VITA MASHARIKI YA KATI: Tujipange, bei ya mafuta kupaa

Dar es Salaam. Mpaka sasa vita vya Mashariki ya Kati vinavyohusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran vimegharimu maisha ya watu wengi katika mataifa hayo, lakini kwa Afrika vinang’ata kwa namna yake, ikiwemo kupanda kwa bei na changamoto ya upatikanaji wa mafuta.

Tayari bei ya mafuta imepanda hadi kufikia karibu Dola 100 za Marekani jana, ikiongezeka kutoka Dola 70 kabla ya vita, na kuna wasiwasi wa bei kufikia Dola 120 endapo vita vitaendelea.

Hofu nyingine kubwa ni kuvurugika kwa mnyororo wa usambazaji wa nishati ya mafuta na gesi ya kupikia (LPG), kwani mataifa ya Mashariki ya Kati huchangia hadi asilimia 30 ya mafuta yote yanayozalishwa duniani.

Pia, zaidi ya asilimia 20 ya mafuta yanayosambazwa duniani hupitia Lango la Hormuz. Aidha, takriban asilimia 50 ya mafuta ghafi kutoka Mashariki ya Kati kwa ajili ya viwanda vya kusafisha mafuta nchini India hupitia lango hilo ambalo kwa sasa halipitiki, jambo ambalo limepaisha bei yake.

Tanzania nayo inaathirika kwa kuwa, katika kipindi cha miezi sita hadi Machi 2026, imeagiza kiasi kikubwa cha mafuta kutoka Falme za Kiarabu (UAE) kwa asilimia 37, India asilimia 40, Saudi Arabia asilimia 8, Oman asilimia 8, Kuwait asilimia 4 na Bahrain asilimia 2. Hivyo, sehemu ya uhakika ya kupata mafuta sasa inabaki kuwa India.

Kwa sasa meli za mafuta kuelekea India zinaruhusiwa kupita katika eneo hilo, lakini endapo India itakosa mafuta kutoka Mashariki ya Kati, uzalishaji wa viwanda vyake vya kusafisha mafuta utaathirika na kuathiri nchi kama Tanzania ambazo zinaagiza takriban asilimia 40 ya mahitaji yake kutoka huko.

Kutokana na kiwanda cha kusafisha mafuta (refinery) kufungwa miaka ya 1990, Tanzania huagiza mafuta safi (refined products) ambayo upatikanaji wake hutegemea zaidi upatikanaji wa mafuta ghafi na urahisi wa kuyasafirisha.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, anasema kwa sasa akiba ya mafuta iliyopo nchini ipo vizuri na Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa akiba hiyo haiishi.

Hata hivyo, kama mbadala, inaweka msukumo katika matumizi ya nishati ya gesi asilia iliyosindikwa (CNG), akisema kwa Dar es Salaam pekee mpaka sasa kuna vituo 10.

“Tunaangalia namna TPDC iweke kituo Morogoro, Dodoma, Arusha na kwingine kama mbadala wa mafuta kwa nishati ya vyombo vya moto. Vilevile tunaendelea na mazungumzo na mataifa ambayo hayapo Mashariki ya Kati ili kuhakikisha kuwa nchi inapata mafuta wakati wote,” amesema Ndejembi.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Clouds juzi, Ndejembi amesema Watanzania hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kwani Serikali inafanya kila jitihada, ikiwemo kuzungumza na wazalishaji wengine wa mafuta tofauti na wa Mashariki ya Kati ili kuhakikisha yanapatikana wakati wote na bei hazipandi kwa kiwango kikubwa.

Kwa kawaida Tanzania hutumia mafuta yaliyonunuliwa miezi miwili iliyopita, hivyo mafuta yanayotumika hivi sasa na mwezi ujao (Aprili) hayakunuliwa wakati wa vita vinavyoendelea. Hata hivyo, bei yake inaweza kuathiriwa na hali ya soko la sasa, kwani kwenye ukokotoaji wa bei hujumuishwa gharama za usafiri ambazo huenda zikawa kubwa kutokana na meli nyingi za mafuta kukwama baharini.

