RIPOTI MAALUMU: Asilimia 40 ya shule za sekondari nchini hazina maabara za sayansi

Lushoto/Rombo. Shule mbili kati ya tano za sekondari za Serikali nchini hazina uhakika wa kuzalisha wabobezi wa masomo ya sayansi kutokana na ukosefu wa maabara za kujifunzia.

Hali hiyo inalazimisha wanafunzi wengi kujifunza sayansi kwa nadharia pekee, bila kupata fursa ya kufanya majaribio ya vitendo.

Kwa mujibu wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Tanzania ilikuwa na shule za sekondari za Serikali 4,894 zenye maabara 8,710 za masomo ya sayansi ya baiolojia, kemia na fizikia.

Hata hivyo, uchambuzi wa takwimu hizo unaonesha kuwa kwa idadi hiyo ya shule kulipaswa kuwe na maabara 14,682 ili kila shule iwe na maabara tatu kama inavyotakiwa.

Hivyo bado kuna upungufu wa maabara 5,972 sawa na asilimia 40.68 ya mahitaji yote. Kwa tafsiri nyingine, takribani shule 1,991 hazina maabara.

Kutokana na hali hiyo, takribani nusu ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi hulazimika kujifunza nadharia pekee bila kugusa vifaa, kufanya majaribio au kuona kwa vitendo kile wanachojifunza darasani.

Kwa mujibu wa Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule wa mwaka 2020, shule inayotaka kusajiliwa inapaswa kuwa na maabara tatu za fizikia, kemia na baiolojia.

Kanuni ya 15 (1)(c) ya mwongozo huo inamtaka ofisa elimu wa mkoa au wilaya kuthibitisha uwepo wa maabara zinazofanya kazi kabla ya usajili kufanyika.

Ili shule ipate usajili, ni lazima iwe na maabara hizo tatu. Hata hivyo, utekelezaji wa kanuni hiyo haujawa thabiti katika baadhi ya maeneo, jambo lililofanya walimu na wanafunzi kukabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya sayansi.

Katika shule nyingi, simulizi za walimu na wanafunzi zinaonesha juhudi kubwa zinazofanywa, ili kuendelea kufundisha licha ya ukosefu wa vifaa na maabara. Wanafunzi wengi hujikuta wakisoma sayansi bila kufanya majaribio ya vitendo kwa kiwango kinachotakiwa.

Baadhi ya wanafunzi hufika hadi kidato cha nne wakiwa wameingia maabara mara chache, wakati mwingine mara moja pekee. Wengine hulazimika kutumia kifaa kimoja wakiwa wanafunzi watano au zaidi.

Hali hiyo inaibua swali kuhusu namna taifa linavyotarajia kuzalisha wataalamu wa sayansi kama wahandisi, madaktari na watafiti wakati mfumo wa elimu hauwapi wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo.

Sayansi si somo la kusoma pekee bali ni la kugundua, kujaribu na kufanya majaribio kabla ya kufikia majibu sahihi. Bila maabara na vifaa vya kujifunzia, mchakato huo unakuwa mgumu kwa wanafunzi wengi.

Asilimia 40.68 ya uhaba wa maabara si takwimu tu, bali ni simulizi ya vikwazo vinavyowakabili wanafunzi na walimu katika shule nyingi za Serikali. Shule nyingi zina bajeti ndogo, huku jamii zinazozizunguka zikifahamu umuhimu wa uwekezaji katika elimu ya sayansi lakini uwezo wa kifedha ukiwa mdogo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kuanzia Novemba 2025 hadi Januari 2026 katika wilaya za Rombo mkoani Kilimanjaro na Lushoto mkoani Tanga umeonesha hali halisi ya changamoto hiyo.

Wanafunzi wa Kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Mraokeryo wakiwa wanamsikiliza mwalimu wa somo la fizikia shuleni hapo huku wengine wakilazimika kueagamia meza ili kuweza kumudu kusimama mida wote wa kipindi kilichofanyika katika chumba cha sayansi kinachotumika kufundishia somo la fizikia, bailojia na kemia

Katika Wilaya ya Rombo, licha ya kuwa karibu na Mlima Kilimanjaro, shule nyingi zinatajwa kuwa na uhaba mkubwa wa maabara.

Katika jitihada za kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo ya vitendo, walimu na uongozi wa shule wamekuwa wakitafuta mbinu mbalimbali. Hata hivyo, katika shule nyingi kuna maabara moja pekee inayotumika kufundishia masomo yote ya sayansi.

Hali hiyo inaathiri ujifunzaji wa wanafunzi na kuongeza mzigo wa kazi kwa walimu ambao wakati mwingine hulazimika kutumia muda wa ziada kuwasaidia wanafunzi kufanya majaribio.

Mwalimu wa baiolojia katika Shule ya Sekondari Mraokeryo iliyopo Kata ya Mraokeryo, Abdallah Thabiti, anasema walimu hulazimika kupanga ratiba ili kuepuka mgongano wa kutumia maabara.

