ACHPR yataka wote waliomteka Mshabaha nchini Kenya wawajibishwe

Dar es Salaam. Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHRO), imepongeza kukamatwa kwa washukiwa watatu wanaodaiwa kuhusika katika jaribio la kumteka nyara mwanaharakati wa Tanzania, Mshabaha Mshabaha lililotokea nchini Kenya.

Washukiwa hao ni raia wawili wa Kenya na Mtanzania mmoja ambao tayari wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayohusiana na tukio hilo.

Tume hiyo pia imeitaka Serikali ya Kenya kuhakikisha uchunguzi wa haraka, wa kina na usiopendelea upande wowote unafanyika ili kubaini na kuwafikisha mahakamani wote waliohusika kupanga, kufadhili na kuwezesha jaribio hilo la utekaji.

Mbali na hilo, ACHPR imeitaka Kenya kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha ardhi yake haitumiki kwa vitendo vya ukandamizaji wa kimataifa, ikiwamo utekaji wa kuvuka mipaka, utoaji usio halali wa watu au vitisho dhidi ya wapinzani wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu kutoka nchi nyingine.

Watuhumiwa waliofikishwa mahakamani ni Edward Mwangi, raia wa Kenya anayeishi Afrika Kusini; Nelson Wanjohi, raia wa Kenya; pamoja na Aziz Hamad, raia wa Tanzania.

Jaribio hilo la utekaji lililotokea Februari 22, 2026 katika Kaunti ya Machakos, linadaiwa kuhusisha kumchoma sindano mwanaharakati huyo kabla hajaokolewa na polisi wa Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa ya ACHPR iliyotolewa Machi 13, 2026 kupitia tovuti yake, kauli hiyo imetolewa na Kamishna Solomon Ayele Dersso ambaye ni mwandishi maalumu wa tume hiyo kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Kenya.

Katika taarifa hiyo, tume hiyo imesema itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa tukio hilo na kushirikiana na Serikali ya Kenya ili kuimarisha ulinzi wa watetezi wa haki za binadamu pamoja na utawala wa sheria katika ukanda.

ACHPR pia imepongeza mamlaka za Kenya kwa hatua walizochukua kulinda uhuru na usalama wa watu waliopo ndani ya mipaka yake.

“Tunaikumbusha Kenya kuwa chini ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, nchi wanachama zina wajibu wa kuhakikisha haki ya kila mtu ya uhuru na usalama wa nafsi yake inalindwa kwa mujibu wa kifungu cha sita cha mkataba huo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Tume hiyo imeongeza kuwa uchunguzi wa kina ni muhimu si tu kwa ajili ya kesi hiyo bali pia katika kuimarisha dhamira ya muda mrefu ya Kenya ya kuhakikisha watu wote wanaoishi au kuingia nchini humo kisheria wanapata ulinzi unaotambuliwa na mkataba huo wa haki za binadamu.

Aidha, tume hiyo imesisitiza kuwa vitendo vya vitisho, utekaji nyara, kupotea kwa watu au kuzuiwa kiholela kwa uhuru wa kutembea vinadhoofisha haki za msingi zinazolindwa na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.

Kenya yatakiwa kuchukua hatua nne

Kwa mujibu wa ACHPR, kuna hatua nne muhimu ambazo Kenya inapaswa kuchukua. Hatua ya kwanza ni kufanya uchunguzi wa haraka, wa kina na usioegemea upande wowote ili kuwawajibisha wote waliohusika kupanga, kuratibu au kufadhili tukio hilo.

Pili, imeitaka Kenya kuimarisha taratibu za ulinzi wa kitaifa kwa watu wote walioko nchini humo, hususan wale wanaokabiliwa na hatari kubwa ya vitisho au unyanyasaji, wakiwemo wanaharakati na watu wanaojihusisha na shughuli za kisiasa kwa njia ya amani.

Hatua ya tatu ni kuhakikisha ardhi ya Kenya haitumiki kwa vitendo vya ukandamizaji wa kimataifa kama vile utekaji wa kuvuka mipaka au vitisho dhidi ya wapinzani wa kisiasa na wanaharakati kutoka nchi nyingine.

Nne, tume hiyo imeitaka Kenya kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili kulinda nafasi ya kiraia na kuhakikisha haki ya uhuru wa kutembea inalindwa kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.

Maelezo ya tukio la utekaji

Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa mahakamani, mwanaharakati Mshabaha Mshabaha alishambuliwa na watu watatu waliomteka Februari 22, 2026 na kumchoma sindano yenye kemikali ambazo bado hazijabainishwa.

Akiwa ndani ya gari la watekaji hao, alijaribu kupambana kuokoa maisha yake, hali iliyosababisha watekaji kumtupa katika eneo la Lukenya. Wakati huo taarifa za tukio hilo tayari zilikuwa zimewafikia polisi wa vituo vya Lukenya na Kyumbi.

Kwa kushirikiana na maofisa wa Directorate of Criminal Investigations pamoja na polisi wa vituo hivyo, walifanikiwa kulisimamisha gari lililotumika na kuwakamata watuhumiwa hao watatu.

Tukio hilo ni la pili kuripotiwa katika kipindi cha miezi michache ambapo Mtanzania anadaiwa kutekwa nchini Kenya.

Januari 12, 2026, mwanaharakati na mwandishi wa habari Maria Sarungi Tsehai pia alinusurika jaribio la utekaji baada ya kupambana na watekaji wake ndani ya gari kabla ya kuachiwa.

Maria Sarungi na Mshabaha wamekuwa wakishiriki mijadala ya kisiasa kupitia jukwaa la Maria Space katika mtandao wa X, lililokuwa likijulikana awali kama Twitter.