Timu ya Mbeya City imeshindwa kutamba ikiwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-1, dhidi ya Singida Black Stars, katika mechi kali ya Ligi Kuu Bara.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja hapo, Mbeya City ilianza kupata bao kupitia kwa Vitalis Mayanga, dakika ya 14, akiunganisha mpira wa kichwa, uliopigwa na beki, Baraka Maranyingi.
Baada ya bao hilo, Singida ilianza kujibu mapigo, ambapo dakika ya 32, Emmanuel Keyekeh, aliifungia timu hiyo kwa mkwaju wa penalti, baada ya nyota wa kikosi hicho, Mossi Nduwumwe, kuchezewa madhambi eneo la hatari na Adilly Buha wa Mbeya City.
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza, timu hizo zilifungana bao 1-1, ingawa kipindi cha pili kilikuwa cha tabu kwa Mbeya City iliyopo chini ya Mecky Maxime, baada ya kuruhusu bao la pili la dakika ya 70, lililofungwa na Mossi, akipokea pasi ya Lamine Jarjou.
Beki wa kushoto wa Singida, Ibrahim Imoro aliyeingia dakika ya 46, akichukua nafasi ya Rahim Shomary, ndiye aliyepeleka zaidi kilio kwa Mbeya City, baada ya kufunga mabao mawili dakika ya 73 na 87, akifunga kwa mashuti makali nje ya eneo la 18.
Kichapo hicho kwa Mbeya City, kinakuwa ni cha pili mfululizo, baada ya mechi iliyopita dhidi ya Fountain Gate kuchapwa bao 1-0, Machi 3, 2026, ingawa kiujumla ni kipigo cha tisa msimu huu, ikiendelea kubakia nafasi ya 14 na pointi zake 13.
Katika mechi 16 ilizocheza Mbeya City msimu huu za Ligi Kuu, imeshinda tatu tu, sare nne na kupoteza tisa, huku kwa upande wa safu ya ushambuliaji imefunga mabao 13, wakati, eneo la kujilinda imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.
Kwa upande wa Singida Black Stars, imepata ushindi wa kwanza baada ya kuchapwa mechi mbili mfululizo, ikianza na kichapo cha mabao 3-0, dhidi ya Yanga, kisha 2-1, mbele ya Simba, ambapo kwa sasa inafikisha pointi 22, ikishika nafasi ya sita.
Kikosi hicho kimecheza mechi 14 za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo imeshinda sita, sare nne na kupoteza nne, ikifunga mabao 16 na kuruhusu 14.