Kanuni za Kukokotoa Bei za Mafuta za Mwaka 2023 [GN Na. 761] zinaeleza kuwa bei hupangwa kwa kuzingatia bei za mafuta safi katika soko la dunia, gharama za uagizaji mafuta (premiums), kiwango cha kubadilisha fedha za kigeni, gharama na faida kwa wafanyabiashara wa jumla na rejareja wa mafuta, pamoja na kodi za Serikali, tozo na ada za taasisi, tozo za manispaa na gharama za usafirishaji.

Mchambuzi wa uchumi na masuala ya fedha, Rashid Aziz, amesema kwa kuwa Tanzania huagiza mafuta yaliyosafishwa (refined products) kama petroli, dizeli na mafuta ya taa, si ghafi, kutoka kwenye viwanda vya kusafisha mafuta (refineries) vya nchi za Kiarabu, upangaji wa bei nchini unafuata mwenendo wa bei za marejeo ya mafuta yaliyosafishwa katika masoko ya Arabuni na Uajemi.

Kwa mfano, ikiwa bei ya mafuta kwenye Ghuba ya Uajemi itapanda kwa asilimia 5, bei ya kikomo (cap price) inayopangwa na Ewura kwa wauzaji nchini lazima iongezeke kwa mafuta yatakayonunuliwa kwa wakati huo.

Upangaji wa bei unazingatia pia ushuru, tozo na mabadiliko ya thamani ya sarafu ili kupata bei ya mlaji. Tanzania inatumia mfumo wa Uagizaji wa Mafuta wa Pamoja ambapo kampuni moja hushinda zabuni ya kuagiza mafuta kwa niaba ya nchi nzima.

“Kwa ujumla sisi hatuna uwezo wa kudhibiti bei kwa kuwa hatuzalishi wala kusambaza. Hatua zilizo ndani ya uwezo wetu ni za kikodi. Serikali inaweza kupunguza baadhi ya kodi katika bidhaa hiyo, ili mlaji wa mwisho asipate maumivu makubwa,” amesema Rashid, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU).

Rashid amesema, mbali na hatua hiyo, Serikali inaweza pia kuamua kuweka ruzuku katika bidhaa hiyo muhimu ili kulinda uchumi na kupunguza athari za kupanda kwa bei, akitolea mfano kuwa Serikali ilifanya hivyo mwanzoni mwa vita kati ya Russia na Ukraine vilivyosababisha ongezeko kubwa la bei.

Ongezeko kubwa la bei za mafuta linaweza kuongeza mfumuko wa bei na kuathiri uchumi, ikizingatiwa kuwa mafuta yanahusika kwa sehemu kubwa katika uzalishaji, lakini pia katika usafirishaji na uchukuzi.

Kupanda kwa bei za mafuta duniani kutaathiri mwenendo wa bei ya mafuta nchini na kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii, hivyo kusababisha mfumuko wa bei na kupunguza uwezo wa wananchi kununua bidhaa (purchasing power).

“Mafuta ni chanzo kikuu cha nishati hapa nchini kwetu. Ongezeko la bei yake lina athari kubwa katika maeneo mengi, hususani sekta za uzalishaji, usafirishaji na uchukuzi,” amesema Dk Goodhope Mkaro, ambaye ni mchambuzi wa uchumi na masuala ya fedha.

Amesema gharama za uzalishaji na uchukuzi zikipanda, gharama za vitu zitakuwa juu wakati kipato cha walio wengi kikisalia kuwa kilekile, hivyo kutakuwa na athari ya moja kwa moja katika uwezo wa watu kufanya manunuzi.

“Kutakuwa na athari kubwa katika eneo la uzalishaji ambazo zitahamia upande wa ulaji, hivyo kutakuwa na athari za moja kwa moja kwa wananchi. Katika usafiri huenda nauli zikapanda, lakini pia gharama za usafirishaji wa mazao na pembejeo zitaongezeka, hivyo hata bei za vyakula huenda zikapaa,” amesema.