Chama la Samatta hatarini kushuka daraja

KLABU ya Le Havre AC anayoichezea mshambuliaji wa Kitanzania, Mbwana Samatta iko kwenye nafasi mbaya na hatari ya kushuka daraja kama haitashtuka mwishoni.

Le Havre iko nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi, nafasi ambayo siyo salama kutokana na tofauti ndogo ya pointi na timu zinazopigania kubaki kwenye ligi hiyo.

Timu hiyo imekusanya pointi 26 tofauti ya pointi saba na Auxerre iliyopo nafasi ya 16 na pointi 19 zikiwa zimepigwa raundi 25.

Ratiba ya mechi zilizosalia inaonyesha Le Havre bado ina kazi kubwa, ikianza na mchezo dhidi ya Olympique Lyonnais. Katika mchezo wa kwanza wa msimu, Lyon iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Le Havre, hivyo mchezo huo unaweza kuwa kipimo kingine kigumu kwa chama la Samatta.

Baada ya hapo Le Havre itacheza na Paris FC kabla ya kukutana na AJ Auxerre, mechi ambazo Le Havre inaweza kuambulia kitu.

Mechi nyingine dhidi ya OGC Nice, Angers SCO, FC Metz, Lille OSC, Olympique de Marseille na FC Lorient.

Kwa ushindani wa ligi ulivyo mechi dhidi ya Paris FC, Auxerre, Angers na Metz hapa Le Havre inaweza kuchukua pointi ili kujiweka salama kwenye hatari hiyo.

Samatta hajafunga bao hadi sasa wala kutoa asisti lakini amekuwa na wastani mzuri wa kushambulia jambo liliendelea kumpa nafasi ya kuanza na kucheza kikosini hapo.

Hata hivyo bado anayo nafasi ya kuisaidia chama hilo itakumbukwa msimu uliopita alipokuwa na PAOK ya Ugiriki hakuanza vizuri lakini mwishoni alikuwa na muendelezo mzuri wa kufunga.

Alicheza mechi 12 alipofunga mabao manne na asisti moja, msimu wake wa kwanza klabuni hapo 2023/24 alicheza mechi 19 akiweka kambani mabao mawili.