Wacongo kumpa muhula mwingine Denis Sassou Nguesso?    

Dar es Salaam. Wananchi wa Jamhuri ya Kongo (Congo Brazzaville), wamepiga kura leo Jumapili Machi 15, 2026 kumchagua Rais wao mpya katika uchaguzi ambao wachambuzi wengi wanaona unaweza kumrejesha tena madarakani kiongozi mkongwe, Denis Sassou Nguesso.

Takribani wapiga kura milioni 3.2 walijiandikisha kushiriki katika uchaguzi huo, lakini mchakato umeingia katika mjadala mkali baada ya vyama kadhaa vikubwa vya upinzani kususia uchaguzi huo vikidai haukidhi viwango vya uhuru na uwazi.

Licha ya kuwapo kwa wagombea sita wanaoshindana na rais huyo mkongwe, wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema hakuna anayetarajiwa kutoa ushindani wa kweli baada ya vyama vikuu vya upinzani kususia uchaguzi huo.

Mchambuzi wa siasa wa Brazzaville, Profesa Jean Claude Mavoungou amenukuliwa na vyombo vya habari vya ndani akisema, “Kwa muundo wa siasa za Kongo-Brazzaville na nguvu ya chama tawala, ni vigumu kuona mgombea yeyote akimzuia Sassou Nguesso kushinda.”

Kwa mtazamo wake, uchaguzi wa mwaka huu unaonekana zaidi kama uthibitisho wa nguvu za kisiasa alizojijengea kwa miongo kadhaa.

Sassou Nguesso ni mmoja wa viongozi waliokaa madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika tangu alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1979, akiwa kiongozi wa serikali ya kijeshi na kutawala hadi 1992 aliposhindwa katika uchaguzi wa vyama vingi.

Hata hivyo, alirejea madarakani mwaka 1997 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoibuka kufuatia mivutano ya kisiasa na kijeshi na tangu wakati huo ameendelea kushinda chaguzi kadhaa, akijenga mtandao mkubwa unaompa nguvu katika mfumo wa utawala wa nchi hiyo.

Mwaka 2015, kura ya maoni ya katiba ilibadilisha masharti yaliyokuwa yanazuia kikomo cha umri na mihula ya rais, hatua iliyomruhusu kugombea tena licha ya amuzi huo kupingwa vikali na makundi ya upinzani, ambayo hadi sasa yanaendelea kuhoji uhalali wa mabadiliko hayo.

Aidha, uchaguzi huo umefanyika huku viongozi wakuu wawili wa upinzani Jenerali Jean Marie michel makoko na Andre Okombi Salissa, wanazuiliwa gerezani  kwa karibu muongo mmoja baada ya kushtakiwa na makosa ya kuhatarisha usalama wa taifa.

Wachambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora nchini humo wanasema changamoto kubwa kwa serikali ijayo haitakuwa ushindi wa kisiasa kwa Rais mpya bali ni hali ya uchumi wa taifa hilo.

Ingawa Jamhuri ya Kongo ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mafuta katika ukanda wa Afrika ya Kati, nchi hiyo inakabiliwa na madeni makubwa ya kimataifa, ukosefu wa ajira na kiwango kikubwa cha umaskini.

Kwa mujibu wa takwimu za wachambuzi wa uchumi nchini humo, zaidi ya nusu ya wananchi wanaishi chini ya mstari wa umaskini huku vijana wengi wakikosa ajira.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Marie Therese Ndziessi, amenukuliwa na vyombo vya habari akibainisha kuwa hitaji la wananchi si nani anashinfa uchaguzi bali majibu ya mahitaji yao.

“Uchaguzi unaweza kuleta mwendelezo wa kisiasa, lakini wananchi wanatarajia mageuzi ya kiuchumi yanayogusa maisha yao ya kila siku,” amesema.

Kwa hali hiyo, kura ya leo haionekani tu kama ushindani wa kisiasa, bali pia kipimo cha namna mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo ulivyojengeka ndani ya zaidi ya miongo minne ya ushawishi wa kiongozi mmoja.

Iwapo matokeo yatakwenda kama wachambuzi wanavyotabiri, Rais Denis Sassou Nguesso aliyetawala kwa mihula minne yenye jumla ya miaka 42, anaendeleza historia ya watawala wa Afrika waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi, akichuana na barani Afrika anafuatia Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea aliyetawala miaka miaka 45 na Paul Biya wa Cameroon aliyefikisha miaka 43 madarakani.