Migogoro ya ardhi bado mfupa mgumu

Dar es Salaam. Migogoro ya ardhi imeendelea kuwa mfupa ulioshindikana kuvunjika, baada ya malalamiko yake kutawala ziara za Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba na viongozi wengine.

Awali, Serikali ilitangaza hatua mbalimbali, ikiwamo upimaji wa ardhi na utoaji wa hati za kimila hasa vijijini, lakini hazikuwa muarobaini wa changamoto migogoro hiyo.

Malalamiko zaidi yaliyowasilishwa na wananchi kwa Dk Mwigulu kuhusu migogoro hiyo, ni watu wenye kipato cha juu kudaiwa kutumia nafasi na ushawishi wao kuwanyang’anya haki wenye kipato duni.

Kutokana na kukithiri kwa malalamiko kuhusu migogoro ya ardhi katika ziara za Dk Mwigulu, amewaagiza wakuu wote wa mikoa, kufanya uchunguzi katika maeneo yanayolalamikiwa na kuchukua hatua.

Ni migogoro hiyo ya ardhi, ndiyo iliyomsababisha Dk Mwigulu alipokuwa Sumbawanga Mjini, kuwataka viongozi na mawaziri wa kisekta kutafakari na kupendekeza mbinu itakayoleta suluhu ya kudumu.

Waliopewa jukumu hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Hamza Johari, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deo Ndejembi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Profesa Riziki Shemdoe.

Akiwa willayani Nsimbo, mkoani Katavi leo Jumapili Machi 15, 2026, Malisterina Kabita, mkazi wa Kijiji cha Lwila alilalamikia kudhulumiwa shamba la familia yao, changamoto iliyochukua muda mrefu kuanzia mwaka 2009 hadi sasa bila kupatiwa ufumbuzi.

“Nimedhulumiwa shamba la familia la marehemu baba yangu, Michael Kabita. Alikuwa analitumia tangu napata fahamu za kufanya kazi; tulikuwa tukilima naye hadi alipofariki dunia mwaka 1981,” amesema Kabita.

Baada ya kifo cha baba yake, amesema aliteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi na waliendelea kulitumia shamba hilo hadi mwaka 2009.

Amesema mwaka huo, kulifanyika mkutano wa kijiji uliotoa maelekezo kwamba, kutokana na kuanzishwa kwa mradi wa maji, kila mwenye shamba angechangia gharama bila kunyang’anywa eneo lake.

“Baadaye viongozi wa kijiji walinivamia na kunipora ardhi wakinieleza nipishe kwa muda ili wafanye usafi wa kusafisha mfereji wa maji. Nilishangaa baada ya wiki mbili wamegawa shamba lote kwa watu wengine,” amesema Kabita.

Amesema baada ya kuona watu asiowafahamu wamegawiwa shamba hilo, aliamua kutafuta haki yake lakini alizungushwa kwa muda mrefu kabla ya kwenda mahakamani.

“Nilienda mahakamani na nikashinda kesi, lakini nashangaa hadi sasa sijapewa eneo langu. Bado nazungushwa; naomba msaada Waziri Mkuu,” amesema Kabita.

Amesema baada ya Mahakama kutoa hukumu hiyo, alifika katika eneo hilo akiwa na wafanyakazi wake ili kuanza kazi, lakini walivamiwa na mmoja wa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akitaka waliovamia waendelee na shughuli zao bila kumsikiliza, wakidai chama kitawalinda.

“Nimekuwa nikizungushwa na kila kiongozi anayekuja sipati haki yangu. Kila nikijaribu kufanya kazi nanyang’anywa fedha na mali zangu hadi nabaki duni. Najua nchi yetu inaongozwa na Katiba na sheria; kama wanaona sina haki kwanini wasinipeleke mahakamani haki itendeke kuliko kunitesa hivi,” amesema.

Baada ya kupokea kilio hicho, Dk Mwigulu alimuuliza Mkuu wa Wilaya ya Nsimbo, Jamila Yusuf aliyekiri kupokea malalamiko hayo na kueleza kwamba suala hilo lilifika mahakamani na hukumu ilielekeza apewe eneo lake.

Alipoulizwa kwa nini bado hajapewa eneo hilo, Jamila amejibu maofisa ardhi waliwahi kufika katika eneo hilo ili kulipima na kubaini ukubwa wa ardhi anayodai mama huyo.

“Maofisa ardhi walifika kwenye eneo hilo. Walipotaka kulipima ili kubaini ekari halisi, mama alienda mamlaka nyingine,” amesema.

Amesema hali hiyo ilisababisha maofisa hao kushindwa kumalizia upimaji na baada ya uchunguzi walibaini kuwa eneo hilo lina takribani hekta 40 ambazo zimeingia kwa watu wengine.

Katika maelezo yake, Dk Mwigulu amedai migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na utapeli unaofanywa na baadhi ya watu waliopo katika ofisi za umma walioaminiwa kufanya kazi.

“Nilipita eneo la Stalike nimekuta maeneo ya vijiji vitatu ya wakulima yameuzwa. Yameuzwa na wenyeviti wetu wanaotembea na mihuri. Tatizo ni rushwa. Wameuza maeneo yote ambayo walitakiwa kuyatunza,” amesema.

Amesema maeneo ambayo viongozi hao walitakiwa kuyatunza yameuzwa bila kuwashirikisha wananchi, vitendo ambavyo havipaswi kuvumiliwa.

“Utapeli wa kuuza maeneo mara mbili, rushwa na matumizi mabaya ya mihuri ni mambo yanayofanyika. Wengine wanaandaa hata mikhtasari ya vikao na kuweka majina ya watu waliokufa wakidai walihudhuria.

“Ni kana kwamba wamewafufua kuhudhuria vikao. Watu wa namna hii wakibainika wasiachwe mtaani; wafikishwe mikononi mwa sheria,” amesema.

Amesema watu wa aina hiyo hawapaswi kuachwa bila kuchukuliwa hatua, kwa sababu vitendo vyao vinaweza kuvunja udugu na mshikamano uliopo katika jamii.

Baada ya maelezo hayo, Dk Mwigulu alimwelekeza mwenyekiti wa CCM wilayani Nsimbo, kuitisha haraka kikao cha Kamati tendaji kujadili suala hilo.

“Hiki si chama cha kunyang’anya watu. Hiki si kichaka cha wanyang’anyi. Ndiyo maana hata wale tuliowachagua kuongoza Serikali za vijiji, hata kama wanatokana na CCM wakibainika wamehusika waondolewe. Mkuu wa mkoa futa wote, tuchague upya,” ameagiza.

Dk Mwigulu amesema lazima haki za watu ziheshimiwe na haiwezekani wananchi waje kulalamika huku baadhi ya viongozi wakichukulia mambo hayo kwa mzaha.

Kwa kuwa Mahakama tayari iliamua, amesema mama huyo arejeshewe shamba lake, hukumu hiyo itekelezwe bila kucheleweshwa huku akimtaka mkuu wa mkoa huo kusimamia kuhakikisha mama anapewa eneo lake.

“Mkuu wa mkoa na timu yako pamoja na mkuu wa wilaya, nitakapomaliza ziara hapa muambatane na kamati ya ulinzi na usalama muende mkamkabidhi mama shamba lake. Tekelezeni hukumu kama ilivyo. Hilo shamba si lenu; mnaenda kupima la nini?” amesema.