Diarra njia nyeupe, apewa mmoja mpya kikosini

INAWEZEKANA unafuatilia matokeo tu ya Simba, Yanga na Azam FC namna zinavyokimbizana msimu huu, lakini kuna vita nyingine ngumu ipo kwenye mabao yao kwani makipa wa timu hizo wanatoana jasho kwa ubora mkubwa huku Djigui Diarra akionekana hana mpinzani wa karibu kwa sasa.

Diarra mmoja kati ya makipa bora kuwahi kutokea kwenye ligi yetu, msimu uliopita alishika nafasi ya pili kwa wale ambao walimaliza wakiwa na clean sheet nyingi baada ya kuwa nazo 17, mbili nyuma ya kinara Moussa Camara wa Simba.

Lakini sasa mambo yanaonekana kubadilika na inavyoonekana ni Diarra anaweza kujitangazia ufalme huo mapema tu kutokana na kasi ambayo amekuwa akienda nayo, lakini akikosa mpinzani sahihi kutokana na Camara kuumia na kuondolewa kwenye usajili wa Simba.

Bingwa mtetezi, Yanga hataki utani kwenye zile mechi za heshima. Golini kwao anatangulia Diarra ambaye anadaka mechi za Ligi Kuu Bara huku zile za Kombe la Shirikisho la CRDB akiwaachia wenzake Aboutwalib Mshery na Hussein Masalanga.

Kwenye mechi tano zilizopita za Ligi Kuu Bara kabla ya jana kucheza dhidi ya Azam, Diarra hajaruhusu bao wakati Yanga ikishinda nne na sare moja dhidi ya Simba iliyomalizika kwa 0-0. Matokeo ya mechi hizo zingine ni Namungo 0-1 Yanga, Yanga 5-0 JKT Tanzania, Singida Black Stars 0-3 Yanga na Tanzania Prisons 0-1 Yanga.

Kabla ya jana, Yanga ikiwa imecheza mechi 13 za Ligi Kuu Bara hata nusu hawajafika, Diarra ameruhusu mabao mawili pekee kwenye ligi ikiwa ni dhidi ya KMC wakati Yanga ikishinda 4-1 na Yanga 3-1 Dodoma Jiji lakini akiwa kinara kwa clean sheet baada ya mechi hizo kumaliza michezo nane bila kuruhusu bao, huku Aishi Manula na Djibrill Kassali ambao wanaonekana kuwa wapinzani wake wa karibu kila mmoja akiwa na clean sheet nne tu kwenye ligi hadi sasa.

Hata hivyo pamoja na ubora wake ukuta wa mabeki ambao wanamlinda Diarra msimu huu una sura mpya moja tu ya ujio wa beki wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye kwa sasa ndiye anapata nafasi zaidi ya Chadrack Boka aliyekuwa chaguo la kwanza msimu uliopita tofauti na ilivyo kwa wapinzani wao wakubwa Simba.

Mabeki wengine wanaopata nafasi ya kumlinda Diarra ni Israel Mwenda upande wa kulia, wakati mabeki wa kati wakiwa Dickson Job na Ibrahim Bacca ambao kama yakifanyika mabadiliko basi nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto huingia.

Job ambaye ameumia na hataweza kucheza tena msimu huu, ina maana kwamba kwa sasa Diarra atakuwa akilindwa na Mwamnyeto na Bacca huku Mghana Frank Assinki akisubiri nje.

Vita ya ubora kwa Diarra haitakuwa rahisi hata kama Moussa Camara hatakuwepo kwani Simba imemshusha kipa mwingine Kassali ambaye naye namba zake zimeanza kuonyesha moto wake kwenye kulilinda lango la wekundu hao lakini ni ngumu kumfikia kutokana na idadi ya mechi zake.

Kassali amefanikiwa kucheza mechi tano za ligi tangu atue kupitia usajili wa dirisha dogo, lakini ndani ya mechi hizo naye ameruhusu bao moja tu, alilofungwa hivi karibuni pale Uwanja wa Airtel na mshambuliaji Mossi Nduwumwe, Simba ikishinda 2-1 dhidi ya Singida Black Stars.

Kabla ya hapo Kassali aliiongoza Simba kushinda mechi tatu na kulazimisha sare moja dhidi ya Yanga, na zote akitoka salama bila wavu wake kutikiswa, akionyesha kwamba hata kama Moussa Camara hayupo lakini Simba itaendelea kubaki salama chini yake.

Kassali wakati mwenyewe akiwa mgeni, ukuta wake una mabadiliko mawili tofauti na msimu uliopita ambapo upande wa kulia nahodha mkuu Shomari Kapombe ameendelea kuwa chaguo la kwanza, kama vile beki Rushine De Reuck akisalia akicheza sambamba na ingizo jipya Olivier Toure huku Nickson Kibabage akiwa kushoto ambapo wawili hao wameingia kwenye usajili wa dirisha dogo.

Simba nako kuna mtu mpya baada ya Moussa Camara kuwa majeruhi, imemleta Kassali kutoka Niger  ambaye zile mechi zote kubwa zipo chini yake, huku zile za shirikisho akimwachia Hussein Abel.

Kule Azam nako kuna mbabe amerejea, Aishi Manula ambaye fasta tu balaa lake limeanza kuonekana akionyesha ubora mkubwa kwenye kulilinda lango la matajiri hao wa Chamazi akiwa na mechi nne hadi sasa bila kuruhusu bao.

Kwenye mechi sita za Azam zilizopita ipo hivi: benchi la ufundi la timu hiyo linafanya mabadiliko ya makipa wa kikosi hicho ambapo Manula amegawana mechi tatu na Zuber Foba.

Kwenye mechi tatu ambazo Manula amedaka za mwisho ameruhusu mabao mawili kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Pamba Jiji uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, huku Foba akitoka salama kwenye mechi hizo bila kuruhusu bao lolote.

Azam imeruhusu mabao manne tu kabla ya mchezo wa jana, lakini ni ngumu kwao kumfikia Diarra kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya makipa wao.