KIUNGO mshambuliaji wa JKT Tanzania, Jafary Maneno, amewataja baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara anaowakubali na kwamba anajifunza mengi kutoka kwao.
Maneno alisema wachezaji hao ni Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli wanaocheza Yanga, pia Elie Mpanzu, Libasse Gueye na Clatous Chama wanaokipiga Simba, huku akibainisha wanachokifanya uwanjani vinamvutia na kujifunza vingi.
“Wapo wengi lakini Pacome ni mchezaji ninayemtazama sana. Mpanzu pia ni mchezaji bora na najifunza mambo mengi kutoka kwake, pia Maxi Nzengeli, Libasse Gueye na Chama wana vitu vingi ambavyo najifunza,” alisema Maneno.
Alisema wachezaji hao wanawapa furaha mashabiki na muda mwingine ubora wao unapungua uwanjani hivyo mashabiki wanapaswa kuelewa.
“Mchezaji hajakamilika, wakituchukulia kama malaika wanatuhukumu kwa sababu sisi ni binadamu. Tukikosea sio kwamba tunapenda, bali ni sehemu ya kazi yetu, tukikosea watu watuelekeze ili tuwe bora zaidi, na tukifanya vizuri watupongeze,” alisema.
Kabla ya kujiunga na JKT Tanzania, Maneno aliwahi kuzichezea TMA Stars ya Ligi ya Championship pamoja na Mlandege FC ya Ligi Kuu Zanzibar.