“Kuna wakati walimu wawili au watatu wote wanahitaji kutumia maabara kwa wakati mmoja. Hivyo tumelazimika kupanga ratiba maalumu, ili kila mmoja apate nafasi ya kuwafundisha wanafunzi,” anasema.

Anaongeza kuwa wakati mwingine hulazimika kutumia muda wa ziada kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo, ili kuhakikisha wanapata uelewa unaohitajika.

Mwalimu John Venance wa Shule ya Sekondari Makiidi iliyopo Kata ya Makiidi anasema kwa kawaida shule ilipaswa kuwa na maabara tatu, lakini ipo moja tu.

“Miundombinu haijaridhisha. Maabara moja inatumika kufundishia masomo yote ya sayansi, jambo ambalo linaathiri ufundishaji kwa vitendo,” anasema.

Anasema pia kukosekana kwa vifaa vya kutosha kunawalazimu wanafunzi kufanya majaribio katika makundi makubwa, jambo linaloweza kuwaacha baadhi yao bila kuelewa vizuri.

Mwananchi pia lilizungumza na mwalimu Perpetua Tesha wa shule hiyo anayesema kutokana na uhaba wa maabara na vifaa mara nyingi, wanafunzi wa kidato cha nne ndiyo wanaopewa kipaumbele kufanya majaribio.

“Tunajitahidi kuwasaidia wanafunzi wa kidato cha nne kwa sababu wanakaribia kufanya mitihani ya taifa. Wengine hulazimika kujifunza kwa nadharia,” anasema.

Katika Shule ya Sekondari Ubaa iliyopo Kata ya Ushiri, mwalimu Krisamta Shirima anasema kukosekana kwa miundombinu ya kutosha kunawalazimu kutumia muda mwingi kutafuta vifaa vya maabara.

“Hata vifaa vilivyopo vinahifadhiwa kwenye maboksi. Tunatumia muda mwingi kuvitoa na kuvirudisha kabla ya kuanza majaribio,” anasema.

Kwa mujibu wa takwimu za Tamisemi, hadi mwaka wa fedha 2024/2025 kulikuwa na maabara 8,710 katika shule za sekondari za Serikali, huku maabara 5,972 zikihitajika ili kukamilisha mahitaji.

Hata hivyo, takwimu hizo hazikuonesha kwa uwazi ni masomo gani ya sayansi yenye upungufu mkubwa zaidi wa maabara.

Kwa mujibu wa takwimu za Best Education zilizotolewa mwaka 2021, Tanzania ilikuwa ikihitaji maabara 4,081 za baiolojia, 4,079 za kemia na 4,060 za fizikia.

Lakini maabara zilizokuwapo zilikuwa karibu nusu ya mahitaji hayo. Baiolojia zilikuwa 2,033, kemia 2,198 na fizikia 1,813.

Somo la fizikia lilikuwa na maabara chache zaidi, zikiwa sawa na asilimia 44.6 ya mahitaji.

Kwa nini Rombo na Lushoto

Takwimu za Best Education za mwaka 2017 zilionesha Wilaya ya Lushoto ilikuwa na upungufu mkubwa wa maabara kwa asilimia 92.2, ikifuatiwa na Rombo yenye asilimia 76.

Dodoma Mjini ilikuwa katika nafasi ya tatu kwa kuwa na upungufu wa asilimia 72.5.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa hata katika shule zenye maabara moja, miundombinu yake mara nyingi haikidhi mahitaji kama ilivyoshuhudiwa katika wilaya mbili za Rombo (Kilimanjaro) na Lushoto (Tanga).

Mwananchi imeshuhudia katika baadhi ya maabara, wanafunzi hulazimika kusimama muda wote wa kipindi kwa sababu ya kukosekana kwa viti.

Hali hiyo hupunguza umakini wa wanafunzi wakati wa kujifunza.

Baadhi ya maabara pia hazitumiki ipasavyo kutokana na kukosekana kwa maji au vifaa muhimu vya kufanyia majaribio.

Mwalimu wa baiolojia katika Shule ya Sekondari Lushoto, Upendo Ayoub anasema ukosefu wa maji na gesi ya maabara unaathiri ufundishaji wa sayansi.

“Tunahitaji gesi na vyanzo vya maji, ili kurahisisha ufundishaji kwa vitendo,” anasema.

Katika Shule ya Sekondari Matoburu, mwalimu wa taaluma, Maombi Mahuna anasema baadhi ya vifaa hulazimika kuhifadhiwa katika vyumba visivyokusudiwa kwa kazi hiyo.

Wataalamu wa maabara wachache

Mbali na changamoto za miundombinu, wataalamu wa maabara pia ni wachache.

Kati ya shule nane zilizotembelewa katika wilaya za Rombo na Lushoto, ni tatu pekee zilikuwa na wataalamu wa maabara.

