Kigoma. Majeruhi walionusurika katika ajali ya boti iliyouwa saba, wakiwemo watumishi wanne wa idara ya afya mkoani Kigoma, wamesimulia mkasa mzima hadi kutokea kwa tukio hilo.
Ajali hiyo, ilitokea Machi 13, 2026 katika Kijiji cha Kalalangabo ndani ya Ziwa Tanganyika, saa 2 asubuhi na mwili wa mtu mmoja hadi sasa bado haujapatikana.
Majeruhi hao, wametoa simulizi hizo leo, Jumapili Machi 15, 2026, walipozungumza na Mwananchi wakiwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Mmoja wa manusura wa ajali hiyo, ambaye ni Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Msimba, Lawi Philemon, amesema walianza safari vizuri asubuhi ingawa kulikuwa na hali ya upepo na dalili ya mvua.
Walipotembea kwa umbali kidogo, amesema walikumbuka kuwa kuna mtu wamemwacha nchi kavu ndipo mratibu wa safari alipompigia simu na kumwambia achukue usafiri wa pikipiki ili wakutane naye katika kijiji cha Kalalangabo kuendelea na safari.
“Akamwambia dereva wa boti naye akasema achukue bodaboda ili tuweze kukutana naye kijiji cha Kalalangabo na ndipo tuweze kuendelea na safari yetu,” amesema Philemon.
Wakiwa njiani, amesema kulikuwa na mawimbi na mvua iliyoambatana na radi, baada ya kufika katika kijiji cha Kalalangabo dereva akawa anataka kutupa nanga ili kuegesha boti.
Amesema nanga ilionekana ndoto akabadilisha na kufunga kubwa ili baada yah apo wote walijikuta wamezama ziwani.
“Baada ya kufika eneo hilo dereva alitupa nanga ili tuweze boti letu liweze kusimama lakini baada ya muda aliona ni ndogo hivyo ilimlazimu kufunga nanga kubwa na kuitupa ziwani, kitendo cha kutupa ile nanga kubwa ziwani tulipinduka moja kwa moja na tukajikuta ziwani,” amesema.
Baada ya kuzama, amesema walipambana kuokoa uhai wao na kwa kuwa mawimbi yalikuwa makubwa, walijikuta wakipigizwa kwenye kuta za ziwa.
“Nilijikuta nakunywa maji ya ziwa na kupoteza fahamu lakini sauti ya mwisho niliyoisikia ilikuwa inasema na huyu ni mzima tumchukue na baada ya hapo sikujua kinachoendelea,” amesema.
Manusura mwingine, Jesca Dabanga, amesema wakati wamefika kwenye kituo ili kumchukua mtumishi mwenzao ndipo mawimbi yalipoongezeka.
“Ninachokumbuka madereva wa boti walijitahidi kutia nanga kwenye maji ili kusimama, wakati anaweka kubwa tukapinduka,” amesema.
Anachokikumbuka, amesema ni sauti za kuitana majina wakiwa ndani ya maji na kuulizana uko wapi na kuanza kushikana na kuomba Mungu huku wakiwa na matumaini ya kuokolewa na alishangaa baada ya muda kuona kimya na watu aliokuwa nao ndani ya maji hawaongei tena.
“Baada ya muda nilishangaa mbona watu hawaongea tena na nikiangalia kama niko peke yangu, sina msaada na wenzangu wameenda wapi, kila nikijaribu kwenda huku naona giza huku giza ni maji tu ndo ninayoyaona ikabidi nisimame hapo hapo nikiwa na boya langu maana nilikuwa sina cha kufanya, nimekuja kushtuka naskia mlio wa gari na nikahisi nipo kwenye gari,” amesema.
Mratibu wa Huduma za Tiba Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni, Yusuph Yagasa, amesema walipokea watu waliokuwa wamepata ajali ya boti ndani ya Ziwa Tanganyika na watatu walikuwa katika hali mbaya kutokana na kunywa maji na mafuta.
Wagonjwa hao, amesema walipatiwa matibabu ya haraka na baadaye waliwawekwa wodini kwa ajili ya uangalizi wa karibu na matibabu zaidi.
Ameeleza tayari wagonjwa wote watatu wamesharuhusiwa kutokana na hali zao za afya kuimarika.
Katika ajali hiyo watu saba walipoteza maisha ambao ni pamoja na Muuguzu msaidizi, Paul Luvanda(29),Katibu wa afya, Rachel Msalila(28), Tabibu wa Kinywa na Meno, Joyce Kandole(29), Mfamasia, Winny Nyabusani (31).
Wengine ni Amos Sika (33), Tabibu ambaye hadi sasa mwili wake bado haujaonekana. Pia, walikuwepo waliokuwa wasaidizi wa shughuli ya kuhamasisha Bima kwa Afya kwa Wote, Erick Dabanga, Omary Mkalima na Geofrey Aron.