MPANDA- KIGOMA KUUNGANISHWA KWA LAMI

******

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imedhamiria kuufungua mkoa wa Katavi kwa barabara za lami ili kuchochea uchumi wa mikoa ya kanda ya magharibi.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi Dkt. Nchemba amesema nia ni kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi ili kukuza uchumi wa wananchi katika mwambao wa ziwa Tanganyika.

Nae Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema barabara ya Vikonge – Mishamo km 52 na Mishamo – Uvinza km 92, zitajengwa kwa lami ili kuunganisha mkoa wa Katavi na Kigoma kwa barabara ya lami. 

Eng. Kasekenya amesema nia ya Serikali ni kuufanya mkoa wa Katavi kuwa wa kiuchumi na kiungo cha mikoa ya kanda ya magharibi.

” Mhe. Waziri Mkuu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema tuufungue mkoa wa Katavi pande zote ili kuchochea ukuaji wa biashara na matumizi ya bandari ya Karema”, amesisitiza Eng. Kasekenya.

Amezitaja barabara nyingine ambazo ziko kwenye maandalizi ya ujenzi mkoani humo kuwa ni Inyonga – Majimoto -Kibaoni km 162, Inyonga – Ilunde-Kishero-Kitunda hadi Chunya Makongolosi km 360 , Sitalike-Kibaoni km  71.8 na Kagwira- Karema ambazo ujenzi wake unaendelea.

Naibu Waziri wa Ujenzi amewahakikishia wananchi wa Kamsisi Wilayani Mlele wanaopisha upanuzi wa mizani kuwa malipo yao yako hatua za mwisho.