Baadhi ya vifaa vya maabara vikiwa vimehifadhiwa katika stoo inayohifadhi vifaa hivyo katika shule ya sekondari Mraokeryo iliyopo wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro. Jambo hili linahatarisha usalama wa vifaa vinavyoweza kuvunjika kwa urahisi vinavyotumiwa shuleni hapo.

Hawa Rajab, mtaalamu wa maabara katika Shule ya Sekondari Shambalai wilayani Lushoto, anasema mara nyingi hulazimika kushughulikia masomo yote matatu ya sayansi.

“Ninawasiliana na walimu ili kujua ni jaribio gani wanataka kufanya na kuwasaidia kuandaa vifaa kabla ya wanafunzi kuingia maabara,” anasema.

Upungufu huu wa maabara unawanyima wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo.

Yosia Enock, mwanafunzi wa kidato cha nne, anasema hadi anafika ngazi hiyo ya elimu amefanya vitendo siku moja pekee katika somo la kemia.

“Hatujawahi kufanya kwa vitendo fizikia na baiolojia. Naathirika kwani vitu vingine lazima uhakikishe ukiwa maabara. Kuna wakati tulifanya mtihani uliohitaji kutumia maabara, lakini tulifanya alternative practical (majaribio mbadala),” anasema.

Lucia Vicent, mwanafunzi wa kidato cha tano, anasema: “Ukifanya vitendo unaweza kukumbuka vizuri zaidi tofauti na kufanya kwa nadharia. Mara nyingi tunaingia tu muda wa vipindi tunaoneshwa lakini hatufanyi vitendo.”

Moja ya chumba kinachotumiwa na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nduweni kama chumba cha maabara wakati wa mitihani ili waweze kufanya mitihani ya vitendo kutokana na uhaba wa maabara uliopo shuleni hapo, shule hii ina chumba kimoja cha maabara pekee kinachotumika kufundisha masomo yote.

Mbali na wanafunzi hao wa Shule ya Sekondari Nduweni, Yusuph Imam kutoka Shule ya Sekondari Matoburu anasema hadi wanafika kidato cha nne wameingia maabara mara tano pekee.

Kauli yake inaungwa mkono na Saumu Idd anayesema labda kwa sababu wameingia kidato cha nne ndiyo wataingia maabara mfululizo tofauti na miaka ya nyuma.

Akitoa picha ya jumla, Ofisa Taaluma Sekondari Wilaya ya Rombo, Vianne Mgoma, anasema halmashauri yake ina shule 45 za Serikali ikiwa na maabara 69 zilizokamilika na kutumika kati ya maabara 135 zinazohitajika.

“Ili kumaliza tatizo hili, fedha zimeendelea kupokelewa kutoka Serikali Kuu na nyingine zinatengwa na halmashauri ili kukamilisha baadhi ya majengo ya maabara yanayohitaji kukamilishwa,” anasema.

Kwa upande wa Wilaya ya Lushoto, Ofisa Elimu Sekondari, Shahara Shaibu, anasema katika wilaya yake yenye shule 66 za sekondari wanazo maabara 13 za fizikia, kemia 30 na baiolojia 15.

Kati ya maabara 198 zinazohitajika, ni 58 pekee zinazofanya kazi huku akiweka bayana mipango waliyonayo.

Maabara mbili kati ya tatu zinazohitajika katika shule ya Sekondari Ubiri zikiwa katika hatua za kusubiri umaliziaji jambo linalofanya madarasa yote kutegemea chumba kimoja kusoma masomo ya vitendo katika masomo ya Baiolojia, kemia na fizikia.

“Lakini Serikali iliratibu ujenzi wa maabara tatu kwa kila shule kwa nguvu za wananchi na baadaye kila mwaka imekuwa ikitenga fedha za kumalizia maabara nne. Jitihada hizo zinaendelea hadi tutakapokamilisha,” anasema.

Naibu Waziri wa Tamisemi, Reuben Kwagilwa, anasema katika kipindi cha awamu ya sita shule 1,300 zimejengwa zikiwa na miundombinu yote ikiwemo maabara.

“Shule zote zilizojengwa katika kipindi hiki zina maabara. Mbali na shule 1,300, pia Serikali imejenga shule saba za kikanda kwa ajili ya watoto wa kiume na 26 za sayansi za wasichana. Hakuna hata moja iliyojengwa bila maabara,” anasema.

Anasema changamoto ipo zaidi katika shule za muda mrefu za kata zilizojengwa kwa nguvu za wananchi.

“Zaidi ya Sh1.3 trilioni kwa sekondari na Sh1.5 trilioni kwa shule za msingi zimetumika. Tunaendelea kupambana na zile za zamani kupitia programu za kuendeleza miundombinu na tunaendelea kujenga maabara katika shule ambazo hazina,” anasema Kwagilwa.

Anaongeza kuwa kutokana na wingi wa mahitaji wakati mwingine wanalazimika kutengeneza maabara moja inayoweza kutumika kufundishia masomo yote, huku wakiendelea kukamilisha maeneo machache ambayo hayana maabara kabisa.