STAA wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Shaban Kisiga aliwahi kusema kipaji kinakijua kipaji kingine hata kama wachezaji wanacheza timu tofauti.
Hali hiyo imetokea kwa winga wa Azam anayecheza JKT Tanzania kwa mkopo, Tepsi Evance ambaye jina la utani wanamwita Okello.
Kauli ya Kisiga ilitokana na kiungo wa zamani wa Yanga, Haruna Niyonzima aliyewahi kukiri moja ya mastaa Tanzania wenye vipaji vikubwa ni Kisiga ambaye hakuwahi kucheza naye timu moja.
Naye Kisiga alipoulizwa, alijibu: “Kipaji kinajua kipaji mwenzake, binafsi Niyonzima ni kati ya kipaji kikubwa nilichowahi kukishuhudia katika Ligi Kuu Bara, labda jambo wasiyolijua wengi wachezaji tunajuana, haijalishi anatoka timu gani.”
Hivi karibuni, Tepsi alisema kati ya vipaji vikubwa alivyowahi kuviona ni Allan Okello anayecheza Yanga akijiunga na kikosi hicho dirisha dogo la Janauri 2026 akitokea Vipers ya Uganda.
Aliifafanua kauli yake akisema: “Wengi waliomjua Okello baada ya kujiunga na Yanga, wanadhani najiita jina hilo baada ya mchezaji huyo kuja nchini, ukipita katika ukurasa wangu wa instagram utakutana na picha yake ina jezi la jina langu akiwa na timu ya KCCA, kwani na yeye alikuwa ananikubali sana.
“Timu ya KCCA ya Uganda ilikuja kucheza Uwanja wa Chamanzi dhidi ya Mtibwa, mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kati ya wachezaji walioonesha kiwango cha juu ni Okello. “Wakati anacheza nikawaita marafiki zangu kina Lusajo Mwaikenda na Novatus Dismas tulikuwa jukwaani wakati huo tulikuwa katika kambi ya timu ya taifa ya vijana, nikawaambia Okello ni mchezaji mzuri sana, wakasema au kwa sababu umemuona anacheza mguu wa kushoto, hatukukaa sawa akafunga bao la pili, mechi ikamalizika kwa mabao Mtibwa 1-2 KCCA, ilikuwa 2018, pale ndipo tulipofahamiana.”
Tepsi aliyezaliwa Desemba 30, 2022 (umri wa miaka 23), alisema ukiacha Okello ambaye hadi sasa amefunga bao moja la ligi akiwa na Yanga, wapo wachezaji wengi wenye vipaji anaowajua.
