokuwa imetolewa dhidi ya warufani na kuamuru warufani wote waachiliwe huru.

Awali warufani hao walishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, kufuatia tukio la shambulio lililotokea katika Kijiji cha Itumbi wilayani Chunya mkoani Mbeya mwaka 2018.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, tukio hilo lilitokea  15 Agosti 2018 nyumbani kwa mfanyabiashara wa dhahabu Luheta Nhandi, aliyetoa ushahidi kama shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka.

Alidai siku ya tukio, kundi la watu hao waliokuwa wamebeba mchanga unaodaiwa kuwa na dhahabu walifika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo na kumuomba awasaidie kusafisha dhahabu kwa kutumia mashine yake ya kuchenjua dhahabu.

Alidai baada ya kukubaliana na ombi hilo,waliendelea kufanya kazi hiyo kwa muda wa saa mbili,aliwaomba wamwache na mchanga na warudi siku inayofuata kutokana na muda kwenda ambapo warufani hao waliomba kubaki wakidai hawakuwa na fedha ya kula.

Alishuhudia kuwa baadaye alipojaribu kutaka kuona maendeleo yao, mrufani wa nne alimshambulia ghafla kwa kitu kizito kichwani na kuendelea kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo mkono wake wa kulia karibu na vidole.

Alidai kuwa mrufani wa kwanza na wenzake walimfuata mkewe (marehemu kwa sasa) na kumkata kw apanga kichwani,ambapo kundi hilo lilidai fedha ambapo alichukua Sh30 milioni kwenye kabati la nguo ambapo pia walichukua gramu 260 za dhahabu kutoka kwenye droo yake ofisini.

Alidai walipotaka kuondoka,walishauriana kwamba watoboe macho familia nzima kama walivyowatambua ambapo mrufani wa kwanza alimtoboa macho mkewe na kumvunja taya,ambapo walifanya hivyo hata kwa mdogo wake kisha wakaondoka.

Alidai siku 33 baadaye (Septemba 17, 2018) mke wake alifariki ambapo ushahidi wa kitabibu ulithibitish chanzo cha kifo hicho ni jeraha kubwa kichwani.

Baada ya tukio hilo kuripotiwa katika kituo cha polisi cha Chunya, uchunguzi ulifanywa na warufani walikamatwa katika maeneo tofauti kati ya Agosti na Oktoba 2018.

Hata hivyo, katika utetezi wao mahakamani, warufani wote walikana kuhusika na tukio hilo na kudai kuwa ushahidi uliotolewa dhidi yao ulikuwa wa kutungwa na polisi.

Katika rufaa hiyo,warufani hao walikuwa na sababu saba ikiwamo Jaji alikosea  kuwatia hatiani kwa utambulisho wa shahidi wa kwanza ambao haukuwa wakutosha ulikuwa dhaifu na usioaminika, kesi ya utetezi haikuzingatiwa vya kutosha na kusababisha upotoshaji wa haki na upande wa mashtaka haukuthibitisa kesi hiyo bila kuacha shaka.