Dar es Salaam. Kutokana na uhaba wa nyumba za makazi kwa watumishi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Karatu, mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Cecilia Paresso, ametoa msaada wa mbao kufanikisha ujenzi wa nyumba hizo.
Watumishi wa CCM na jumuiya zao, kwa maana makatibu wa wilaya hiyo, hawakuwa na nyumba za kuishi, hivyo walilazimika kupanga, jambo lililosababisha chama hicho kuanza ujenzi ambao sasa umefikia hatua ya renta.
Katika utekelezaji wa hilo, Paresso leo, Jumapili, Machi 15, 2026, amekabidhi mbao zenye thamani ya Sh2.5 milioni kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa nyumba hizo.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Paresso amesema kwa kuwa chama kiliekeza kuhakikisha watumishi wake ngazi za wilaya wapate mahali pa kuishi na sio kupanga, alichokitoa ni kutekeleza maelekezo hayo.
“Mimi ni kama mdau, tunachangia kuhakikisha hili linatimia. Karatu tulishaanza ujenzi wa nyumba za viongozi hao na zimefikia hatua ya renta. Kilichobaki ni kupaua, na mbao nilizotoa zitatumika kufanikisha hilo,” amesema.
Paresso amesema, kwa sababu bado kutakuwa na mahitaji kwa ajili ya kumalizia nyumba hizo, ni muhimu wadau waendelee kujitokeza kuchangia kukamilisha ujenzi huo.
Amesisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano katika kujenga na kuimarisha miundombinu itakayowawezesha watumishi wa chama hicho kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Ameeleza kuwa ufanisi katika utendaji wa watumishi hao wa chama ngazi hizo utaimarika iwapo watakuwa na uhuru wa makazi, badala ya kuishi kwenye nyumba za kupanga.
Katika ufafanuzi wake, amesema ni muhimu viongozi hao, hasa makatibu wa chama na jumuiya zao ngazi za wilaya na mikoa, wajengewe makazi ili wasilazimike kupanga wanapokuwa kwenye vituo vya kazi.
Katibu wa CCM Wilaya ya Karatu, Hanafi Msabaha, amesema katika wilaya hiyo hakukuwa na mradi wa nyumba za watumishi wa chama hicho.
Ameeleza kuwa walipoanza, wamejenga nyumba mbili zenye uwezo wa kuchukua familia nne kila moja, ujenzi wake umefikia hatua ya renta.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Cecilia Paresso akıkabidhi bahasha yenye fedha kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Karatu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi za watendaji wa CCM.
“Kwa hatua tuliyofikia, tulikuwa tunahitaji msaada wa mbao kwa ajili ya kupaua. Tunashukuru mbunge ametuchangia,” amesema.
Ameeleza kuwa mchango huo wa mbunge ni matokeo ya ushirikiano mzuri alionao na chama hicho, akisisitiza ni muhimu kuendelea kushirikiana ili kuijenga CCM.