Serikali yaeleza siri kushirikiana na sekta binafsi huduma za afya

Dar es Salaam. Serikali imeeleza utayari wake wa kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta binafsi, likiwamo Jukwaa la Watendaji Wakuu nchini (CEOrt) ili kuhakikisha huduma ya afya kwa wote inapatikana kwa Watanzania wote.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe ametoa kauli hiyo jana Jumamosi Machi 14, 2026 wakati wa hafla ya chakula cha jioni  kilichoandaliwa na jukwaa hilo jijini Dar es Salaam.

Viongozi Serikali, sekta biashara, watunga sera, washirika wa maendeleo na wadau wa afya walikutana kujadili nafasi ya sekta binafsi katika kuimarisha mfumo wa afya nchini, chini ya kauli mbiu isemayo: “Afya kama Uwekezaji: Hoja ya kibiashara kwa Afya kwa wote.”

Dk Magembe amesema Serikali inatambua umuhimu wa ushirikiano na sekta binafsi katika kuendeleza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini kote.

“Serikali iko tayari kushirikiana na sekta binafsi kupitia majukwaa kama CEO Roundtable of Tanzania ili kuhakikisha bima ya afya kwa wote inakuwa halisi kwa kila Mtanzania,” amesema mganga mkuu huyo.

Amesema ajenda ya Serikali ya kufanikisha huduma ya afya kwa wote inaongozwa na nguzo kuu tatu ambazo ni kupanua upatikanaji wa huduma za afya, kuboresha uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu, pamoja na kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya.

“Bima ya Afya kwa Wote inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kukumbana na changamoto za kifedha. Miundombinu na huduma za afya zinaendelea kupanuliwa, lakini mfumo wa bima unahakikisha gharama hazizuii wananchi kupata huduma wanazohitaji,” amesema.

Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mfumo wa afya katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Pia, amesema takribani asilimia 80 hadi 85 ya Watanzania sasa wanaweza kufika kwenye kituo cha afya ndani ya umbali wa kilomita tano.

Aidha, amesema uwekezaji unaoendelea katika teknolojia za uchunguzi wa magonjwa, huduma za dharura pamoja na mafunzo ya kitaalamu kwa madaktari bingwa umeimarisha uwezo wa mfumo wa afya nchini.

“Rasilimali muhimu zaidi kwa taasisi yoyote ni watu wake. Tukiiwekeza katika rasilimali watu na kulinda afya ya wafanyakazi wetu, tunaimarisha uzalishaji, ustahimilivu wa uchumi na maendeleo ya muda mrefu ya Taifa,” ameongeza.

Awali, akizungumza katika jukwaa hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Strategis Insurance Group Tanzania Limited, Dk Flora Minja amesema mifumo imara ya afya ni muhimu si tu kwa ustawi wa jamii bali pia kwa uendelevu wa biashara na maendeleo ya uchumi.

Dk Minja pia ameonya kuwa gharama za huduma za afya zinaendelea kuongezeka duniani kwa kasi kubwa kuliko mfumuko wa bei wa kawaida, akisisitiza umuhimu wa kupanua huduma za bima na kuimarisha mifumo ya kinga ya afya ili kuhakikisha huduma za afya zinabaki kuwa nafuu na endelevu kwa waajiri na wafanyakazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa CEO Roundtable of Tanzania, Santina Benson amesema sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kusaidia vipaumbele vya afya vya taifa kupitia programu za afya mahali pa kazi, bima za afya na ushirikiano unaoimarisha mfumo mzima wa afya.